TANGAZO


Wednesday, November 27, 2013

ICC yataka Kenyatta kuwepo mahakamani

 


Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya
 

Mahakama ya Kimataifa ya kushughulikia kesi za uhalifu wa kivita, ICC imetengua uamuzi wake wa awali uliomruhusu Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta kutohudhuria baadhi ya vikao vya kesi ya uhalifu wa kivita inayomkabili.
 
Mahakama hiyo sasa imesema kuwa ni lazima Bwana Kenyatta afike binafsi mbele ya mahakama hiyo kusikiliza kesi yake na ushahidi unaotolewa dhidi yake.

 
Mahakama hiyo imesema kama sheria inavyotaka, Bwana Kenyatta lazima binafsi ahudhurie vikao vya kesi inayomkabili. Imesema maombi yoyote ya baadaye ya kutaka asihudhurie baadhi ya vikao vya kesi hiyo, yatafikiriwa kutokana na msingi wa suala linaloombewa ruhusa hiyo.

Mahakama hiyo imefikia uamuzi kwamba hukumu iliyotolewa katika rufaa ya tarehe 25 Oktoba 2013 ya Mwendesha mashitaka dhidi ya William Samoei Ruto na Joshua Arap Sang, imetoa taarifa mpya muhimu ambayo inahalalisha kuangaliwa upya kwa suala la kesi hiyo.

Mahakama ya Rufaa ya ICC imehitimisha kuwa Mahakama ina hiyari kwa mujibu wa kifungu namba 63(1), kinachosema kuwa "mtuhumiwa ni lazima awepo mahakamani wakati kesi inayomkabili ikiendeshwa", lakini hiyari hiyo imewekewa kikomo. Mahakama ya Rufaa imetoa uamuzi kwamba mtuhumiwa kutofika mahakamani, inaruhusiwa pale tu panapokuwa na sababu maalum na za kipekee, na lazima sababu hizo ziwe zinakidhi hoja kwa mtuhumiwa kutofika mahakamani hapo.Imeendelea kusema kwamba uamuzi wa kama mtuhumiwa aruhusiwe kutohudhuria sehemu ya vikao vya kesi yake lazima uzingatie hali halisi ya ombi la mtuhumiwa.



Fatou Bensouda,Mwendesha Mashtaka Mkuu ICC
 
Awali mahakama hiyo ya ICC katika uamuzi wake wa tarehe18 October 2013, ilitoa masharti kwa upande wa utetezi wa Bwana Uhuru Muigai Kenyatta kuwepo mahakamani hapo wakati wa ufunguzi na kufunga kesi inayomkabili badala ya kuwepo wakati wote. Wakati huo angeweza kusikiliza maelezo kutoka pande zote na kusikiliza maoni ya waathirika wa ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa 2007 nchini Kenya. Pia angetakiwa kuwepo siku ya kufunga kesi hiyo kwa kusikiliza hukumu yake.
Kutokana na uamuzi huo wa kumruhusu Bwana Kenyatta kuhudhuria vikao vya ufunguzi na kufunga kesi yake pamoja na vikao vingine ambavyo angeitwa pale mahakama inapoona umuhimu wa yeye kuwepo mahakamani, mwendesha mashitaka alipinga uamuzi huo tarehe 28 Oktoba 2013, kwa kukata rufaa, akitaka kuangaliwa upya kwa uamuzi wa tarehe 18 Oktoba 2013, ambapo mwendesha mashitaka aliomba mahakama kufuta uamuzi wake wa kumruhusu mtuhumiwa kutohudhuria baadhi ya vikao vya kesi yake na badala yake mahakama izingatie sheria kuu chini ya kifungu cha 63(1).

Bwana Kenyatta ameshitakiwa kama mchochezi asiye rasmi, akikabiliwa na mashitaka matano ya uhalifu dhidi ya binadamu, yakiwemo mauaji, kuhamishwa watu kwa nguvu, ubakaji, utesaji na vitendo vingine visivyo vya kibinadamu, vinavyodaiwa kufanyika wakati wa ghasia za baada ya uchaguzi nchini Kenya mwaka 2007-2008.

Mashitaka dhidi yake yalithibitishwa tarehe 23 Januari 2012, na kesi hiyo kukabidhiwa Chemba namba V(b) ya mahakama hiyo ya ICC. Kesi yake imepangwa kuanza kusikilizwa katika mahakama hiyo tarehe 5 Februari 2014.

No comments:

Post a Comment