TANGAZO


Monday, October 21, 2013

Ofisi ya Taifa ya Takwimu yatoa hali halisi ya ukuaji wa Pato la Taifa kwa bei za Soko

Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi toka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Morrice Oyuke, akielezea kwa waandishi wa habari (hawapo pichani), leo jijini Dar es Salaam, hali halisi ya ukuaji wa Pato la Taifa kwa bei za soko, uliongezeka kwa kasi ya asilimia 6.7 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013, ikilinganishwa na kasi ya asilimia 6.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2012.
Waandishi wa habari wakimfuatilia kwa makini habari zilizokuwa zikitolewa na Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, toka Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Morrice Oyuke (hayupo pichani), wakati alipokuwa akielezea kuhusu ukuaji wa Pato la Taifa katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013, uliongezeka kwa asilimia 6.7 ikilinganishwa na asilimia 6.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2012.
Mkurugenzi wa Takwimu za Uchumi, toka Ofisi ya Taifa ya Takwimu Morrice Oyuke, akielezea kwa waandisi wa habari (hawapo pichani) leo, jijini Dar es Salaam kuhusu ukuaji wa shughuli za uchumi za kilimo zilivyokua kwa kasi ya asilimia 5.3 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013, ikilinganishwa na asilimia 5.1 katika kipindi kama hicho, mwaka 2012. (Picha zote na Eliphace Marwa - MAELEZO)


OFISI ya Taifa ya Takwimu, Wizara ya Fedha ina jukumu la kukokotoa Pato la Taifa kwa robo Mwaka ili kuwapatia takwimu  kwa wakati, wadau wa takwimu za Pato la Taifa katika vipindi vifupi vya robo mwaka ili kuweza kutathmini mabadiliko ya ukuaji wa uchumi.


Ukuaji halisi wa Pato la Taifa la Tanzania kwa bei za soko uliongezeka kwa kasi ya asilimia 6.7 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 6.4 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Jumla ya thamani ya Pato la Taifa katika kipindi husika ilikuwa Shilingi 5,012,935 milioni mwaka 2013 ikilinganishwa na Shilingi 4,699,884 milioni mwaka 2012.

Kasi ya Ukuaji wa Pato la Taifa kwa Robo Mwaka, Robo ya Pili, Aprili – Juni, 2003 – 2013


Ukuaji wa Shughuli za Uchumi za Kilimo na Uvuvi
Shughuli za kiuchumi za kilimo zilifikia kasi ya ukuaji ya asilimia 5.3 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 zikilinganishwa na asilimia 5.1 ya robo kama hiyo mwaka 2012. Katika kipindi hicho, kulikuwa na mvua za kutosha katika mikoa inayozalisha mazao kwa wingi. Aidha, maelekezo ya ma-ofisa Ugani kwa wakulima kama kuchagua aina bora ya mbegu yalisaidia kuongeza uzalishaji.


Shughuli za uvuvi zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 2.4 katika robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na asilimia 6.5 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Kasi ya ukuaji huu ilipugua kutokana na kupungua kwa mavuno ya samaki kutoka kwenye maziwa, mito na mabwawa.

Shughuli za Uchumi za Viwanda na Ujenzi
Shughuli za uchimbaji madini, mawe na kokoto ziliongezeka kwa kasi ya asilimia 4.3 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na kuporomoka kwa kasi ya ukuaji wa asilimia 5.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Kuongezeka kwa kasi hii ya ukuaji ilitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa madini ya almasi na Tanzanite katika robo ya pili ya mwaka 2013.


Shughuli za uzalishaji bidhaa viwandani zilifikia kasi ya ukuaji ya asilimia 5.8 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 8.2 mwaka 2012. Kupungua kwa kasi ya ukuaji ya asilimia 2.4 (percentage point) kulitokana na kupungua kwa uzalishaji wa sementi, vyakula vilivyosindikwa na nguo.

Uzalishaji wa nishati ya umeme ulifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 4.5 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na kuporomoka kwa kasi ya ukuaji ya asilimia 1.1 katika kipindi kama hicho mwaka 2012. Kuongezeka kwa ukuaji wa nishati ya umeme kwa asilimia 5.6 (percentage point) kulitokana na kuongezeka kwa uzalishaji wa nishati ya umeme unaotokana  na mafuta na gesi.


Ukuaji wa Shughuli za Uchumi za Utoaji Huduma
Shughuli za biashara za jumla na reja reja, ukarabati wa magari na pikipiki na vifaa vingine vya majumbani zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 5.9 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2013 ikilinganishwa na kasi ya asilimia 7.0 katika kipindi cha robo ya pili ya mwaka 2012. Kupungua kwa kasi kwa asilimia 1.1 (percentage point) kulitokana na kupungua kwa bidhaa zilizotengenezwa hapa nchini na zilizoagizwa kutoka nje ya nchi zilizouzwa katika kipindi hicho.  Shughuli za upangishaji nyumba, na shughuli zingine za biashara zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 6.7.


Shughuli za uchukuzi na mawasiliano zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 14.8 katika kipindi husika. Shughuli nyingine ni huduma za Hoteli na migahawa zilizofikia kasi ya ukuaji wa asilimia 3.2; Shughuli za uendeshaji Serikali zilifikia kasi ya asilimia 5.0, Elimu asilimia 5.7 na huduma za Afya na shughuli nyinginezo zilifikia kasi ya ukuaji wa asilimia 3.8 katika kipindi hicho.

Imetolewa na: Morrice  Oyuke
Mkurugenzi wa Takwimu za Kiuchumi
Ofisi ya Taifa ya Takwimu
Dar es Salaam

No comments:

Post a Comment