TAARIFA YA MAWASILIANO YA
SERIKALI KWA UMMA KUHUSU MRADI WA MABASI YAENDAYO HARAKA KATIKA JIJI
LA DAR ES SALAAM
(DAR RAPID TRANSIT – DART)
1.0 UTANGULIZI
1.1 UANZISHWAJI WA WAKALA
Wakala wa Mabasi
Yaendayo Haraka (Dar Rapid Transit - DART) ulianzishwa kupitia Notisi ya
Serikali, Namba 120 ya tarehe 25 Mei 2007 na kuzinduliwa rasmi tarehe 16 Juni
2008 ili kuongeza ufanisi wa utekelezaji wa Mfumo wa Usafiri wa Haraka. Wakala
una malengo makuu matatu ya utekelezaji;
(i)
Kusimamia utekelezaji na uendeshaji wa Mfumo wa Mabasi
Yaendayo Haraka katika Jiji la Dar es Salaam;
(ii)
Kuweka mpangilio
makini wa matumizi ya barabara kuu na ndogo kwa
watumiaji wote ili kupunguza msongamano; na
(iii) Kuhakikisha kuwepo kwa menejimenti ya Wakala
wa Mabasi Yaendayo Haraka yenye kuleta
tija na ufanisi.
1.2 DIRA YA MFUMO WA DART
Kuwa na usafiri bora wa umma
wenye gharama nafuu unaotumia mabasi ya ujazo mkubwa yaendayo kwenye njia
maalum uzingatiao mazingira na kwenda kwa wakati.
kutoa huduma
bora na nafuu Jijini Dar es Salaam na kuleta ukuaji wa uchumi endelevu kwa wananchi na kuwa kichocheo baina ya sekta ya umma na sekta binafsi
katika nyanja ya usafirishaji wa umma mijini.
2.0 MRADI WA MABASI YAENDAYO HARAKA
Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART)
ulibuniwa mwaka 2002 chini ya Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam. Utekelezaji
wake ulianza kwa kazi ya Usanifu wa mradi ambao ulifanyika
kwa hatua kuu mbili.
2.1 USANIFU WA MRADI
Usanifu wa
Ujumla (mwaka 2005) uliofanikisha kupatikana kwa michoro ya awali, makadirio ya
gharama na mchanganuo wa kibiashara (business plan) pamoja na jinsi ambavyo
mradi ungeweza kutekelezwa kwa awamu sita kama ifuatav
AWAMU
|
BARABARA ZITAKAZOHUSIKA
|
UREFU (KM)
|
1
|
Morogoro, Kawawa (kaskazini),
Msimbazi, Kivukoni
|
20.9
|
2
|
Kilwa, Kawawa (kusini)
|
19.3
|
3
|
Nyerere, Uhuru, Bi Titi, Azikiwe
|
23.6
|
4
|
Bagamoyo na Barabara ya Sam Nujoma
|
16.1
|
5
|
Mandela, Barabara mpya
|
22.8
|
6
|
Old Bagamoyo, na barabara mpya mbili
|
27.6
|
|
JUMLA
|
130.3
|
2.2 USANIFU
WA KINA
Usanifu wa kina wa miundombinu ya
awamu ya kwanza ambayo inajumuisha pamoja na njia maalum za mabasi, vituo
vikuu (terminals) 5, vituo vya mabasi 29 na vituo vya maegesho (Bus depot) 2
ulikamilika mwaka 2007. Mradi pia utahusisha ujenzi wa njia maalumu za waenda
kwa miguu na baiskeli na vivutio vya mji kama vile bustani za
mapumziko (Kwa ushirikiano na sekta binafsi).Kufuatia usanifu huo, Halmashauri
ya Jiji iliiomba Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(TAMISEMI) kuanzisha Wakala ambao utatekeleza mradi wa DART na masuala mengine
ya usafiri hususan usafiri wa umma.
2.3
JUKUMU LA WAKALA
Jukumu kuu la Wakala katika kipindi hiki ni
utekelezaji wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (Dar Rapid Transit –
DART). Mradi huu unalenga katika kuongeza tija na ufanisi katika kuchochea kasi
ya maendeleo katika Jiji la Dar es salaam na taifa zima kwa ujumla hasa
tukizingatia zaidi ya 80% ya pato la ndani la Taifa linachangiwa na Jiji la Dar
es salaam.
Sheria na taratibu
zinazoongoza utekelezaji wa mradi huu, ni pamoja na makubaliano (Financing Agreement)
kati ya serikali na Benki ya Dunia, Sheria ya Ardhi na Mwongozo (Resettlement
Action Plan) kuhusu ulipaji wa fidia kwa mali na watu watakaoathiriwa na ujenzi
wa miundombinu ya mradi. Pia sheria
iliyoanzisha SUMATRA inazingatiwa kikamilifu katika maandalizi ya utoaji
huduma.
2.4 GHARAMA ZA MRADI
Mradi unagharimiwa na
fedha toka Benki ya Dunia (Dola za Kimarekani
325.37 milioni na Serikali ya
Tanzania imechangia shilingi 23.5
Bilioni kwa ajili ya kugharimia ulipaji fidia mali zilizoathiriwa na
miundombinu ya mradi. Sekta binafsi inatarajiwa kuchangia Dola za Kimarekani 100 milioni kwa ajili ya kuwekeza
kwenye ununuzi wa mabasi na mfumo wa kisasa wa ukusanyaji nauli na utunzaji wa
fedha zinazotokana na mfumo.
Mchango wa Serikali Kuu
pia inachangia gharama za Mishahara,Fedha za uendeshaji wa Wakala za Matumizi
ya Kawaida na vifaa vya uendeshaji na usimamizi wa mradi.
Utekelezaji wa mradi
huu unashirikisha wadau mbalimbali wakiwamo wakazi wa Jiji la Dar es salaam
pamoja na vitongoji vyake. Aidha, wadau wakuu
ni pamoja na Ofisi ya Waziri Mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Wizara
ya Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Wizara ya Ujenzi,Wizara ya Mawasiliano
na Uchukuzi, Wizara ya fedha na Ofisi ya
Rais Tume ya Mipango, Mamlaka ya Usafiri wa Nchi kavu na Majini (SUMATRA), Wakala
wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mamlaka ya Serikali za Mitaa katika Jiji la
Dar es Salaam, Benki ya Dunia, na Chama cha Wamiliki wa Daladala (DARCOBOA).
Katika Kipindi
cha utekelezaji cha Mwaka 2010/2011 na 2011/12 Ujenzi wa
miundombinu awamu ya kwanza ulianza kutekelezwa kwa kushirikiana
na Wakala wa Taifa wa Barabara (TANROADS) kufuatia uzinduzi rasmi uliofanywa na
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dk. Jakaya Mrisho Kikwete,
tarehe 10 Agosti 2010 katika eneo la Kituo cha Mabasi cha Kivukoni.
Katika kipindi hicho,
Makandarasi walioanza shughuli za ujenzi ni pamoja na Beijing Construction Engineering Company anayejenga Kituo cha
Kivukoni, Vituo Mlisho. Mkandarasi Mkuu wa ujenzi wa Awamu ya Kwanza ya
njia maalum za DART kampuni ya Strabag ya Ujerumani ilipatikana katika kipindi hiki cha
utekelezaji cha Mwaka 2011/2012.
2.5 UTEKELEZAJI wa shughuli
zilizopangwa na gharama ya fedha kwa mwaka 2012/13
Shughuli
kubwa katika kipindi hiki ni ujenzi wa miundombinu ya mfumo awamu ya 1
unaendelea kwenye barabara ya Morogoro kuanzia Kimara mpaka mjini kati na
Kivukoni ambao unatarajia kukamilika mwaka 2014. Ujenzi wa Barabara ya Kawawa kuanzia
Magomeni mpaka Morocco na Mtaa wa Msimbazi eneo la FIRE mpaka Gerezani Kota
ujenzi utakamilika mwaka 2015.
Katika awamu hii
ya kwanza, mtandao wa barabara za DART unahusisha njia kuu kuanzia Kituo Kikuu
cha Kivukoni, karibu na kivuko cha kigamboni na kupitia Kivukoni Front hadi
barabara ya Morogoro, na kuishia katika Kituo Kikuu cha Kimara, kwa kupitia
Kituo Kikuu cha Ubungo karibu na makutano
ya barabara ya Nelson Mandela /
Sam Nujoma. Aidha, awamu hii ya kwanza inajumuisha ujenzi wa matawi mawili ya
Barabara ya Kawawa kutoka Magomeni hadi Kituo Kikuu cha Morocco na Mtaa wa
Msimbazi ikiishia Kituo Kikuu cha Kariakoo.
2.6 Usimamizi wa Ujenzi wa Miundombinu
Utekelezaji wa Ujenzi wa Miundombinu ya
Awamu ya Kwanza ya Mradi wa Mabasi ya Haraka (DART) Dar es Salaam –,
unasimamiwa na kampuni ya ushauri kutoka nchini Australia iitwayo SMEC International Pty. Mkataba wa
usimamizi wa utekelezaji wa mradi huu, kati ya kampuni hiyo na Mtendaji Mkuu wa
Wakala wa Barabara (TANROADS) kwa niaba ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania ulitiwa saini tarehe 16 Julai 2009. Mkataba wa usimamizi wa ujenzi wa
miundombinu ya mradi huu utagharimu shilingi bilioni 2.5.
3.0 UJENZI WA MIUNDOMBINU
Ujenzi wa Miundombinu ya DART Awamu ya Kwanza unajumuisha
miundombinu ifuatayo:
3.3.1 Barabara
Ujenzi wa barabara yenye urefu wa jumla ya
kilomita 20.9 ambao unajumuisha barabara ya Morogoro kutoka Kimara hadi Kivukoni,
Barabara ya Msimbazi kutoka Fire hadi Kariakoo- Gerezani na sehemu ya barabara
ya Kawawa kutoka Magomeni hadi Morocco.Ujenzi unahusisha njia maalumu za
mabasi ya DART ambazo zinajengwa
katikati ya barabara kwa zege (cement concrete). Barabara hizi zitakuwa na njia
moja kwa kila mwelekeo zenye upana wa wastani wa mita 3.5 kutegemeana na upana
toka sehemu moja hadi nyingine. Katika sehemu za vituo vya mabasi, kutakuwa na
njia mbili kila mwelekeo kuwezesha basi moja kupita basi jingine.
Aidha, kunajengwa njia mbili kwa kila mwelekeo
kwa ajili ya magari mchanganyiko.Barabara za magari mchanganyiko zinajengwa kwa
lami kama kawaida. Aidha Sehemu ya kutoka Kibo hadi Kimara inajengwa njia moja
kwa magari mchanganyiko kwa kila mwelekeo. Mtaa wa Msimbazi, utajengwa barabara
moja moja ya mabasi na magari mchanganyiko kwa kila mwelekeo.
Sehemu ya barabara ya Morogoro kutoka makutano
ya barabara ya Bibi Titi na barabara ya
Sokoine, kunajengwa njia maalumu za mabasi moja kwa kila mwelekeo pamoja na
njia za waendao kwa miguu tu. Magari mchanganyiko hayatakuwa na njia ya kupita
katika kipande hiki.Vizuizi vitawekwa ili kutenganisha njia ya mabasi na ile ya
waendao kwa miguu.Kivukoni Front, kumepangwa kujengwa barabara moja ya magari
mchanganyiko kwa mwelekeo mmoja tu. Tathmini inafanywa kuangalia uwezekano wa
kuongeza njia ya pili kwa mwelekeo mwingine.
3.3.2 Vituo
vidogo
Vituo vidogo vya abiria (Bus Stations)
vinajengwa katikati ya barabara. Awali, ilipangwa kujengwa vituo vidogo 29; lakini kutokana na sababu za
kiufundi na uendeshaji, vituo viwili vimeondolewa yaani kituo cha Chai Bora
karibu na Tanesco Ubungo na kituo cha Kempiski mbele ya hoteli ya Kilimanjaro.
Vituo vitakuwa na uwezo wa kuhudumia mabasi 65 kwa saa kwa kila mwelekeo.
3.3.3 Vituo Mlisho (Feeder Stations)
Kutakuwa na Vituo Mlisho (Feeder Stations) sita (6) katika maeneo ya Shekilango, Urafiki, Kinondoni A,Mwinjuma, Magomeni na Fire.Vituo hivi ndiko mabasi madogo yatakapokuwa yakishusha na kupakia abiria waingiao na kutoka katika mfumo wa mabasi makubwa wa DART aidha wakitokea au kuelekea maeneo ambayo mfumo huo wa mabasi makubwa bado haujafika.
3.3.4 Vituo Vikuu (Terminals)
Kutakuwa na Vituo Vikuu (Terminals) vitano (5) katika maeneo ya Kimara, Ubungo, Morocco, Kariakoo, na Kivukoni.Vituo hivi ndiko mabasi yatakapokuwa yanaanzia na kumalizia safari. Vitakuwa mahsusi kwa ajili ya kubadilishana abiria kati ya njia kuu na njia mlisho (feeder roads). Hivi vitakuwa vikubwa na vya kisasa ili kutoa nafasi ya kuweza kuanzishwa kwa huduma za ziada kwenye vituo hivyo na kuruhusu aina nyingine za huduma za usafiri nje ya vituo.
3.3.5 Karakana ya Mabasi (Depot)
Kutakuwa na karakana mbili (2) katika maeneo
ya Ubungo na Jangwani.Mabasi yatasafishwa na kukarabatiwa kwenye karakana hizo.
Karakana zitakuwa za kisasa zitakazotoa huduma ya kutosha kwa mabasi kama
ukaguzi, usafishaji na ukarabati na sehemu ya kuegeshea mpaka siku ya pili.
3.3.6
Madaraja na Njia za waenda kwa Miguu
Ujenzi utahusisha njia maalumu za waenda kwa
miguu na watumia baiskeli. Aidha kutakuwa na madaraja maalum ya waenda kwa
miguu kwa kuvuka toka Vituo mlisho kwenda vituo vya mabasi ya BRT. Madaraja
hayo yanajengwa katika vituo vikuu katika maeneo ya Kimara, Ubungo na Morocco.
3.3.7 Miundombinu mingine
Daraja la Msimbazi eneo la Jangwani linapanuliwa
sambamba na ongezeko la njia maalumu za mabasi, baiskeli na waendao kwa miguu.
Aidha, upanuzi huo unajumuisha ujenzi wa vyuma vya kuzuia ajali, vya kuongoza
magari na njia za waendao kwa miguu. Njia ya waendao kwa miguu iliyopo sasa na
sehemu ya ukingo wa barabara vitaondolewa ili kutoa nafasi ya ujenzi wa njia
mpya.
Utekelezaji wa ujenzi
wa miundombinu ya awamu ya kwanza ya mradi unaendelea kwa mgawanyo wa vipengele
(Work packages) saba (7) vya mikataba.
Usimamizi wa ujenzi wa awamu ya kwanza upo mikononi mwa TANROADS Makao
Mkuu kwa mujibu wa makubaliano (Memorundum of Understanding-MOU) na
Wakala wa DART ya tarehe 16 Juni 2008).
3.3.8 Hali halisi ya ujenzi
Kwa ujumla ujenzi
unaendelea vizuri katika maeneo mengi katika awamu hii ya kwanza. Mathalani
tukiangalia twakimu za ujenzi kwa mradi mzima ni zaidi ya asilimia 30 hii ikiwa
ni pamoja na usanifu wa michoro na ujenzi wa miundombinu ambao unahusisha
ujenzi wa barabara za magari yaendayo haraka, watembea kwa miguu, vivuko,
waendesha baiskeli, karakana za mabasi maeneo ya Jangwani na Ubungo na vituo
vya mabasi. Mpango wa awali, malengo ni asilimia 50 lakini kutokana na
changamoto za ujenzi malengo haya hayakuweza kufikiwa. Changamoto
zilizojitokeza ni pamoja na kuchelewa kupatikana kwa maeneo ya ujenzi- baadhi ya wafidiwa waligoma
na kufungua kesi mahakamani.
4.0 MPANGILIO
WA UTOAJI HUDUMA
Utoaji huduma kwenye
mfumo wa DART unahusisha zaidi Sekta binafsi. Sekta binafsi inatarajia kuwekeza
kiasi cha Dolla za Kimarekani 100 milioni kwa ajili ya ununuzi wa mabasi, na mfumo wa ukusanyaji wa
nauli na utunzaji wa fedha ambazo pia zinatakiwa kuwa tayari mfumo unapoanza kazi. Yafuatayo yamefanyika kuhakikisha
malengo ya utoaji huduma yanafanikiwa.
Makabrasha zabuni za ununuzi wa mabasi,
uwekezaji kwenye mfumo wa ukusanyaji nauli na utunzaji wa fedha zinafanyiwa
mapitio ili zilingane na uhalisia kitakwimu na kiuendeshaji kutokana na muda
mwingi kupita tangu ziandaliwe. Kazi ya mapitio ya makabrasha ya zabuni inatarajiwa
kukamilika mwezi Septemba 2013.
Wakala wa DART pia umefanikiwa kumpata Mshauri
Mwelekezi Mkuu (Chief Technical Advisor)
ambaye atasaidia wakala kufanikisha azma yake ya kukamilisha utekelezaji wa
shughuli za ujenzi wa miundombinu na upatikanaji wa watoa huduma katika mfumo
wa DART wanapatikana katika muda uliopangwa. Wakala unaendelea na mchakato wa kumpata mtaalam (Trasaction Advisor) atakayeongoza
mchakato wa zabuni kazi ambayo imepangwa ianze mwezi Oktoba 2013. Aidha kabla
ya kuanza machakato wa zabuni za watoa huduma katika mfumo..
5.0 SHUGHULI NYINGINE KUFANIKISHA MRADI
5.1 Usimamizi, Uratibu Na
Ushirikishwaji Wadau
Kupitia Ofisi ya
Waziri Mkuu - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa ziliundwa
Kamati za kusaidia kuongeza kasi ya utekelezaji na usimamizi ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka
(DART). Kamati zilizoundwa ni pamoja na Kamati ya Usimamizi inayoongozwa na
Meya wa Jiji, Kamati ya Ufundi na Kamati ya Uratibu. Kamati hizi kwa kiasi
kikubwa zimesaidia sana kusukuma kasi ya utekelezaji wa Mradi na kutoa msukumo
mkubwa katika kutatua changamoto zilizojitokeza.
Aidha Bodi ya Ushauri ya Wizara (Ministerial Advisory Board) ilizinduliwa tarehe 19 Julai, 2013. Kuzinduliwa
kwa Bodi hii kutaendelea kuimarisha usimamizi na uratibu wa mradi.
5.2 Uandaaji Rasimu ya Mwongozo wa Sera ya kuwahusisha wamiliki wa
Daladala katika mfumo wa DART
Katika utekelezaji wa Mradi wa mabasi
Yaendayo Haraka awamu ya kwanza jumla ya daladala 1,600 zitahamishwa sehemu
nyingine kupisha utekelezaji wa mradi wa mabasi Yendayo Haraka Katika Jiji la
Dar es Salaam.Wakala hivi sasa kwa kushirikiana na wadau unandaa rasimu ya
mwongozo wa sera ya ushirikishaji wamilki wa Daladala ‘’Daladala Transition Policy
Framework’’. Aidha Wakala unandaa Mkutano maalumu na wamilki wote wa
daladala ili kuendelea kuwahamasisha wajiunge katika Makampuni na baadaye
kununua hisa katika uendeshaji wa mabasi yaendayo haraka.
5.3 Ulipaji Fidia
Ulipaji wa fidia ulianza mwaka 2007 na umefikia
hatua za mwisho. Maeneo matatu yaliyokuwa yamebaki yamekamilishwa katika
kipindi hiki cha ujenzi.
·
Kituo Kikuu cha
mabasi cha Ubungo:
Zoezi la ulipaji wa
fidia katika Kituo Kikuu cha mabasi cha
Ubungo limekamilika. Hadi kufikia Juni 2013 ya wafanyabishara wote 230 sawa na asilimia 100 walikuwa
wamelipwa fidia zao na kuhama kupisha ujenzi wa miundombinu ya mfumo
DART.
Magomeni – Bondeni:
Kwa upande wa fidia
ya Magomeni – Bondeni wakazi wote 42 waliokuwa wanadai fidia wamelipwa na
kupisha uhamishaji wa nguzo za umeme na kazi ya uhamishaji imekamilika.
·
Kariakoo Gerezani:
Kwa upande wa
waliokuwa wakazi wa Kariakoo Gerezani – Kota Jumla ya wakazi 81 kati ya 106 wamekwisha chukua fidia
zao. Bado kuna baadhi ya waliokuwa wakazi wa eneo la Kariakoo Gerezani ambao
bado wanaoendelea na shauri dhidi ya Wakala wa Majengo (TBA).
5.4 Usanifu
wa Awamu ya 2 Na 3:
Kampuni ya Ushauri ya
M/S Kyong Dong Engineering Co. LTD ya Korea iliyosaini mkataba tarehe 25
Februari 2011 kwa ajili ya kusanifu Miundombinu ya DART awamu ya Pili na ya Tatu kazi ambayo inatarajiwa kukamilika mwezi
Desemba 2013, baada ya kulazimika kuongezewa muda kutokana na changamoto
zinaojitokeza. Changamoto kuu kwenye usanifu wa kina hususan ugumu wa
upatikanaji wa maeneo ya ujenzi wa vituo vikuu na Maegesho.
6.0 CHANGAMOTO
Changamoto kuu ya mradi huu kwa sasa ni:
·
Upatikanaji wa fedha za kulipa fidia kwa
wakati.
·
Upatikanaji wa maeneo ya ujenzi.
·
Uondoaji wa vikwazo vinavyojitokeza wakati
wa ujenzi
·
Kesi zisizoisha kuhusiana na eneo la Gerezani,
waliokuwa wakazi wameendelea kufungua kesi ambazo hazina msingi.
·
Kuwawezesha wamiliki wa Daladala wauelewe
mfumo na kujipanga. Juhudi za kuwaandaa hazijazaleta
mafanikio yanayokusudiwa kutokana na mtazamo wa kunyang’anywa biashara.
·
Ufinyu wa Bajeti.
7.0 KAZI
ZILIZOPENDEKEZWA KUTEKELEZWA KATIKA MWAKA WA FEDHA 2013/14
Serikali imejipanga kuhakikisha ujenzi wa
miundombinu unakamilika kwa wakati na upatikanaji wa watoa huduma ya mfumo wa
Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Katika Jiji la Dar es Salaam unafanikiwa. Mambo
ya msingi yatakayo tekelezwa ni pamoja na:-
·
Kufuatilia kwa
karibu maendeleo ya ujenzi wa miundombinu ya mfumo wa DART kwa kushirikiana na Wakala wa Barabara wa Tanzania
(TANROADS) ili ujenzi ukamilike kabla ya Julai 2015;
·
Kukamilisha mikataba na manunuzi ya watoa huduma katika
mfumo wa DART watakaohusika katika ununuzi wa mabasi, ukusanyaji wa nauli na
usimamizi wa fedha mwaka wa Fedha 2013/14;
·
Kukamilisha usanifu na kuanza ujenzi wa kituo cha
Mawasiliano ya Mfumo wa DART;
·
Kufanikisha ufuatiliaji wa fedha kwa ajili ya ujenzi wa
miundombinu awamu ya 2 na 3;
·
Kufanikisha
ukarabati wa barabara za mlisho (feeder roads), za mfumo wa DART awamu ya
kwanza kupitia Halmashauri za Manispaa za Ilala na Kinondoni kabla ya mfumo
kuanza Julai 2015;
·
Kufanya mkutano maalum (Road show) ili kuwatafuta Wawekezaji
katika mfumo wa DART;
·
Kuhakikisha Miundombinu ya Mfumo wa DART inayokamilika
kujengwa na inayoendelea inalindwa na kutunzwa ipasavyo kabla ya mfumo kuanza;
·
Kubuni na kuweka
Mikakati ya Kutafuta vyanzo vya mapato katika mfumo wa DART kuipunguzia
Serikali gharama;
·
Kutoa mafunzo, usimamizi na uendeshaji wa mradi kupitia
vikao vya Kamati ya uratibu, Ufundi, Usimamizi na Bodi ya Ushauri ya Wizara na
vikao vya wadau mbalimbali katika Mfumo wa DART kwa mujibu wa sheria.
·
Kukamilisha usanifu wa kina kwa Awamu ya pili na ya
tatu ambao unafanywa na kampuni ya
Ushauri ya M/S Kyong Dong Engineering Co. LTD ya Korea kufuatia mkataba
uliosainiwa tarehe 25 Februari 2011 kwa ajili ya kusanifu Miundombinu ya DART
awamu ya Pili na Tatu.
8.0 HITIMISHO
Utekelezaji na kukamilika
wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ni muhimu sana hata hivyo juhudi zaidi za
pamoja na kwa kushirikisha Wadau wote zinahitajika. Lengo ni kuhakikisha mfumo DART
unaanza kutoa huduma Julai 2015 au mapema zaidi ili kuwaondolea adha ya usafiri
wakazi wa Dar es salaam pamoja na kuhakikisha kuwa msongamano wa magari katika
barabara zake unapungua au kuondoka kabisa.
Ili kufikia lengo
hilo mapema, mradi huu umepewa kipaumbele na Serikali na uko katika Mpango
maalumu wa ”Matokeo Makubwa Sasa’’ (Big Result Now) chini ya usimamizi wa
kitengo cha Ofisi ya Rais kinachoitwa “President’s Delivery Unit”.
No comments:
Post a Comment