TANGAZO


Friday, May 2, 2014

MAKAMU WA RAIS DKT. BILAL KUZINDUA MBIO ZA MWENGE WA UHURU 2014 LEO

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohamed Gharib Bilal akivishwa skafu na mmoja wa Skauti mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege wa Bukoba.Kushoto ni Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Gharib Bilal (kushoto) akisalimiana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bi. Sihaba Nkinga alipowasili mjini Bukoba mkoani Kagera mapema leo.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Gharib Bilal (kushoto) akisalimiana na Katibu mstaafu wa CCM mkoa wa Kagera Bw. Faustine Kamaleki mara baada ya kuwasili uwanja wa ndege mjini Bukoba tayari kwa uzinduzi wa Mbio za Mwenge.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal akifurahia burudani ya ngoma za asili kutoka katika kundi la sanaa la Kakau Band mara baada ya kuwasili katika uwanja wa ndege mjini Bukoba.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali mstaafu Fabian Masawe (kulia) akitoa taarifa ya hali ya mkoa wa Kagera na maandalizi ya uzinduzi wa mbio za Mwenge wa Uhuru 2014 kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara akitoa taarifa kwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal kuhusu kukamilika kwa maandalizi ya uzinduzi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2014.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara (kushoto) akizungumza jambo na makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Mohammed Gharib Bilal Ikulu ndogo mjini Bukoba. (Picha zote, Habari na Frank Shija na Aron Msigwa)
Na Waandishi wetu
2/5/2014, Bukoba, Kagera.
MAKAMU wa Rais  Dkt. Mohammed Gharib Bilal  leo, atazindua Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa kwa mwaka 2014  katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba, mkoani Kagera ambapo  jumla  ya miradi 69 yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 69 itatekelezwa.

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Kanali Mstaafu Fabian Masawe ameeleza kuwa Mwenge wa Uhuru ukiwa mkoani humo utakimbizwa katika wilaya 7  za Biharamulo, Bukoba, Karagwe, Kyerwa, Missenyi, Muleba na Ngara na kufafanua  kuwa mkoa wake kwa  kushirikiana na Wizara ya Habari ,Vijana,Utamaduni na Michezo na ile ya Uwezeshaji, Ajira, Wanawake  na Watoto ya Zanzibar umekamilisha maandalizi ya uzinduzi wa  mbio hizo.

Amesema kwa sasa mkoa wa Kagera umepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa programu mbalimbali za maendeleo ya wananchi zikiwemo za uwekaji wa mkazo kwa wananchi katika masuala ya kilimo, ulinzi na usalama, mipango ya utunzaji wa mazingira , utekelezaji wa mkakati wa kuinua kiwango cha elimu inayotolewa katika mkoa huo kwa kuongeza miundombinu ya shule ikiwemo ujenzi wa maabara ili kuinua viwango vya ufaulu.

Kuhusu utunzaji wa mazingira hasa utoaji wa vibali  vya ukataji miti hususan maemeo ya mapori ya akiba yaliyo katika mkoa wake amesema kuwa  mkoa unaendelea kuwasiliana na mamlaka husika ili kuhakikisha kuwa mapori ya akiba ya mkoa huo yanaendelea kulindwa na kuheshimiwa.

Ameeleza  kuwa ili kuhakikisha kuwa mkoa wa Kagera unaendelea kuwa salama kwa kutokuwa na malumbano baina ya jamii za wakulima  na wafugaji,  serikali inaendelea na zoezi la utambuzi wa mifugo ili kuweka udhibiti wa uharibifu wa Mazingira na ufugaji holela.

Kuhusu uzinduzi wa mbio hizo katika uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba ameeleza kuwa maandalizi kwa ajili ya ufanisi wa kazi hiyo yamekamilika na kutoa wito kwa wananchi kujitokeza kwa wingi katika uzinduzi wa mbio hizo.

“Maandalizi ya shughuli ya uzinduzi wa Mwenge yamekamilika, tumekamilisha ujenzi wa jukwaa kuu, tumewahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi leo pia  wawakilishi kutoka nchi majirani na washirika wa maendeleo kutoa Burundi, Rwanda, Uganda na Korea wanahudhuria sherehe hizi”

No comments:

Post a Comment