Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini, Joyce Fisoo
akiwaeleza jambo Mkurugenzi wa Kikundi cha Harakati Fatia Musa (katikati) na
Mjumbe wa kikundi hicho na Mwigizaji wa filamu hiyo Ramadhani Nassoro kuhusu
filamu yao inayoitwa Dark Forest, kwenye ofisi ya Bodi hiyo jijini Dar es
Salaam leo.
Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini, Joyce Fisoo, akionesha moja ya sehemu ya
filamu ya Dark Forest ya Kikundi cha Harakati wakati akiakipitia na kukagua
filamu hiyo ili kuboresha kazi za Wasanii nchini.Kazi hiyo ilifanyika kwenye
ofisi ya Bodi hiyo jijini Dar es Salaam leo.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini, Joyce Fisoo (kulia)
akieleza jambo wakati akipitia na
kukagua filamu ya Dark Forest ya Kikundi cha Harakati kwenye ofisi za Bodi hiyo
jijini Dar es Salaam leo.Kutoka kushoto ni Mkaguzi Mkuu wa Filamu Tabu Magembe,
Mkaguzi wa Filamu Beatrice Sumari, Mjumbe wa kikundi Ramadhani Nassoro na
Mkurugenzi wa Kikundi Fatia Musa.
Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini, Joyce
Fisoo,akifafanua jambo wakati akizungumza na baadhi ya wawakilishi wa Kikundi
cha Harakati kutoka jijini Dar es Salaam kuhusu filamu yao ya Dark Forest
wakati wa kupitia na kukagua kazi wa wasanii wa tasnia ya filamu nchini leo.
Katikati ni Mkurugenzi wa kikundi hicho Fatia Musa na Mwigizaji wa filamu hiyo
Ramadhani Nassoro.
Muongozaji
wa Filamu ya Dark Forest, Ramadhani Kisoka akitia saini makubaliano ya
kutekeleza maazimio waliokubaliana na Bodi kuhusu kurekebisha filamu hiyo.
Mwigizaji wa
filamu hiyo, Ramadhani Nassoro, akitia saini makubaliano ya kutekeleza maazimio
waliokubaliana na Bodi kuhusu kurekebisha filamu hiyo huku akishuhudiwa na Katibu
Mtendaji wa Bodi ya Filamu nchini.
Mkurugenzi
wa Kikundi cha Harakati, Fatia Musa, akitia saini makubaliano ya kutekeleza
maazimio waliokubaliana na Bodi kuhusu kurekebisha filamu hiyo huku
akishuhudiwa na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini Joyce Fisoo.
Na Hussein Makame-MAELEZO
BODI ya
Filamu imewaonya wazalishaji wa filamu nchini kuwa watakaotengeneza filamu
chini ya kiwango kwa makusudi watafungiwa ikiwa ni moja ya njia ya kuboresha
tasnia ya filamu nchini na kukuza vipaji vya wasanii wachanga.
Onyo hilo limetolewa
na Katibu Mtendaji wa Bodi ya Filamu Nchini, Joyce Fissoo baada ya kupitia na
kuikagua filamu ya Dark Forest ya Kikundi cha Harakati ambayo imeonekana
imetengenezwa chini ya viwango vinavyotakiwa.
Alisema utengenezaji
wa filamu hiyo haikutumia vifaa vya kitaalamu, ina mwanga mbaya, haikutumia
vifaa vya sauti vya kitaalamu na kufanya kuingiliana kwa sauti nyingine
zisizohitajika na kasoro nyingine nyingi.
Fissoo
alisema Bodi hiyo pia ilibaini kuwa
uchukuaji wa picha wa filamu hiyo ulitumia siku tatu jambo ambalo ni
kuidhalilisha tasnia ya filamu na kutowatendea haki Watanzania ambao ndio
watumiaji wa kazi hiyo.
“Baada ya
kupitiwa ilibainika filamu hiyo kuwa katika kiwango cha chini sana na kwamba
Kampuni ya Lee One Production ilishiriki kuchukua picha zake ni kampuni yenye
uzoefu na kazi zake zilikwishawahi kuja Bodi zikiwa katika kiwango cha
kuridhisha” alisema Fissoo.
Akizungumza
kwa njia ya simu na MAELEZO, Mkurugenzi wa Lee One Production Emmanuel Mapunda alisema
awali filamu hiyo ilirekodiwa vizuri lakini kanda ya picha za filamu hiyo
haikutunzwa kwenye vifaa bora kama alivyoshauri.
Alisema
baada ya kugundua kuwa picha za filamu hiyo zimeharibika, aliwashauri wahusika
wa filamu hiyo kutoitoa kutokana na kutokuwa na viwango vinavyohitajika na kwamba
wanatakiwa wakairekodi upya, hata hiyo hawakukubaliana.
Kutokana na
filamu hiyo kutengenezwa chini ya kiwango, Fissoo aliitisha kikao kukutana na
kikundi cha Harakati kilichotoa filamu hiyo na wahusika wote kujadiliana nao
kwa kina, walifikia maazimio kuwa tabia ya kuharibu kwa makusudi kazi za wasanii
wanaoibukia iachwe mara moja.
“Wanaotengeneza
filamu chini ya kiwango kwa makusudi watafungiwa, onyo kali kwa Mkurugenzi wa
kampuni ya Lee One Production na Mwongozaji wa filamu husika Bwana Ramadhani Kishoka
kwa kutotekeleza majukumu yao kwa kuzingatia weledi na taalum” alisema Fissoo
na kuongeza :
”Marekebisho
hayo yafanyike kwa kuzingatia viwango vya ubora kwani kuipeleka sokoni filamu
hiyo ni kutowatendea haki Watanzania na kuiua tasnia ya filamu jambo ambalo
Serikali haitaliruhusu”.
Waandaaji wa
filamu hiyo walikiri kuwa kiwango cha filamu hiyo ni cha chini na muongozaji
wake Ramadhani Kisoka ameahidi kuwa ataandika barua ya kuomba radhi na kurudia
kazi hiyo na kuiwasilisha Bodi.
Bodi ya
Filamu imekuwa ikitekeleza majukumu yake ikiwemo kupitia na kukagua filamu
zinazotengenezwa nchini na kuzipitisha kwenda sokoni ambapo filamu hiyo ya Dark
Forest ilikamatwa na Bodi wakati wa operesheni zake za kawaida.
No comments:
Post a Comment