TANGAZO


Saturday, September 7, 2013

Dk. Shein azindua madarasa ya Chuo cha Sayansi ya Afya, asema: Tumepania kukabiliana na Changamoto katika Sekta ya Afya

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya, Dk. Haji Mwita, alipotembelea Daghalia ya Wanafuzi wa Chuo hicho, kabla ya kuzindua  madarasa ya chuo hicho leo, huko Mbweni nje ya Mji wa Unguja. (Picha zote na Ramadhan Othman, Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akipata maelezo kutoka kwa Mkuu wa Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya, Dk. Haji Mwita, alipotembelea na kuona vifaa mbalimbali vya kufundishia chuoni hapo, alipofika kuzindua madarasa ya kusomea yaliyojenga kwa ufadhili wa Serikali ya Oman kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akifungua pazia kama ishara ya uzinduzi wa jengo la madarasa ya Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya, lililogharamiwa  na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ushirikiano na Serikali ya Oman, huko Mbweni, nje ya Mji wa Unguja leo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein na Mshauri wa Mambo ya Afya, Wizara ya Afya ya Oman, Dk. Sayeed Sultan Bin Yarub Bin Qaatan Al- Busaid, wakikata utepe kama ishara ya uzinduzi wa jengo la madarasa ya Chuo cha Taaluma  za Sayansi ya Afya, lililogharamiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ushirikiano na Serikali ya Oman, huko Mbweni, nje ya Mji wa Unguja leo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akitoa ushauri wakati alipotembelea moja ya madarasa ya Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya, huko Mbweni baada ya kuyazindua rasmi leo, ambayo yamejengwa kwa ufadhili ya Serikali ya Oman kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Baadhi ya wanafunzi wa Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya, wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, wakati akitoa nasaha zake, baada ya kuyazindua rasmi madarasa ya chuo hicho leo, hapo Mbweni, Mkoa wa Mjini Mgharabi, nje ya Mji wa Unguja. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akipokea risala ya Chuo cha Taaluma za  Sayansi ya Afya, kutoka kwa Mkuu wa Chuo hicho, Dk. Haji Mwita, baada ya  kuyazindua rasmi madarasa ya kusomea, yaliyojengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Oman na ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. 
Mshauri wa Mambo ya Afya,Wizara ya Afya ya Oman, Dk. Sayeed Sultan Bin Yarub Bin Qaatan Al- Busaid, akitoa salamu zake wakati wa sherehe za uzinduzi wa madarasa mapya ya kusomea  katika Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya, yaliyojengwa na  Serikali ya Oman na ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, alipokuwa akitoa hutuba yake kwa Wananchi na wanafunzi (hawapo pichani), wakati wa Sherehe za uzinduzi wa jengo la madarasa ya Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya, lililogharamiwa na Serikali ya Oman kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, huko Mbweni, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja leo. Kushoto ni Waziri wa Afya wa Zanzibar, Juma Duni Haji na kulia ni Mshauri wa Mambo ya Afya, Wizara ya Afya ya Oman, Dk. Sayeed Sultan Bin Yarub Bin Qaatan Al-Busaid.
Baadhi ya wananchi na viongozi walioalikwa katika sherehe za  uzinduzi wa jengo la madarasa ya Chuo cha Taaluma za Sayansi ya Afya, lililogharamiwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa ushirikiano na Serikali ya Oman, huko Mbweni, nje ya Mji wa Unguja leo, wakimsikiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, wakati alipokuwa akitoa nasaha zake.

SERIKALI ya Mapinduzi Zanzibar imewahakikishia watumishi wa sekta ya afya kuwa changamoto zinazowakabili, ikiwemo maslahi yao, zinatafutiwa ufumbuzi hatua kwa hatua ili waweze kutoa huduma vizuri kwa wananchi.
Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein leo wakati akifungua majengo mapya ya Chuo cha Taaluma ya Sayansi za Afya kilichoko Mbweni,Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibu Unguja.
Amesema, “Serikali inachukua jitihada mbalimbali za kuendelea kuimarisha mazingira ya kufanyia kazi kwa watumishi wetu wa sekta ya afya kwa kutambua umuhimu wao” na kuongeza kuwa maslahi ya watumishi hao yataboreshwa kadri uchumi utakavyoruhusu na kwa kuzingatia miundo ya utumishi iiyopitishwa hivi karibuni.
Amesema changamoto kubwa inayoikabili Serikali katika kutekeleza azma hiyo ni ukosefu wa fedha jambo ambalo alikiri kuwa si kwa Serikali yake tu bali katika nchi nyingi duniani.  
Dk. Shein aliwaambia wanachuo na wageni waliohudhuria hafla hiyo kuwa Serikali itajitahidi kuhakikisha kuwa ajira kwa wanafunzi wanaohitimu mafunzo katika sekta ya afya hazicheleweshwi na kwamba zitafanyika kwa kuzingatia muundo wa utumishi kwa watumishi wa sekta hiyo.
Katika hotuba yeke hiyo Rais wa Zanzibar ametangaza rasmi uamuzi wa Serikali wa kukiweka chuo hicho chini ya Uongozi wa Chuo Kikuu cha Taifa Zanzibar –SUZA.
“Tumeamua chuo hiki kiwe chini ya uongozi wa SUZA bila ya kubadili mitaala yake ya masomo na kwamba taratibu za mabadiliko haya yanashughulikiwa na kamati iliyoundwa kufanya kazi hiyo”alieleza Dk. Shein na kusisitiza kuwa hakuna mjadala tena wa jambo hilo.
Sambamba na kutangaza uamuzi huo Dk. Shein ametoa wito kwa Wizara na Uongozi wa Chuo cha afya kukubali mabadiliko vinginevyo watabaki nyumba wakati wengine wakisonga mbele.
“wito wangu kwa uongozi wa Chuo na Wizara ya Afya msikatae mabadiliko mtaachwa nyuma.Msiwe wagumu kukubali mabadiliko. Msipokubali wengine wataendelea sisi tutabaki nyuma.”Alisisitiza na kuongeza kuwa chuo hicho kina kazi kubwa ya kutoa watumishi kukidhi mahitaji ya huduma ya afya nchini.
Alifafanua kuwa chini ya mpango wa serikali wa kuimarisha huduma za afya nchini sekta hiyo inahitaji watumishi wengi wenye sifa na Chuo hicho ni miongoni mwa vyuo vinavyotegemewa na Serikali kutoa wataalamu hao.
Alibainisha kuwa Serikali inatambua jukumu lake la kikatiba la kulinda uhai na afya za wananchi wake lakini wajibu wa kuitekeleza haki hiyo unahitaji ushirikiano kati ya serikali, watumishi wa sekta ya afya na jamii kwa jumla.
Kwa hiyo alitoa wito kwa wahitimu wa vyuo vya afya kubaki nchini kuwatumikia wananchi wenzao wanaowategemea badala ya kukimbilia sehemu nyingine.
“napenda nikusihini vijana nyote mnaopata fursa hii kuwa wazalendo na mapenzi kwa jamii yenu inayowategemeeni kuihudumia”aliwaambia Dk. Shein na kuwataka wanapomaliza masomo yao kufanyakazi katika hospitali na vituo vya afya humu nchini.
Hata hivyo alisema Serikali si kwamba inawakataza kabisa wahitimu hao isipokuwa wengine hukimbia bila ya kuomba ruhusa hivyo utaratibu umeandaliwa na Serikali wahitimu hao kurejesha gharama za masomo yao kwa Serikali.
“hatumkatazi mtu kwenda atakako lakini Serikali tumeweka utaratibu mzuri mzazi wa mhitimu kurejesha gharama za mafunzo ya mtoto wake na tumeziagiza Wizara za Fedha, Elimu na Ajira kushughulikia utekelezaji wa utaratibu huo” alisema Dk. Shein.
Katika hotuba yake hiyo kwa wanachuo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali itaendelea na jitihada zake za kuimarisha sekta ya afya nchini kwa kuchukua hatua zifaazo.
Alizitaja baadhi ya hatua hizo kuwa ni pamoja na kutilia mkazo katika usambazaji wa huduma, ubora wa vifaa na miundombinu na kuimarisha utoaji na upatikanaji wa mafunzo mbalimbali kwa watumishi wa afya.
Katika mnasaba huo aliwashukuru washirika wa maendeleo kwa kuziunga mkono jitihada hizo za serikali na kueleza kitendo hicho ni uthibitisho wa uhusiano mzuri uliopo kati ya serikali na washirika hao wa maendeleo.
“tunafarijika kuona washirika wetu mbalimbali wa maendeleo na Taasisi za Kimataifa wamekuwa wakituunga mkono katika juhudi zetu hizi” na kutoa shukrani maalum kwa Serikali ya Ufalme wa Oman kwa msaada mkubwa katika ujenzi wa chuo hicho.
Dk. Shein aliyataja mashirika mengine ya kimataifa yaliyosaidia chuo hicho kuwa ni pamoja na Shirika la Maendeleo la Denmark-DANIDA, Shirikika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia Idadi ya Watu-UNFPA, Benki ya Maendeleo ya Afrika-ADB na Shirika la Afya Ulimwenguni-WHO.
Akimkaribisha mgeni Rasmi Waziri wa Afya Juma Duni Haji alieleza kuwa kukamilika kwa ujenzi wa majengo hayo matatu ambayo moja ni la madarasa na mawili mabweni ya wanafunzi wa kike kunadhihirisha namna hatua kwa hatua chuo hicho kinavyoimarika.
“tangu mwaka 1989 ambapo chuo hicho kilipata majengo yake kwa msaada wa Ufalme wa Oman kimeendelea kujiimarisha kwa kupata usajili rasmi Baraza la NACTE ambao unakifanya Chuo kutambulika kitaifa na kimataifa pamoja na kuanzisha kozi nyingi zaidi” alisema Waziri.
Akizungumza katika hafla hiyo Mshauri wa Waziri wa Afya wa Ufalme wa Oman Dk. Sultan Al-Busaid alisema msaada wa Serikali ya Ufalme wa Oman kwa Zanzibar unaonyesha uhusiano maalum uliopo kati ya nchi mbili hizo.
Kwa hiyo alieleza kuwa wananchi wa Zanzibar watarajie misaada zaidi katika kutekeleza miradi ya sekta afya ambayo ina umuhimu wa kipekee kwa ustawi wa nchi.
Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dk. Saleh Jidawi alieleza kuwa ujenzi wa majengo hayo umegharimu jumla ya dola za kimarekani milioni 2.6.   
Viongozi mbalimbali walihudhuria hafla hiyo akiwemo Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi pamoja na mawaziri na makatibu wakuu.

No comments:

Post a Comment