Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam Kamishna (CP) Suleiman Kova akitoa ufafanuzi ameeleza kwa waandishi wa habari kuhusu wakazi wa jiji la Dar es Salaam hususan madereva wa bodaboda na Bajaji kufuata sheria za barabarani na kajenga tabia ya kufanya tathmini ya safari zao iwapo wanakidhi vigezo vya usalama barabarani ili kuepusha madhara.
Ofisa Mfawidhi wa SUMATRA Kanda ya Mashariki Bw. Conrad Shio akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu sheria inayosimamia usafiri wa Bajaji na Bodaboda nchini. (Picha zote na Aron Msigwa – MAELEZO)
Na Aron Msigwa –MAELEZO, Dar es Salaam.
MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam Saidi Mecki Sadiki amewaagiza viongozi na watendaji wa jiji la Dar es
salaam kuhakikisha kuwa wanawaondoa na kuwachukulia hatua za kisheria ikiwa ni
pamoja na kuwafikisha mahakamani wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanaovunja sheria za jiji kwa kuendesha
shughuli mbalimbali katika maeneo
yasiyoruhusiwa.
Aidha amewataka waendesha
pikipiki maarufu kwa jina la “Bodaboda”,
Bajaji, waendesha baiskeli na mikokoteni wanaofanya biashara ya kubeba abiria
na mizigo maeneo yasiyoruhusiwa kisheria kuondoka wenyewe kabla hatua kali za
kisheria hazijachuliwa dhidi yao.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam
Saidi Mecki Sadiki amesema kuwa jiji la
Dar es Salaam limeamua kuchuakua uamuzi huo kufuatia tatizo la baadhi ya
wananchi kuamua kuvunja sheria zilizowekwa kwa kisingizio cha ugumu wa maisha
na kutafuta fedha hali inayoleta usumbufu kwa wananchi wengine.
Amesema kuwa licha ya
changamoto inayolikabili jiji la Dar es Salaam hasa maeneo ya katikati ya mji
hali iliyopo sasa ya biashara holela na uvunjifu wa sheria unaofanywa na
maendesha Bodaboda, Bajaji, baiskeli, mikokoteni na Taxi bubu maeneo
yasiyoruhusiwa kisheria hauwezi kuvumilika.
“Jiji la Dar es Salaam
tumekuwa na kero ya muda mrefu hasa ya omba omba, waendesha baiskeli, bodaboda
na wafanyabiashara katika maeneo ya makutano ya barabara katika maeneo
yasiyoruhusiwa hali hii hatuwezi kuivulimia, sisi hatufukuzi watu bali
tunawataka wafuate sheria za jiji” Amesisitiza.
Ameeleza kuwa serikali
haina lengo la kuwazuia wananchi kufanya biashara na shughuli nyingine za
kujiingizia vipato kama wanazingatia sheria na taratibu zilizowekwa na kuongeza
kuwa wale wote wanaoomba leseni za kufanyia biashara wanapewa taratibu na
miongozo na masharti ya kuzingatia wanapofanya biashara zao jambo ambalo wengi
wao wanashindwa kulizingatia.
“Kila Manispaa ina
miongozo na kanuni za uendeshaji wa shughuli zake ikiwa ni pamoja na mamlaka ya
kutenga maeneo ya biashara na kuwaruhusu wale wanakidhi masharti ya leseni zao
kufanya biashara zao ila wengi wao hasa madereva wa Bajaji na Bodaboda
hawazingatii haya” Amesisitiza Mh. Sadiki.
Ameeleza kuwa sheria
zote zilizotungwa zimewekwa ili zifuatwe kwa ustawi wa taifa na si vinginevyo
na kubainisha kuwa wote waliovamia maeneo ya vituo vya mabasi, maeneo ya vituo
vya umeme na hifadhi za barabara ni vema wakaondoka wenyewe na kukubali kutii
sheria bila shuruti huku akitoa mfano wa baadhi ya wafanyabiashara na wauza
vyakula “mama lishe” walio anza kuvamia maeneo ya ujenzi wa mradi wa mabasi
yaendayo Kasi (DART).
“Haiwezekani sheria za
jiji zikavunjwa na sisi tukaendelea kuwaangalia baadhi yao wamefikia hatua ya
kuvamia maeneo ya mradi wa mabasi yaendayo kasi na kuanza kufanya biashara na
kuwasumbua mafundi jambo lisilokubalika”.
Akizungumza kuhusu
biashara ya bodaboda inayofanywa na vijana walio wengi jijini Dar es Salaam Mh.
Sadiki ameeleza kuwa mpango wa serikali kuruhusu Bodaboda na Bajaji kutumika
kubebea abiria ulikuwa na maana nzuri ya kuwawezesha wananchi kupata usafiri
hasa katika maeneo yasiyofikika kirahisi kwa magari hasa vijijini na kuongeza
kuwa utakua na mafanikio kama watafuata sheria.
‘Serikali iliruhusu
usafiri wa Pikipiki na Bajaji kutumika kubebea abiria kwa nia nzuri ikiwa ni
pamoja na kurahisisha usafiri na kuongeza ajira,hivyo siyo nia yetu kuwadhalilisha
vijana hawa tunachowataka wafanye ni kufuata sheria za nchi”.
Aidha kwa upande wa
ongezeko la ombaomba ambao baadhi yao walirudishwa katika maeneo yao ya awali
na kurejea tena jijini Dar es Salaam ameeleza kuwa utaratibu wa kuwafuatilia
uko pale pale na kufafanua kuwa watakaokutwa na makosa ya kukaa maeneo
yasiyoruhusiwa watafikishwa mahakamani.
Kwa upande wake
Kamishna wa Jeshi la Polisi wa kanda maalum ya Dar es Salaam, Suleman Kova
ameeleza kuwa ni wakati sasa wa wakazi wa jiji la Dar es salaam hususan
madereva wa bodaboda na Bajaji kufuata sheria na kusisitiza kuwa ni vema
wananchi wakajenga mazoea ya kufanya tathmini ya safari zao iwapo wanakidhi
vigezo vya kuwawezesha kutembea barabarani.
“Kwa waendesha pikipiki
“bodaboda” hali ni mbaya wengi wameumia na kupata ulemavu wa kudumu kwa
kutozingatia sheria za usalama
barabarani na kukidhi matakwa ya kuendesha pikipiki hizo”.
Amesema kuwa Jeshi la
Polisi litafanya kazi yake kwa kushirikiana na manispaa zote tatu kuhakikisha
kuwa vitendo vya uvunjifu wa sheria vinakomeshwa na kutoa wito kwa wananchi
kutoa taarifa pindi wanapoona dalili zozote za uvunjifu wa amani hasa matukio
ya ujambazi kwa kutumia pikipiki yayoendelea kuongezeka kwa kasi.
“Napenda niwahakikishie
wananchi kuwa jeshi la polisi tumejipanga vizuri kukabiliana na vitendo vyote
vya uhalifu wa aina zote, pia natoa wito kwa wakazi wa jiji la Dar es salaam
hasa wafanyabiashara kuepuka kutembea na fedha nyingi ili kuepuka madhara ya
kuvamiwa”.
Naye Afisa Mfawidhi wa
SUMATRA Kanda ya Mashariki ameeleza kuwa sheria ya usafirishaji kusimamia
Bajaji na Bodaboda iko wazi na kuongeza kuwa serikali ina wajibu wake na pia
waendesha pikipiki na Bajaji wanawajibu wao wa kuzingatia kanuni taratibu na
kanuni zilizowekwa.
“Sisi kama SUMATRA
tunaendelea kufanya kila tuwezalo kukabiliana na vitendo vyote vya uvunjivu wa
sheria za barabarani”.
No comments:
Post a Comment