TANGAZO


Monday, May 5, 2014

Maalim Seif Shariff aongoza mazishi ya Sheikh Ilunga jijini Dar es Salaam




Katibu Mkuu wa Chama cha Wananchi (CUF), ambaya pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad (katikati), akishiriki mazishi ya Sheikh Ilunga Hassan Kapungu katika Makaburi ya Mwinyimkuu Magomeni jijini Dar es Salaam leo.


Maelfu ya Waislamu wakiwa wamejitokeza kumzika Sheikh Ilunga. (Picha zote na Salmin Said, OMKR)

 Maelfu ya Waislamu wakiwa wamejitokeza kumzika Sheikh Ilunga jijini leo.

Na Hassan Hamad (OMKR).
MALAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad, amewaongoza maelfu ya Waislamu katika mazishi ya sheikh maarufu wa Mkoa wa Mwanza na mwanaharakati wa dini ya Kiislamu marehemu sheikh Ilunga Hassan Kapungu.
 
Sheikh Ilunga amefariki dunia mjini Dar es Salaam na kuzikwa katika makaburi ya Mwinyimkuu Magomeni. 
 
Katika uhai wake sheikh Ilunga Kapungu alikuwa mwanaharakati ambaye mara nyingi alikuwa akiendesha mihadhara ya wazi ya dini ya Kiislamu, ambapo mwishoni mwa mwaka 2013 alikamatwa kwa tuhuma za uchochezi mkoani Tabora na baadaye kuachiwa huru.
 
Kwa mujibu wa taarifa za kimtandao, kabla ya kukamatwa kwake na kuachiwa huru Disemba mwaka 2013, marehemu sheikh Ilunga alikwenda nchini India kwa matibabu baada ya kusumbuliwa na matatizo ya figo pamoja na sukari.
 
Akizungumza katika mazishi hayo  sheikh Basaleh wa Dar es Salaam, amesema marehemu sheikh Ilunga alikuwa mwanaharakati imara na ni mfano mzuri wa kuigwa katika harakati za dini ya Kiislamu.
 
Mazishi yake yameweka historia baada ya maelfu ya waislamu kujitokeza kushiriki kwao, hali iliyopelekea mchanga wa kaburi lake kufukiwa kwa mikono badala ya kutumia mapauro na majembe kama ilivyozoeleka.
 
Masheikh kutoka Mikoa mbali mbali ya Tanzania wameshiriki mazishi hayo akiwemo sheikh Kishki, pamoja na wawakilishi wa Jumuiya ya Uamsho.


No comments:

Post a Comment