TANGAZO


Tuesday, August 27, 2013

Serikali kuchimba visima 300 nchini

 Ofisa Masoko wa Wakala wa Uchimbaji Visima na Mabwawa, Nungu Egwaga akiongea na waandishi wa habari juu ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya uchimbaji visima tangu kuanzishwa kwake mwaka 1997 chini ya Wizara ya Maji, wakati wa mkutano uliofanyika, ukumbi wa Idara ya Habari, Maelezo leo, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Ofisa Habari wa Idara ya Habari, Maelezo, Frank Mvungi. (Picha zote na Georgina Misama-Maelezo)

Na Eliphace Marwa - MAELEZO
SERIKALI kupitia Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA)iko katika mpango wa kuchimba visima virefu 300 vya maji katika mwaka wa fedha wa 2013⁄2014 katika maeneo mbalimbali nchini ili kupambana na tatizo la maji nchini.

Akizungumza na waandishi wa habari leo, katika ukumbi wa Idara ya Habari – Maelezo, jijini Dar es Salaam, Ofisa Masoko wa Wakala hiyo, Nungu Egwagwa amesema kuwa katika mwaka wa fedha wa 2013⁄2014, Wakala imejipanga kuwafikia wananchi mahali popote walipo na kuwapatia huduma sahihi  na kufanya kazi kwa kasi zaidi ili kukabiliana na soko la ushindani.

Wakala inajitahidi kutoa elimu kwa wananchi juu ya viwango vinavyotakiwa wakati wa uchimbaji visima ili kuweza kupambana na ushindani ulioko sasa ambapo wachimbaji binafsi walio wengi kutozingatia viwango vya ubora wakati wa uchimbaji hivyo kufanya gharama zao kuonekana nafuu ukilinganisha na za Wakala, alisema Nungu.

Aidha wakala imebainisha changamoto mbalimbali wanazokutana nazo hivi sasa ikiwemo tatizo la mabadiliko ya tabia nchi hivyo kuongezeka kwa gharama za uchimbaji kutokana na maji kupatikana katika umbali mrefu.

Pia Wakala imebainisha kuwa uchakavu wa mitambo wanayotumia imechangia kuongezeka kwa gharama za uendeshaji ila katika mwaka wa fedha wa 2013⁄2014 Wakala imejipanga kutoa huduma bora zaidi kwa kuwatumia wataalamu wao na vifaa vya kisasa zaidi ili kuongeza ufanisi katika uchimbaji visima.

Wakala wa Uchimbaji Visima na Ujenzi wa Mabwawa (DDCA) ulianzishwa mwaka 1997 ambapo toka Januari 1997 mpaka Juni mwaka huu wamechimba jumla ya visima 6929 na visima 5899 ambayo ni sawa na asilimia 85 ya mafanikio.

No comments:

Post a Comment