TANGAZO


Tuesday, November 26, 2013

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Makame Mbarawa afungua mkutano wa Baraza la Wafanyakazi wa Posta

Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania, wakati alipokuwa akiufungua mkutano wa baraza la shirika hilo, Dar es Salaam leo. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Waziri wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania, wakati alipokuwa akiufungua mkutano wa baraza lao, Dar es Salaam leo. Kulia ni Postamasta Mkuu, Deos Mndeme na katikati ni Mkurugenzi Msaidizi wa Mawasiliano wa wizara hiyo, Samson Mwela.


*Awataka wafanyakazi kuwa wabunifu
Na Grace Gurisha
WAZIRI wa Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Profesa Makame Mbarawa, amewataka wafanyakazi wa Shirika la Posta Tanzania wawe wabunifu ili wapate vyanzo vipya vya mapato.

Akizungumza leo, jijini Dar es Salaam wakati akifungua Mkutano wa 22 wa Baraza Kuu la Wafanyakazi wa shirika hilo, Profesa Mbarawa alisema wakipata vyanzo vipya wataboresha  maslahi ya watumishi na kutoa gawio kwa Serikali.

"Kama mnavyo jua hivi sasa hakuna mambo ya kuandikiana barua kama zamani, kwa hiyo mnatakiwa muwe wabunifu ili muweze kupata ushindani wa kibiashara kuendana na mazingira yaliyopo sasa ya Sayansi na Teknolojia", alisema Profesa Mbarawa.

Profesa Mbarawa alisema anaamini kuwa bado kuna fursa  ya kufanya vizuri zaidi endapo watapambanua na kutangaza huduma zao kwa wadau katika wizara tofauti, taasisi na ofisi za Serikali pamoja na kampuni na asasi binafsi ambazo zingependa kutumia shirika hilo, kufikisha huduma na bidhaa zao kwa wananchi wa kawaida ambao wako nje ya miji mikuu ya mikoa.

Hata hivyo, alisema  utaratibu wa kuboresha mtaji utabainishwa baada ya kukamilika mchakato wa la kurekebisha mizania ya shirika, wizara yake itaendelea kushirikiana na Wizara ya Fedha ili kuhakikisha madeni yaliyosalia ya pensheni yanalipwa.

Pia alisema katika mkutano huo wafanyakazi hao watapata fursa ya kujadili mada tatu ikiwemo kujua huduma zinazotolewa na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), kwa hiyo watumia fursa hiyo kwa kupima afya zao.

"Tumieni fursa hii vizuri kwa sababu watakuja wataalamu hapa muweze kupima afya zenu, tunatakiwa kwenda na wakati, kwa sababu ukishajua afya yako utaishi vizuri", alisema.

Alisema bado kuna furza za kufanya kazi zaidi za kusambaza huduma, ambapo aliwataka wafanyakazi hao kuwatafuta wateja sio wasubiri wateja wenyewe waende ofisini kutokana na wateja wengine kuwa waoga.

"Kila mtanzania anaimani na shirika lenu, nendeni mkafanye kazi msikae tu ofisini, kila mtu anatakiwa apate kwa kile wanachokifanya", alisema.

Pia aliwashauri kuwa kuwepo na huduma kupitia simu ya mkononi, baada ya mteja kutumia mzigo wake atakuwa anatumiwa ujumbe mfupi wa maneno  katika  simu yake mpaka pare mzigo utakapo pokelewa.

Alisema wafanyakazi hao wanapaswa kujadili mafanikio waliyopata na changamoto walizokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu na mipango ya shirika hilo pamoja na kujiwekea malengo na mpango kazi utakaowezesha kuendeleza ustawi wa shirika hilo.

Naye Mwenyekiti  wa Baraza Kuu na Postamasta Mkuu wa shirika hilo, Deos Mndeme alisema mkutano huo unawawakilishi kutoka Tanzania Bara na Visiwani.

Alisema wajumbe hao watapata fursa ya kujadili mada juu ya mafao ya Mfuko wa Pensheni wa PPF, huduma zinazotolewa na
Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF), fursa za mikopo ya nyumba za makazi kutoka  Benki ya CRDB na pia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).


Hata hivyo, Mwenyekiti wa Bodi ya shirika hilo, Yamungu Kayandabila alisema wafanyakazi hao wanafanya kazi kwa bidii na hakuna malumbano yoyote, wanafanya kazi kwa kuelewana.

No comments:

Post a Comment