TANGAZO


Wednesday, August 28, 2013

TPSF: Serikali isitishe ugawaji wa vitalu vya gesi

Baadhi ya wajumbe wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania wakiwa katika kikao cha kwanza tangu bodi hiyo kuteuliwa ambapo kilijadili mambo mbalimbali yakiwemo ya uwekezaji nchini. (Picha zote kwa hisani ya Francis Dande) 
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya TPSF, Salum Shamte akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari. 
 Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye akizungumza. 
Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi akifafanua jambo wakati wa mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, juu ya maazimio ya bodi hiyo kuhusu sera ya uwekezaji nchini. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa TPSF, Salum Shamte. 

Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Dk. Reginald Mengi akifafanua jambo wakati wa kikao cha kwanza tangu bodi hiyo iteuliwe. Kushoto ni mjumbe wa Bodi hiyo, Arnold Kileo na Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Godfrey Simbeye akizungumza.



Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imetakiwa kusitisha mara moja mpango wake wa ugawaji wa leseni za vitalu vya gesi hadi hapo itakapopatikana sera ya gesi ili kuwapa fursa watanzania kumiliki vitalu hivyo.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mwenyekiti mpya wa Bodi ya Taasisi ya Uwekezaji nchini (TPSF), Dk. Reginald Mengi, alisema kuwa endapo ugawaji wa vitalu hivyo utafanyika Oktoba mwaka huu kama ilivyopangwa, watanzania hawatakuwa na uwezo wa kumiliki rasilimali hiyo.

Dk. Mengi ambaye alikuwa akizungumzia maazimio ya bodi hiyo iliyokutana mara ya kwanza jana tangu ilipoteuliwa hivi karibuni, alisema wakati Serikali iko mbioni kufanya mnada wa vitalu hivyo saba vya gesi, hakuna kipengere kinachomwezesha mtanzania kumiliki gesi hiyo.

Akizungumzia sera za uwekezaji kwa ujumla, Dk. Mengi alisema taasisi hiyo inaitaka Serikali kuingiza kwenye Katiba mpya inayokuja kipengere kinachowapa haki watanzania kuwa na ubia na wawekezaji wa nje badala ya kuwaachia wageni hao kumiliki rasilimali za hapa nchini kwa asilimia 100.

Alisema hali hiyo itawawezesha watanzania kuwa na hali ya kumiliki na kulinda rasilimali zao ambazo kwa sasa zinawanufaisha zaidi wageni kuliko watanzania wenyewe.

“Sisi tunaitaka Serikali ihakikishe kuwa shughuli yoyote ya uwekezaji wa kiuchimi, iwe na mtanzania ndani yake na watanzania hawa, wasishindwanishwe na wawekezaji wakubwa wan je,” alisema Dk. Mengi.

Naye Makamu mwenyekiti Salum Shamte, alisema kuwa Serikali inapaswa kuhakikisha sheria ya manunuzi za umma inawanufaisha zaidi watanzania kuliko wawekezaji.

Alisema hivi sasa kiasi kikubwa cha fedha za Bajeti ya kila mwaka, zinatumika katika kufanya manunuzi ya bidhaa na huduma na kazi hiyo imekuwa ikifanywa na wawekezaji badala ya kuwawezesha watanzania.

Akifafanua kuhusu hoja hiyo, Dk. Mengi alisema kuwa asilimia 80 ya Bajeti ya mwaka huu wa fedha, itatumika kwa ajili ya manunuzi ya umma hivyo ni vyema kazi hiyo ikafanywa na watanzania.

“Ukiangalia bajeti ya mwaka huu, karibu asilimia 80, sawa na sh trilioni 14 zitatumika kwa ajili ya manunuzi ya bidhaa na huduma za umma. Fedha hizi zikiingia kwa watanzania, zitachangia sana kukuza uchumi wa taifa,” alisema Dk. Mengi.

No comments:

Post a Comment