Kaganda (kulia) akielezea kwa waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo Jijini Dar Es Salaam namna mabasi hayo yatakavyofanya
safari zake mara awamu ya kwanza ya
mradi huo itakapoanza mapema mwakani , Kushoto ni Afisa Habari wa Idara ya
Habari Maelezo Frank Mvungi.
Meneja uendeshaji wa DART, Bw. Peter Munuo akieleza jambo kwa waandishi wa habari kuhusu faida
za mradi huo ikiwemo kuondoa tatizo la
foleni katika jiji la Dar es Salaam na viunga vyake, mara mradi huo
utakapoanza mapema mwakani. (Picha zote na Georgina Misama)
Na Frank Mvungi- Maelezo
Serikali inatarajia kuanza kutoa huduma za awali
(interim services) katika mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) Kutoka Kimara
mwisho hadi Kivukoni jijini Dar es salaam mwaka 2015 baada ya miundombinu
kukamilika.
Hayo yamesemwa na Meneja Uhusiano wa Wakala wa mabasi
yaendayo haraka (DART) Bw.William Gatambi
wakati wa mkutano na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam.
Gatambi alisema kuwa mara baada ya kukamilika kwa
miundo mbinu ya mradi huo awamu ya kwanza mwishoni mwa mwaka 2014 itasadia
kufanikisha usafiri wenye tija kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam na vitongoji
vyake.
Miundombinu hiyo, inajumuisha barabara ya kilomita
20.9 kuanzia Kimara Mwisho hadi Kivukoni,Barabara ya Kawawa kutoka Morocco hadi
Magomeni na Barabara ya Msimbazi hadi eneo la Gerezani Kariakoo.
Aliongeza kuwa
ina vituo vidogo 27,vituo vikuu vitano, vituo mlisho vine na karakana mbili.
Pia inajumuisha njia za waenda kwa miguu na baiskeli.
Akifafanua Gatambi alisema mradi wa majaribio utaanza
na mabasi 20 yatakayokuwa na uwezo wa kuchukua abiria kati ya 145 hadi 160 kwa
wakati mmoja hali itakayosaidia kuondoa kabisa kadhia ya usafiri kwa wakazi wa
jiji la Dar es salaam.
Aidha, katika mradi huo wa majaribio Gatambi amesema
kutakuwa na mabasi mengine 10 yenye uwezo wa kuchukua abiria kati ya 50 na 60
ambayo yatatumika kuchukua abiria kutoka pembezoni mwa jiji la Dar es salaam
kuja katika vituo vikuu vya mabasi yaendayo Haraka.
Kwa upande wakeMeneja Usimamizi wa Barabara wa DART
Mhandisi Mohamed Kuganda amesema mradi huo utasaidia kuondoa tatizo la foleni
Jijini Dar es salaam na kuwafanya wananchi kupata huduma ya usafiri yenye
kukidhi viwango vya Kimataifa.
Pia Kuganda alisema DART kwa kushirikiana na
Halmashauri za Jiji la Dar es salaam inafanya maandalizi ya kuboresha barabara
mlisho (feeder roads) katika maeneo yatakayotumiwa na mabasi mlisho.
Katika mradi wa mabasi yaendayo haraka kutakuwa na
Vituo Vikuu (terminals) vitano 5 katika, maeneo ya Kimara, Ubungo, Morocco, Kariakoo
na Kivukoni ambapo vituo hivi ndiko mabasi yatakapokuwa yanaanzia na kumalizia
safari kubadilishana abiria kati ya njia kuu na njia mlisho (feeder roads)
ambapo vituo hivyo vikubwa vinatoa nafasi ya kuweza kuanzishwa kwa huduma
muhimu kwenye vituo hivyo kama maeneo ya kukatia tiketi na vyoo.
No comments:
Post a Comment