TANGAZO


Saturday, September 14, 2013

Dk. Shein ajuilia hali Padri aliyemwagiwa tindikali, Anselmo Mwang’amba wa Kanisa Katoliki, Machui Unguja

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein,akisalimiana na Padri Joseph Monesmo Magamba, wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui, alipofika katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kumpa pole, Mjini Unguja, baada ya kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikana katika Mtaa wa Mlandege Mkoa wa Mjini Magharibi jana jioni. Padri alimwagiwa tindikali alipokuwa akitoka kupata huduma ya Mtandao. (Picha na Ramadhan Othman, Ikulu)
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk.Ali Mohamed Shein, akimsikiliza Padri Joseph Monesmo Magamba wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui,akitoa maelezo jinsi alivyopata mkasa wa kutiwa tindikali jana na watu wasiojulikanwa,katika mtaa wa Mlandege Mjini Unguja, alipofika katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kumpa pole,ambapo amelazwa na kuapatiwa matibabu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akiwafariji jamaa  na wafuasi wa Padri Joseph Monesmo Magamba wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui,waliofika katika Hospitali ya Mnazi Mmoja kumpa pole Padri huyo baada ya kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikanwa jana jioni Mtaa wa Mlandege Mjni Unguja.
Mmoja wa Ngugu wa Padri Joseph Monesmo Magamba wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui, akimueleza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, hisia zake kwa uchungu kutokana na kitendo hicho cha kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikanwa  kwamba zilichukuliwe hatua za kisheria na kukomeshwa vitendo kama hivyo.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,akifafanua jambo wakati alipokuwa akiwafariji jamaa na wafuasi wa Padri Joseph Monesmo Magamba wa Kanisa la Romani Katoliki Parokia ya Machui, waliofika kumuangalia Padri huyo aliyelazwa katika Hospitali ya Mnazi Mmoja baada ya kumwagiwa tindikali na watu wasiojulikanwa jana jioni katika Mtaa wa Mlandege Mjini Unguja.

Na Said Ameir, Zanzibar
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa Jeshi la Polisi nchini kujitahidi kuimarisha uchunguzi wa matukio ya watu kumwagiwa tindikali ili wahusika wapelekwe kwenye vyombo vya sheria.
Dk. Shein ametoa wito huo leo, huko Hospitali la Mnazi Mmoja mjini Unguja alipokwenda kumjulia hali Padri Anselmo Mwang’amba wa Kanisa Katoliki, Machui Unguja, ambae amelazwa katika hospitali hiyo kufuatia kumwagiwa tindikali jana jioni.
“hatuwezi kuviacha vitendo hivi viendelee... ni lazima Jeshi la Polisi lijitahidi kuwatafuta wahusika ili sheria ichukue mkondo wake” alisisitiza Dk. Shein.
Amekieleza kitendo hicho kuwa ni cha kikatili na kisichovumika na kuongeza kuwa wahusika lazima wasakwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.
Dk. Shein amesema amesikitishwa na kitendo hicho na kumpa pole Padri Mwang’amba na kumuomba Mwenzi Mungu ampe nafuu haraka apone ili endelee kuitumikia jamii.
Akizungumza na waumini wa kanisa hilo nje ya Wodi alipolazwa Padri huyo Dk. Shein aliwataka waumini hao kuwa na subira wakati Serikali ikichukua hatua kukabiliana na kitendo hicho.
“Ni jambo la kusikitisha kumfikisha binadamu wenzako katika hali kama hii ya majonzi. Hakuna anayeyataka haya. Tuwe wastahamilivu Serikali tunachukua hatua”aliwaambia waumini hao.
Akizungumzia hali yake, Padri Mwang’mba alimueleza Rais kuwa hali yake ni nzuri na anaona vizuri lakini anatarajia kupata nafuu zaidi baada ya uvimbe kupungua sehemu za machoni.
“Hali yangu ni nzuri lakini natarajia uvimbe ukipungua nitaona vizuri zaidi” alisema Padri Mwang’amba na kuongeza kuwa ilikuwa ni bahati kwake hakuathirika sana.
Amefafanua kuwa tukio hilo lilitokea eneo la Mlandege jioni wakati akitoka katika ofisi moja inayotoa huduma za intaneti/mtandao katika eneo hilo ndipo akatokea kijana mmoja na kumwagia tindikali.
Wakati huo huo Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya Dk. Mohamed Saleh Jidawi akiwa amefuatana na Mkurugenzi wa Hospitali hiyo Dk. Jamala Adam Taibu amesema alipofikishwa katika hospitali hiyo Padri Mwang’amba alipatiwa huduma zote muhimu za matibabu zinazostahiki.

Kuhusu majeraha aliyopata Dk. Jidawi alieleza kuwa kwa ujumla asilimia 30 ya mwili wa Padri Mwang’amba umeathirika na kidogo sehemu za macho. 

No comments:

Post a Comment