TANGAZO


Friday, October 25, 2013

Bonanza la mpira wa miguu la Vituo vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu lafanyika jijini Dar es Salaam


*Serikali yatoa wito kwa wadau wa michezo kuendelea kuwekeza katika sekta hiyo
 
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel akisalimiana na Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diana Melrose (kulia) leo, katika Viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari ya Kibasila, wakati wa Bonanza la mchezo wa mpira wa miguu, lililohusisha vijana kutoka katika vituo 19 vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu vya jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diana Melrose, akipiga mpira kuashiria kuanza kwa Bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililohusisha vijana kutoka katika vituo 19 vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu vya jijini Dar es salaam. Kulia anayeonekana kudaka mpira huo ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diana Melrose (kulia) akikagua timu ya mpira ya FC Kigamboni kutoka Kituo cha kulelea watoto walio katika mazingira magumu cha Kigamboni kabla ya kuanza kwa michuano ya kuwania kombe katika bonanza lililovihusisha vituo 19 vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu vya jijini Dar es Salaam.
Mashindano hayo yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa Ubalozi wa Uingereza, British Council, Baraza la Michezo Tanzania na Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo yakiendelea katika Viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Kibasila leo, jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi wa British Council nchini Tanzania, Richard Sunderland akikagua timu ya mpira ya kituo cha kulelea watoto walio katika mazingira magumu cha Dogodogo leo, katika Viwanja vya michezo vya Shule ya Sekondari Kibasila.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo (kulia), akimvisha medali kijana Juma Abdul wa kituo cha kulelea watoto walio katika mazingira magumu cha Kigamboni leo, jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diana Melrose (kushoto), akizungumza jambo na Arafa Abdul kutoka kituo cha mpira wa miguu cha Twalipo (Twalipo Camp Soccer Foundation) leo, jijini Dar es salaam. Arafa Abdul alikua mmoja wa waamuzi wa Bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililohusisha vijana kutoka katika vituo 19 vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu vya jijini Dar es Salaam.
Washindi wa jumla wa Bonanza hilo, timu kutoka kituo cha kulelea watoto walio katika mazingira magumu cha Dogodogo wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi kutoka Wizara ya Habari, Ubalozi wa Uingereza, Baraza la Michezo Tanzania, Right to Play Tanzania mara baada ya kunyakua Kombe na medali mbalimbali.
Washindi wa jumla wa Bonanza hilo, timu ya mpira wa miguu kutoka kituo cha kulelea watoto walio katika mazingira magumu cha Dogodogo Centre, wakifurahia ushindi mara baada ya kutangazwa leo, jijini Dar es Salaam.
Balozi wa Uingereza nchini Tanzania, Diana Melrose (kulia), akizungumza jambo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo mara baada ya kumalizika kwa Bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililohusisha vijana kutoka katika vituo 19 vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu vya jijini Dar es salaam. Kushoto ni Mkurugenzi wa British Council nchini Tanzania, Richard Sunderland. (Picha zote na Aron Msigwa - MAELEZO)

 
Na Aron Msigwa -MAELEZO.
Dar es salaam.
SERIKALI imetoa wito kwa wadau mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi kuendelea kuwekeza katika sekta ya  michezo , kuibua na kuendeleza vipaji vya vijana walio katika maeneo mbalimbali nchini.

 Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Prof. Elisante Ole Gabrile  ametoa wito huo leo jijini Dar es salaam wakati  wa Bonanza la mchezo wa mpira wa miguu lililowahusisha vijana kutoka katika vituo 9 vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu  na shule zilizo jirani na vituo hivyo jijini Dar es salaam.

Prof. Elisante ameeleza kuwa Tanzania kwa sasa ina fursa nyingi za uwekezaji katika sekta ya michezo na kuongeza kuwa serikali kwa kuliona hilo inaendelea kuwezesha na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha kuwa sekta hiyo inapiga hatua kutokana na mchango wake katika katika kudumisha amani na upendo, kukuza ajira ,uzalendo na ushirikiano.

“ Sekta ya michezo nchini sasa inapiga hatua kwa kuwahamasisha vijana wengi kushiriki katika mashindano mbalimbali na kutumia fursa zilizopo kujiajiri na serikali tutaendelea kutoa msukumo kwa wadau mbalimbali kuingia katika juhudi hizi za kusaidia vikundi mbalimbali vya michezo vilivyopo nchini” amesema Prof. Elisante.

Kuhusu Bonanza la mchezo wa mpira wa miguu kwa vijana wanaoishi katika vituo vya kulelea watoto walio katika mazingira magumu lililofanyika leo jijini Dar es salaam amesema wengi wa vijana hao walikua wamekata tama kutokana na wengi wao kukosa wazazi kutokana na sababu moja au nyingine  na kuwataka vijana hao ambao wengi sasa wamefanikiwa kuendelea na masomo yao katika ngazi mbalimbali kuzitumia fursa walizopata ili kutowakatisha tama wafadhiri.

Amewataka vijana waliofanikiwa na kupiga hatua kimasomo kuwasaidia wenzao ambao bado wanahitaji msaada walio ndani ya vituo hivyo na wale ambao bado wako mitaani.
 
Kwa upande wake Balozi wa Uingereza nchini Tanzania Bi. Diana Melrose ameeleza kuwa kufanyika kwa bonanza hilo jijini Dar es salaam ni ishara kubwa ambayo imeonyesha kuwa vijana wengi walio katika mazingira magumu wakipewa fursa wanafanya mambo makubwa.

Amewapongeza vijana hao kwa kuonyesha mfano wa kushiriki katika bonanza la mashindano hayo ambapo washindi pamoja na mambo mengine wamekabidhiwa medali huku kombe  likienda kwa timu ya mpira wa miguu ya kituo cha dogodogo cha jijini Dar es salaam.

Naye mratibu wa mashindano hayo kutoka “British Council” Bi. Malula Nkanyemka ameeleza kuwa lengo la kuanzishwa kwa mashindano hayo mbali na kuibua vipaji na kuwajengea uwezo vijana hao kimichezo yanalenga kuwafanya vijana hao kujitambua na kuzitumia haki zao,  kucheza na kubadilisha tabia.

Mashindano hayo yaliyoratibiwa kwa ushirikiano na Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania, British Council, Rotary Club, Baraza la Michezo Tanzania (BMT), Right lo Play, Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo na wenyeji wa bonanza hilo  shule ya sekondari Kibasila yamefanyika katika viwanja vya michezo vya shule ya sekondari Kibasila na kuzishirikisha nyumba 9 za kulelea watoto walio katika mazingira magumu.

No comments:

Post a Comment