Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa Wakala wa Ukaguzi wa
Madini Tanzania, Bruno Mteta akielezea kwa waandishi wa habari, jinsi Wakala
alivyowezesha Serikali kukusanya mapato katika Sekta ya Madini, wakati wa
mkutano uliofanyika ukumbi wa Idara ya Habari, Maelezo, Dar es Salaam leo.
Kushoto ni Ofisa Habari wa Idara ya Habari, Maelezo, Georgina Misama. (Picha na
Eliphace Marwa)
WAKALA wa Ukaguzi wa
Madini Tanzania (Tanzania Minerals Audit Agency - TMAA) ni Wakala wa
Serikali ulioanzishwa tarehe 2 Novemba, 2009 chini ya Sheria ya
Wakala wa Serikali, Sura ya 245. Tamko la
Waziri la kuanzisha Wakala lilichapishwa kwenye Gazeti la Serikali Namba 362 la
tarehe 6 Novemba, 2009.
Lengo la Wakala ni
kuhakikisha kwamba, Serikali inapata mapato stahiki kutoka kwenye shughuli za
uzalishaji na biashara ya madini nchini kupitia usimamizi na ukaguzi makini wa
shughuli za uchimbaji, na kuhakikisha kuwa shughuli hizo zinafanyika kwa
kuzingatia uhifadhi na utunzaji thabiti wa mazingira katika maeneo ya migodi.
WAJIBU NA MAJUKUMU YA WAKALA
Wajibu na majukumu ya
Wakala ni pamoja na:
1.
Kusimamia
na kuhakiki kiasi na ubora wa madini yanayozalishwa na kuuzwa nje na wachimbaji
wakubwa, wa kati na wadogo kwa lengo la kutathmini mapato halisi ya madini hayo
na kuwezesha ukusanyaji wa mrabaha stahiki;
2.
Kukagua mapato,
gharama za uwekezaji na uendeshaji wa migodi mikubwa na ya kati, kwa lengo la
kukusanya taarifa sahihi za kodi na kuziwasilisha Mamlaka ya Mapato Tanzania na
vyombo vingine husika vya Serikali;
3.
Kufuatilia
na kukagua shughuli za utunzaji wa mazingira katika maeneo ya migodi, bajeti
iliyotengwa na matumizi ya fedha kwa ajili ya ukarabati endelevu wa mazingira
na ufungaji wa migodi;
4.
Kukusanya,
kuchambua, kutafsiri na kusambaza taarifa za uzalishaji na mauzo ya madini nje ya nchi kwa ajili ya
maoteo ya mapato ya Serikali, ili kusaidia katika mipango na utoaji wa maamuzi
ya usimamizi wa shughuli za madini;
5.
Kufuatilia
na kuzuia utoroshaji/magendo ya madini, na ukwepaji wa ulipaji mrabaha kwa
kushirikiana na vyombo na mamlaka
nyingine husika za Serikali;
6.
Kutoa
ushauri kwa Serikali kuhusu masuala yanayohusu usimamizi wa sekta ya madini
hususan katika usimamizi na ukaguzi wa shughuli za uzalishaji na biashara ya
madini ili kuhakikisha Serikali inapata mapato stahiki;
7.
Kuendeleza
shughuli za utafiti na maendeleo katika sekta ya madini kwa lengo la kuongeza
mapato ya Serikali; na
8.
Kutathmini
na kufuatilia utekelezaji wa taarifa za migodi zinazohusu upembuzi yakinifu,
mpango wa uchimbaji, uchimbaji uliofanyika na mpango wa usimamizi na utunzaji
wa mazingira.
MAFANIKIO
Katika kutekeleza
majukumu hayo, Wakala umepata mafanikio makubwa yafuatayo:
1.
Kampuni
zinazomiliki migodi mikubwa ya dhahabu nchini zimelipa kodi ya mapato ikiwa ni
matokeo kazi za ukaguzi wa hesabu za fedha na kodi zilizofanywa na TMAA kwa
kushirikiana na TRA. Katika kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi Machi 2013, jumla ya
Shilingi bilioni 473.8 zimelipwa kama kodi ya
mapato kwa mchanganuo ufuatao:
·
Kampuni ya
Geita Gold Mining Limited inayomiliki Mgodi wa Dhahabu wa Geita imelipa jumla
ya Shilingi bilioni 299.4;
·
Kampuni ya
Resolute Tanzania Limited inayomiliki Mgodi wa Dhahabu wa Golden Pride imelipa
jumla ya Shilingi bilioni 97; na
·
Kampuni ya
Pangea Minerals Limited inayomiliki Mgodi wa Dhahabu wa Tulawaka imelipa jumla
ya Shilingi bilioni 77.4.
2.
Migodi
mikubwa ya dhahabu imelipa ushuru wa mafuta (fuel levy) wa jumla ya Dola za Marekani milioni
2 ambazo zilikuwa hazijalipwa mpaka mwaka 2010.
3.
Migodi mikubwa
imelipa kiasi cha Shilingi bilioni 4.8 kama Kodi ya Zuio kutokana na kushindwa kujumuisha
kodi hiyo katika malipo yaliyofanywa kwa watoa huduma mbalimbali kwa migodi
hiyo kwa kipindi cha mwaka 2009 hadi 2012.
4.
Jumla ya
Shilingi bilioni 2.41 zimelipwa na migodi mikubwa
kama ushuru wa Serikali za Mitaa. Malipo hayo yalikuwa hayajafanywa kwa kipindi
cha mwaka 2004 hadi 2011.
5.
Kiasi cha
Shilingi bilioni 1.15 kimelipwa na migodi mikubwa
kama mrabaha kutokana na ukaguzi na ulinganisho wa takwimu za malipo ya mrabaha
kwa kipindi cha mwaka 2004 hadi 2010. Kiasi
hiki hakijumuishi Shilingi bilioni 317.74 zilizolipwa
kama mrabaha na migodi mikubwa wakati wa kusafirisha madini nje ya nchi kwa
kipindi cha mwaka 2009 hadi 2012.
6.
Kwa
kipindi cha Julai hadi
Disemba 2012, Wakala kwa kushirikiana na Ofisi ya Madini Kanda ya Ziwa
umewezesha ukusanyaji wa Shilingi milioni 230 kama
mrabaha kutokana na kilo 89.52 za dhahabu
zilizozalishwa na wamiliki wa leseni wanaofanya uchenjuaji wa marudio katika
maeneo mbalimbali yaliyopo katika mikoa ya Geita na Mwanza.
7.
Wakala kwa
kushirikiana na Ofisi ya Madini Kanda ya Mashariki, umeendelea kukagua na
kudhibiti shughuli za uzalishaji na mauzo ya madini ya ujenzi katika mikoa ya Dar
es Salaam na Pwani, ukaguzi ambao umeiwezesha Serikali kuongeza maduhuli
yatokanayo na madini hayo. Zoezi hili ambalo lilianza mwezi Juni 2011 linafanyika
kwa ufanisi mkubwa. Mfano, hadi kufikia Disemba 2012, Wakala umewezesha kukusanywa
kwa mrabaha wa Shilingi bilioni 1.47 kutokana
na madini ya ujenzi yaliyozalishwa na kuuzwa na wachimbali halali wa madini ya
ujenzi katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani.
Kiasi hiki ni ongezeko kubwa ukilinganishwa na wastani wa Shilingi
milioni 3 zilizokuwa zinakusanywa na Ofisi ya Madini Kanda ya Mashariki kwa
mwaka kipindi cha nyuma (kabla ya ukaguzi wa TMAA).
8.
Wakala umeanzisha madawati kwenye viwanja vya
ndege vya Dar es Salaam, Kilimanjaro na Mwanza kwa lengo la kuwabaini na
kuwakamata watu wasio waaminifu wanaojaribu kusafirisha madini kinyume cha
sheria. Kwa kupitia madawati hayo,Wakala umeweza kukamata
watoroshaji wa madini aina mbalimbali katika matukio 23 tofauti. Madini
yaliyokamatwa yana thamani ya jumla ya Dola za Marekani 8,231,740, sawa na
Shilingi za Kitanzania bilioni 13.17.
9.
Kaguzi za mazingira zimesaidia kuboresha
shughuli za utunzaji wa mazingira kwenye maeneo ya uchimbaji madini.
Pamoja
na mafanikio hayo, maabara ya kisasa ya Wakala ambayo inatoa huduma kwa niaba
ya Serikali sasa umeanza kutoa huduma za maabara kibiashara kwa wadau
mbalimbali wakiwemo watafiti wa madini, wachimbaji, wafanyabiashara za madini,
wanunuzi na wasafirishaji wa madini wanaohitaji kufanyiwa uchunguzi wa sampuli
za madini ya aina mbalimbali. Uchunguzi
huo unafanyika kwa gharama nafuu ikilinganishwa na maabara za kampuni binafsi
zilizopo nchini.
HITIMISHO
Wakala umejipanga kuendelea na ukaguzi wa shughuli za uchimbaji na biashara
ya madini nchini ili kuhakikisha kuwa Taifa linanufaika ipasavyo na rasilimali
ya madini. Wakala unatoa wito kwa wadau wote kuendelea kutoa ushirikiano ili
kuhakikisha kwamba majukumu ya Wakala yanatekelezwa kikamilifu.
IMETOLEWA NA
WAKALA WA UKAGUZI WA
MADINI TANZANIA
23 AUGUST, 2013
No comments:
Post a Comment