Msanii wa filamu Elizabeth Michael (Lulu) akieleza jambo mbele ya Katibu Mtendaji Bodi ya Filamu Tanzania Bi. Joyce Fissoo wakati kampuni yake ya Proin Promotions ikiwasilisha filamu yake ya “Foolish Age” kwa ajili ya ukaguzi.
Msanii wa filamu Elizabeth Michael (Lulu) akiweka sahihi yake kuashiria amekubaliana na taratibu zote alizoelekezwa na Bodi ya Filamu wakati wa ukaguzi wa filamu yake ya “Foolish Age”.
Jengo jipya la kisasa la
Kampuni ya Proin Promotions ambalo linatarajiwa kuzinduliwa rasmi hivi karibuni
likionekana kwa nje. (Picha zote na Benedict Liwenga-MAELEZO)
Na Benedict
Liwenga-MAELEZO.
KAMPUNI ya Proin
Promotions imewasilisha filamu yake iliyopewa jina la “Foolish Age” Bodi ya
Filamu Tanzania kwa ajili ya ukaguzi ambapo baada ya kufanyiwa marekebisho
filamu hiyo inaweza kuruhusiwa katika uzinduzi wa Kampuni hiyo hivi karibuni.
Bodi ilifikia hatua ya
kuwaita wahusika yaani Proin Promotions na Elizabeth Michael (Lulu) kwa ajili
ya kufanya majadiliano kuhusu maudhui na maadili katika filamu hiyo kabla ya
kufanyia maamuzi.
Katika majadiliano hayo
Bodi ya Filamu iliwakumbusha wahusika hao kufanya baadhi ya marekebisho katika
filamu hiyo ili iweze kuwa kivutio kwa umma, pia Bodi ya Filamu iliwakumbusha
juu ya umuhimu wa kuzingatia kifungu cha 14 cha Sheria ya Filamu na Michezo ya Kuigiza
ambacho kinaipa Bodi mamlaka ya kukagua filamu, matangazo na maelezo yote na
kile cha 24 (1) (d, n na t) cha Kanuni za sheria ya
Filamu na Michezo ya Kuigiza kinachofafanua mambo yanayotakiwa na yale
yasiyotakiwa katika filamu ambayo filamu hiyo imekwenda kinyume.
Kwa upande wake
Mwanasheria wa Kampuni ya Proin Promotions Bi. Gift Msuya alikubaliana na
ushauri uliotolewa na Bodi ya Filamu na aliiomba Bodi itoe muda kwao kwa ajili
ya kufanyia marekebisho katika filamu hiyo.
Naye msanii Elizabeth
Michael (Lulu) aliieleza Bodi ya Filamu kuwa Filamu hiyo aliitengeneza muda
mrefu na kwa sasa atazingatia maelekezo ya sheria, Kanuni na taratibu hususani
katika eneo la maadili. Aidha alikiri kuwa ni kweli maeneo yaliyobainishwa
kweli yanahitaji marekebisho.
Katibu Mtendaji Bodi ya
Filamu Bi Fissoo alimalizia kwa kuishauri Kampuni hiyo kutotumia filamu hiyo
katika uzinduzi wa kampuni yao hadi hapo watakapofanyia marekebisho katika
baadhi ya maeneo muhimu ndani ya filamu hiyo.
Proin Promotions ni
Kampuni inayojikita katika kuandaa na kutengeneza filamu za kitanzania na
kuzisambaza nchini, pia ni kampuni inayotarajiwa kutoa ushindani mkubwa katika
tasnia ya filamu. Kampuni hiyo inatarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni baada ya
maandalizi rasmi kukamilika.
No comments:
Post a Comment