Mkurugenzi Msaidizi Urejeshaji Mikopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Bw. Robert Kibona akitoa mada wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini mjini Dodoma leo.
Baadhi ya washiriki wa mkutano mkuu wa mwaka wa Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini wakifatilia mada mjini Dodoma leo.
Na Happiness Shayo-Utumishi
WAAJIRI wote nchini wanaoshindwa kuwasilisha taarifa za watumishi wao
waliosoma kwa mikopo inayotolewa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu nchini
watashitakiwa mahakamani kwa
kushindwa kuwasilisha taarifa za watumishi
hao katika Bodi hiyo.
Mkurugenzi Msaidizi Urejeshaji
Mikopo, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Bw. Robert Kibona ameyasema hayo leo, katika mkutano mkuu wa mwaka
wa Wakurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu Serikalini mjini Dodoma.
“Mpaka sasa tumewachukulia hatua jumla ya waajiri watano ambao
wameshindwa kuwasilisha taarifa za watumishi wao wanaodaiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu” alisema
Bw.Robert.
Alisema, mwajiri atakayeshindwa kutoa taarifa za wahitimu wa elimu ya
juu katika Bodi kwa wakati atatakiwa kulipa faini ya shilingi milioni saba au
kutumikia kifungo kisichopungua miezi 12 au vyote kwa pamoja.
Aidha,Bw. Robert alisema kuwa mpaka sasa takribani waajiriwa 18
wamefikishwa mahakamani kwa kosa la kushindwa kurejesha mikopo hiyo.
Bw.Robert alifafanua kuwa ili kufanikisha zoezi la urejeshaji mikopo kutoka kwa wadaiwa, Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu iko
mbioni kutunga sheria na mifumo mbalimbali ya kuwadhibiti wadaiwa hao.
“Tunatengeneza sheria ambazo zitawazuia wadaiwa wa mikopo ya elimu ya
juu kupata hati ya kusafiria nje ya nchi au kibali cha kusafiri hadi
atakapowasiliana na Bodi.”
Pia,alisema mhitimu atakayeshindwa kulipa mkopo taarifa zake
zitatangazwa kwenye vyombo vya habari na kwenye taasisi za mikopo ili asipate
huduma yoyote ya kifedha.
Naye, Msaidizi wa Mtendaji Mkuu Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu Bi. Veronica
Nyahende amewataka wahitimu wa elimu ya juu nchini kutumia elimu waliyonayo
kujiajiri wenyewe badala ya kusubiri kuajiriwa.
Alisema changamoto ya kurejesha mikopo ni kubwa kwa upande wa wahitimu wa elimu ya juu ambao hawana
kazi ama hawajajiajiri.
“Changamoto iliyopo ni wahitimu kushindwa kulipa mikopo hiyo kutokana na
kuwa na kipato cha chini ama kukosa ajira.”
Alisema Bodi imeingia mkataba na kampuni zitakazokusanya mikopo kwa walionufaika
na mikopo hiyo na kushindwa kuilipa .
Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu iko katika mchakato wa kuelimisha umma na
watendaji wakuu Serikalini ili kuhakikisha wanawasilisha taarifa za watumishi
wao wanaodaiwa mikopo hiyo.
No comments:
Post a Comment