TANGAZO


Wednesday, April 2, 2014

Rwanda inawatafutia haki waliouawa


Mafuvu yaliobaki baada ya mauaji ya halaiki Rwanda
Serikali ya Rwanda imesema kuwa ni asilimia mbili tu ya washukiwa wakuu wa mauaji ya kimbari ambao wameshakamatwa na kufikishwa mbele ya sheria.
Hii ni licha ya kusambaza hati zaidi ya 193 katika mataifa 30 kwa ajili ya kuwatia nguvuni washukiwa.
Mwendesha mashitaka ngazi ya taifa akiwa pia mkuu wa tume ya taifa inayofuatilia na kuwasaka washukiwa wakuu wa mauaji ya kimbari waliokimbilia nchi za nje,Jean Bosco Mutangana amewaambia waandishi wa habari kuwa ni hatua kubwa ambayo Rwanda imefikia katika malengo yake ya kutaka washukiwa wa mauaji ya kimbari wafikishwe mbele ya sheria.Afisa mwandamizi anayehusika na ufuatiliaji wa kesi hizo amesema kuwa pamoja na hayo serikali inapongeza hatua za baadhi ya mataifa ya Ulaya kuonyesha ushirikiano katika kuhakikisha washukiwa hao wanafuatiliwa kisheria.
Amesema kuwa tangu serikali kuunda tume mwaka 2007 ikiwa na jukumu la kufuatilia na kuwasaka washukiwa hao wakuu kwa makosa ya kupanga na kutekeleza unyama ,zilisambazwa hati 193 katika mataifa 30 duniani.
Mutangana amebaini ni asilimia mbili tu ya hati hizo ambazo zilitekelezwa ambapo baadhi wamekwisha fikishwa mahakamani na kupata hukumu na wengine wakiendelea na kesi.
Watutsi wengi waliuawa pamoja na watutsi wenye msimamo wa kadri-hizi ni juhidi za kupatanisha jamii hizo mbili
Ameshukuru mataifa ya ulaya na Afrika kwa kuonyesha nia ya ushirikiano katika juhudi za kuwafikisha washukiwa hao mbele ya sheria na akasema serikali ina imani na hatua ya Ufaransa na mataifa mengine kwa kuruhusu sheria kufuata mkondo wake.
Kulingana na kiongozi huyo katika kitengo cha mwendesha mashitaka mkuu,Tume hiyo hujulikana kama 'Genocide fugitive tracking Unit,'' na kwamba ilikabidhi hati hizo kwa polisi ya kimataifa ama Interpol.
Mutangana,amejizuia kulaumu moja kwa moja mataifa ambayo yalitupilia mbali mwito wa ushirikiano na mahakama ya kimataifa kwa ajili ya Rwanda kuwasaka washukiwa hao ambao walipewa hifadhi kwenye mataifa hayo wengi wao wakiwa katika mataifa ya Afrika na Ulaya.
Aidha amebaini kuwa hatua ya vyombo vya kisheria kuwa na imani na Rwanda kwake ilionekana kuwa kama maajabu.
Afisa huyu amekuwa akielezea vyombo vya habari sura ya sheria kuambatana na watuhumiwa wakuu wa mauaji ya kimbari wakati Jumatatu wiki ijayo kutaadhimishwa kwa mara ya 20 mauaji ya kimbari dhidi ya jamii ya watutsi.
Zaidi ya hayo amesema kuwa si ajabu kesi za mauaji ya kimbari zikachukua miongo kadhaa kwa kulinganisha na zile za wanazi dhidi ya mayahudi ambazo hadi sasa ni hai.

No comments:

Post a Comment