Na Mwandishi Wetu
MKUU wa mkoa wa Mwanza, Eng.
Everisti Ndikilo, hivi karibuni amezindua rasmi msimu wa ununuzi wa pamba wa
2014/15 katika kijiji cha Isole Wilayani Sengerema.
Wadau wa msingi wa zao la
pamba ambao ni pamoja na wanunuzi wa Pamba kupitia Chama cha Wafanyabiashara wa
Pamba Tanzania (TCA), Wakulima kupitia Chama cha Wakulima wa Pamba Tanzania (TACOGA)
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo Chakula na Ushirika na Bodi ya Pamba pamoja
na wadau wengine walikutana mjini Dodoma hivi karibuni (Juni 13, 2014) kujadili
na kukubaliana juu ya bei elekezi (indicative price) ya kununulia
pamba kwa msimu 2014/15.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa
Bodi ya Pamba nchini Tanzania (TCB), Gabriel Mwalo, alisema kuwa wadau
walikubaliana bei elekezi ya kununua na
kuuza pamba (indicative price) msimu huu kuwa Shilingi za Kitanzania 750/=. kwa kilo moja ya
pamba mbegu.
“Bei elekezi (indicative
price) kwa msimu husika inawekwa kwa lengo la kumlinda mkulima wa pamba asipate hasara kutokana na
baadhi ya wafanyabiashara kununua pamba kwa bei ndogo kuliko ilivyo katika soko
la kimataifa. Wanununuzi wa pamba wanatakiwa kununua pamba kwa bei iliyo juu ya
bei ya elekezi na si vinginevyo. Mnunuzi atakayenunua pamba kwa bei chini ya bei
elekezi atakuwa anavunja sheria na taratibu zinazosimamia zao la pamba,” Bw.
Mwalo alisema.
Aidha, Bw. Mwalo, alisema
kuwa bei hiyo ni elekezi kwa maana kwamba, wakulima hawatakiwi kuuza pamba
chini ya bei hii, na wakati huo huo wanunuzi wanatakiwa kutonunua pamba kwa bei
iliyo chini ya bei husika.
“Ni matarajio yetu kwamba wadau
wote wanohusika watazingatia utaratibu huu ambao umewekwa kisheria, kwani
kufanya kinyume ni kosa chini ya sheria ya pamba namba 2 ya mwaka 2001,”
alisema.
Aliongeza kuwa mchakato wa
kupata bei elekezi (indicative price) unazingatia vigezo vingi ili kulinda maslahi
ya wadau wote ambao kimsingi ni wakulima na wanunuzi wa pamba.
“Kwa vile Pamba ya Tanzania
kwa kiasi kikubwa inauzwa nje ya nchi ikiwa ghafi, kigezo cha kwanza kabisa kinachotumika
katika kuandaa Bei elekezi ni hali ya bei ilivyo katika soko la dunia kwa
wakati huo,” alisema.
Vigezo vingine ni gharama za
uzalishaji wa pamba kwa mkulima, gharama za ununuzi, usafirishaji na uchambuaji
wa pamba, mchango wa Mfuko wa Wakfu wa Kuendeleza zao la pamba na kodi za Serikali
(Ushuru wa Halmashauri za Wilaya).
“Wakulima kupitia TACOGA
wanaandaa gharama za uzalishaji wakati wanunuzi wa pamba chini ya TCA
wanakokotoa bei kwa upande wao. Serikali kama msimamizi wa sheria na taratibu,
haifanyi maamuzi juu ya Bei elekezi bali wadau (wakulima na wanunuzi)
wanakubaliana wenyewe na serikali kupitia Bodi ya Pamba inashauri kwa kutoa
taarifa ili kupata muafaka wenye manufaa kwa pande zote mbili,” alisema.
Pamba ni zao la biashara la
msimu ambalo linazalishwa katika mikoa 15 nchini.; Mikoa hii imegawanyika
katika Kanda mbili ambazo ni Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa ya Mwanza,
Shinyanga, Simiyu, Geita, Tabora, Mara, Kigoma, Singida na Kagera, wakati Kanda
ya Mashariki inajumuisha mikoa ya Morogoro, Iringa, Pwani, Tanga, Kilimanjaro
na Manyara.
Kanda hizi mbili
zinatofautia kwa kiasi kikubwa katika hali ya udongo, mtawanyiko wa mvua,
magonjwa ya pamba na aina ya wadudu wanapatikana katika maeneo husika na kuanza kwa misimu ya
kilimo.
Msimu wa kilimo/kupanda
pamba kwa Kanda ya Magharibi unaanza katikati ya mwezi Novemba wakati Kanda ya
Mashariki msimu wa kupanda pamba unaanza mwanzoni mwa mwezi Februari.
Kutokana na tofauti hizi
uvunaji na uuzaji wa pamba unaanza katika vipindi tofauti hivyo kulazimu Tasnia
ya Pamba kuweka utaratibu wa kuzindua msimu wa ununuzi mwezi wa Juni kwa Kanda ya Magharibi na
Septemba kwa Kanda ya Mashariki. Uzalishaji wa pamba msimu huu unakadiriwa kuwa
tani 250,000 za pamba mbegu.


No comments:
Post a Comment