TANGAZO


Friday, April 4, 2014

Maadhimisho ya Siku ya afya Duniani Aprili 7, Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Rashid atoa tamko

Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid akizungumza na waandishi wa habari, mjini Dodoma leo, wakati alipokuwa akitoa tamko kuhusu maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani, inayoadhimishwa Aprili 7 duniani kote. Kulia ni Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ndani, Dodoma, Zainab Chaula. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Waandishi wa habari, wakimsikiliza Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, wakati alipokuwa akitoa tamko kuhusu maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani, inayoadhimishwa Aprili 7 duniani kote. 
Wapiga picha na waandishi wa vyombo mbalimbali vya habari, wakichukua maelezo ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, wakati alipokuwa akitoa tamko kuhusu maadhimisho ya Siku ya Afya Duniani, inayoadhimishwa Aprili 7 duniani kote.


TAMKO LA WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII MHE.  DKT. SEIF SULEIMAN RASHID (MB). KUHUSU MAADHIMISHO YA SIKU YA AFYA DUNIANI.

Ndugu wananchi,
Tarehe 7 Aprili  ya kila mwaka ni siku ambayo imeridhiwa na nchi zote  wanachama wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Tanzania ikiwa mojawapo, kuadhimisha Siku ya Afya Duniani.

Katika kuadhimisha siku hiyo, Shirika la Afya Duniani linatoa  kaulimbiu yenye  ujumbe maalum  ambao unalenga  kuhamasisha  na kuelimisha jamii juu ya suala mojawapo muhimu na lenye manufaa kiafya kwa nchi zote wanachama.

Ndugu wananchi,
Kaulimbiu  ya  Maadhimisho ya  Siku ya  Afya  Duniani mwaka  huu  wa 2014 ni : Jikinge na  ‘magonjwa yanayoenezwa na wadudu’ (vector borne diseases) ujumbe unaombatana na kauli mbiu hii ni ‘Mng’ato Mmoja Madhara Makubwa’  (Single Bite, Big Threat). Kaulimbiu hii inalenga kuhamasisha wadau wote na jamii kwa ujumla  kutambua ukubwa wa tatizo la magonjwa yanayoenezwa na wadudu kitaifa na kimataifa, visababishi vyake, madhara na umuhimu wa kubadili tabia na mienendo hatarishi ili kudhibiti na kujikinga na magonjwa haya.

Ndugu wananchi,
Wadudu wanaoeneza magonjwa haya hapa nchini ni pamoja na mbu, aina ya anopheles ambao hueneza  malaria, matende na mabusha; mbu aina ya Aedes ambao hueneza ugonjwa wa chikungunya, homa ya dengue na homa ya manjano. Mbu wa aina ya Culex pamoja na kuwa na tabia ya usumbufu, pia hueneza ugonjwa wa matende na mabusha. Viroboto hueneza ugonjwa wa tauni, mbung’o hueneza ugonjwa wa malale na papasi hueneza homa ya papasi.   
Magonjwa mengine yanayoenezwa na wadudu ni kuhara,vikope na usubi yanayoenezwa na nzi.

Ndugu Wananchi,
Takwimu zinaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya watu duniani wako hatarini kuambukizwa na magonjwa yanayoenezwa na wadudu.  Aidha, magonjwa haya yanaua watu zaidi ya milioni moja kila mwaka duniani.

Nchini Tanzania, magonjwa yanayoenezwa na wadudu bado ni tatizo kubwa kutokana na usugu wa vimelea dhidi ya dawa na viuatilifu, mabadiliko ya tabia nchi, mazingira hatarishi ikiwemo kiwango cha chini cha matumizi ya vyoo bora, usafi duni wa mazingira ambao hujenga mazingira rafiki kwa mazalia ya wadudu na matumizi ya maji yasiyo safi na salama.

Magonjwa yanayoenezwa na wadudu huchangia kupunguza nguvu kazi katika ngazi ya familia, jamii na taifa kwa ujumla na hivyo kuzorotesha maendeleo na kuongeza kasi ya umasikini.

Ndugu wananchi,
Ningependa kuchukua nafasi hii kuelezea juhudi za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika kukabiliana na baadhi ya magonjwa yanayoenezwa na wadudu hapa nchini.

Ugonjwa wa malaria bado ni tatizo kubwa nchini ingawa takwimu zinaonesha kupungua kwa ugonjwa huu kutoka asilimia 18.8 mwaka 2008 hadi asilimia 10  mwaka 2012.  Hadi sasa idadi kubwa ya wagonjwa wanaohudhuria kwenye vituo vya kutolea huduma za Afya ni wagonjwa wa malaria. Aidha, malaria huathiri zaidi kina mama wajawazito na watoto chini ya umri wa miaka mitano. Ugonjwa huu pia unaongoza kwa kusababisha vifo katika jamii.

Wizara kwa kushirikiana na wadau inaendelea kuratibu na kusimamia udhibiti wa maambukizi ya ugonjwa wa malaria kupitia Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Malaria. Afua zinazosimamiwa na mpango huu ni pamoja na;
·       Matibabu sahihi ya malaria ikiwa ni pamoja na kupima malaria
·       Kununua na kusambaza vipimo vya haraka vya kupima malaria (Rapid Diagnostic Tests) na dawa za kutibu malaria
·       Mkakati wa kusambaza vyandarua vilivyotiwa viuatilifu ikiwa ni pamoja na kusambaza vyandarua kwa mama wajawazito na watoto wa umri chini ya miaka mitano kwa kutumia hati punguzo
·       Kuangamiza viluwiluwi vya mbu
·       Kuangamiza mbu kwa kupuliza dawa ya ukoko
·       Kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na  utoaji taarifa

Ndugu wananchi,
Ugonjwa wa Homa ya Dengue ni ugonjwa uliojitokeza kwa mara ya kwanza nchini mwaka 2010. Hadi sasa, nchi imeshuhudia kuwepo kwa milipuko mitatu (3) ya ugonjwa huu, yaani mwaka 2010, 2012 na mwaka 2013. Idadi kubwa ya wagonjwa imekuwepo kwa mwaka 2012,  ambapo jumla ya watu 172 walipata ugonjwa huo. Katika mlipuko ulioanza  Januari 2014 hadi sasa, jumla ya watu 144 wamepata ugonjwa wa dengue na kumekuwa na kifo cha mtu mmoja.

Ndugu wananchi,
Homa ya dengue husababishwa na kirusi kinachoenezwa na mbu aina ya Aedes ambaye ni mbu mweusi mwenye madoa meupe. Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na homa ya ghafla, kuumwa kichwa hususani sehemu za macho, maumivu ya viungo na uchovu, kuvimba tezi na kupatwa na harara. Vilevile mara chache mgonjwa anaweza kutokwa na damu sehemu za fizi, mdomoni, puani, kwenye macho na pia njia ya haja kubwa na ndogo. Dalili za ugonjwa huu zinaweza kufanana sana na dalili za ugonjwa wa malaria, hivyo basi wananchi wanaaswa kuwa wakipata dalili za homa, wawahi vituo vya kutoa huduma za afya ili wafanyiwe vipimo na kugundua kama wana vimelea vya malaria au dengue na hatua stahiki kuchukuliwa.

Ndugu Wananchi,
Magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele ambayo yanaenezwa  na wadudu ni pamoja na ngirimaji yaani mabusha, matende, usubi, malale, vikope, tauni, homa ya papasi na kichocho. Takwimu zinaonesha uwepo wa magonjwa haya katika jamii yetu hivyo, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na wadau inaendelea kutekeleza afua mbalimbali za kupambana na magonjwa haya kwa kutoa dawa katika jamii kupitia Program ya Taifa wa Kudhibiti magonjwa yaliyokuwa hayapewi kipaumbele. Manufaa ya dawa hizi kama zitatumika kwa usahihi ni pamoja na;
·       Kupunguza maambukizi kutoka mtu mmoja kwenda kwa mwingine
·       Kuua vimelea vya magonjwa
·       Kumuepusha mtu kupata upofu
·       Kuondoa athari zinazosababishwa na magonwa haya

Ndugu wananchi,
Homa ya manjano ni mojawapo ya magonjwa hatari yanayoambukizwa na wadudu. Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani, kila mwaka watu wapatao 200,000 huambukizwa homa ya manjano ambapo kati yao watu 30,000 hufariki duniani. Watanzania wapo hatarini kupata maambukizi ya ugonjwa huu kutokana na kuwa na mwingiliano na nchi nyingine na kwa kuwa mbu wanaombukiza homa ya manjano wapo Tanzania.

Dalili za ugonjwa huu ni pamoja na mwili kubadilika rangi na kuwa wa njano maeneo ya macho, viganja, ngozi na kucha, kupata homa, kuumwa na kichwa na misuli  na mgonjwa kutokwa na damu mdomoni, puani na masikioni. Ugonjwa huu hauna tiba, hivyo njia pekee ya kujikinga ni kupata chanjo ya homa ya manjano. Ili kuzuia ugonjwa huu kuingia nchini, Serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii imeweka utaratibu wa kufanya ufuatiliaji wa wasafiri wanaoingia nchini kutoka nchi zilizo na ugonjwa huu kupitia vyombo vya usafiri kwenye bandari, viwanja vya ndege na mipakani ili kuhakikisha wamepata chanjo inavyostahili. Wizara pia inaratibu upatikanaji wa huduma za chanjo kwa wananchi wa Tanzania wanaosafiri kwenda nchi za nje zenye maambukizo. 

Ndugu wananchi,
Magonjwa yanayoenezwa na wadudu yanazuilika endapo kanuni za afya zitafuatwa. Wananchi wanashauriwa kujikinga na magojwa hayo kwa kuzingatia yafuatayo;

·       Angamiza mazalia ya wadudu kwa kufukia madimbwi, kufyeka nyasi na kuondoa makopo, vifuu vya nazi, chupa za maji na magurudumu ya magari ambayo hayatumiki
·       Tumia dawa za kuua wadudu wanaoeneza magonjwa
·       Weka nyavu kwenye madirisha za kuzuia wadudu wanaoeneza magonjwa kuingia ndani ya nyumba
·       Hakikisha unalala kwenye chandarua kila siku kwani sehemu kubwa ya magonjwa haya yanaenezwa kwa kung’atwa na mbu

Ndugu Wananchi,
Jitihada nyingine zinazotekelezwa na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii katika Kuzuia na kudhibiti magonjwa yanayoenezwa na wadudu ni pamoja na;

·       Kuendelea kufanya ufuatiliaji wa magonjwa yaliyotajwa ili kudhibiti kuenea kwa magonjwa haya.
·       Kuongeza kasi ya utoaji elimu ya afya kwa jamii kuhusu kujikinga na magonjwa hayo.
·       Kuhakikisha huduma za uchunguzi na matibabu zinapatikana kwenye vituo vya kutolea huduma wakati wote.
·       Kuendelea na tafiti zitakazoongeza uelewa wetu wa magonjwa hayo na kubuni mbinu mpya za kupambana nayo

Ndugu wananchi
Napenda kuhitimisha kwa kusisitiza kwamba mapambano dhidi ya magonjwa yanayoenezwa na wadudu ni  jukumu la kila mmoja wetu hivyo basi, ni muhimu kuzingatia njia za kujikinga na magonjwa haya. Endapo utaona dalili mojawapo kati ya hizo zilizotajwa, nenda katika kituo cha kutolea huduma za afya mapema kwa uchunguzi na matibabu.

‘Kumbuka, Mng’ato Mmoja Madhara Makubwa’,  Chukua Tahadhari 
                      
ASANTENI  KWA KUNISIKILIZA

No comments:

Post a Comment