Katibu Mtendaji toka Mpango wa Afrika Kujitathmini Kiutawala Bora (APRM), Rehema Twalib akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mpango wa Serikali kuanza utekelezaji wa ripoti ya APRM, kwenye mkutano uliofanyika leo, ukumbi wa Idara ya Habari, Dar es Salaam. Kulia ni Ofisa Habari na Mawasiliano wa APRM Hassan Abbas. (Picha zote na Eliphace Marwa-MAELEZO)
Ndugu wanahabari,
Mabibi na Mabwana;
Tumewaita leo kuwapa
mrejesho ninyi kama wadau wa APRM lakini pia muwafikishie wananchi kwa ujumla
taarifa hii muhimu kuhusu hatua zilizofikiwa na Serikali ya Tanzania katika kutekeleza
majukumu yake kwa mujibu wa Mkataba wa Umoja wa Afrika wa Kujitathmini
Kiutawala Bora chini ya APRM.
Kama mnavyofahamu Tanzania
ni miongoni mwa nchi 33 sasa kati ya 54 za Umoja wa Afrika zilizosaini Mkataba
wa kutekeleza mpango huu wa APRM unaolenga kutathmini hali ya utawala bora kwa
kuwashirikisha wananchi kuzishauri Serikali zao ili kupata maendeleo endelevu
nay a pamoja.
Tanzania imekamilisha
zoezi hili la kwanza na la aina yake kwa nchi yetu na tayari Mh. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Jakaya Mrisho Kikwete aliiwasilisha Ripoti ya Tanzania
na kujadiliwa mbele ya viongozi wenzake wa Umoja wa Afrika Januari 26 mwaka huu
jijini Addis Ababa, Ethiopia.
Katika wasilisho hilo, Tanzania
ilipongezwa kwa hatua kadhaa ilizofikia katika kuimarisha utawala bora na vile
vile Serikali ilipewa muda wa kufanyiakazi maeneo yenye changamoto.
Kwa mujibu wa Mkataba wa
APRM sasa nchi yetu, inatakiwa kuanza kutekeleza Mpangokazi wa Kitaifa wa miaka
minne (NPoA) unaolenga kufanyiakazi maeneo anuai yaliyobainishwa kuwa na
changamoto ambayo kimsingi ni maoni ya wananchi.Taarifa za utekelezaji
zitatolewa kila mwaka. Tathmini ya APRM hurudiwa kila baada ya miaka minne ya
utekelezaji wa NPoA.
KALENDA
YA UTEKELEZAJI
Tunapenda kuwaarifu
rasmi kuwa pamoja na kwamba Ripoti hii itazinduliwa rasmi Oktoba mwaka huu,
tayari Serikali ya Tanzania imeonesha dhamira ya dhati kwa kuanza utekelezaji
wa maoni ya wananchi kama ifuatavyo:-
1. Baadhi ya
masuala yaliyoainishwa na yanayohusu Katiba yaliwasilishwa kwenye Tume ya
Mabadiliko ya Katiba na mengi yameingizwa kwenye rasimu iliyotolewa hivi
karibuni;
2. Baadhi ya
Masuala yameingizwa kwenye mfumo wa Mpango wa Mwaka na Bajeti iliyopitishwa
hivi karibuni ya 2013/14;
3. Baada ya
uzinduzi mwezi Oktoba, masuala mengine yote yaliyosalia yataingizwa katika Mipango
na Bajeti za miaka ijayo za wizara na taasisi nyingine husika.
4. APRM Tanzania
itaendelea kusimamia utekelezaji na kuripoti kwa umma. Tathmini ya utawala bora
itarudiwa tena kila baada ya miaka minne.
Asanteni kwa kutusikiliza na kuipokea taarifa hii na kwa
mchango wenu jadidi katika kutangaza shughuli za APRM Tanzania.
Imetolewa
na:
HASSAN
ABBAS,
AFISA
HABARI NA MAWASILIANO,
APRM
TANZANIA.
0713 584467
_________________________________________________________________________
KUHUSU APRM Tanzania:
Ni taasisi
iliyoundwa na Serikali ya Tanzania kusimamia na kuratibu utekeleza wa majukumu
ya nchi kwa mujibu wa Mkataba wa Afrika kuhusu APRM. Bunge liliridhia kuanza
APRM Tanzania Februari mosi, 2005, 2007 Mhe. Rais akateua Bodi yenye wajumbe 20
kutoka sekta za umma, binafsi na wawakilishi wa Bunge inayoongozwa na Prof.
Hasa Mlawa. Shughuli za kila siku zinaratibiwa na Sekretarieti inayoongozwa na
Katibu Mtendaji, Bi. Rehema Twalib. Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Kimataifa ndiyo inayoratibu shughuli za APRM hapa nchini.
RIPOTI ya Tanzania:
Mambo mazuri: Muungano,
amani, utulivu, lugha ya Kiswahili, kurithishana madaraka kwa amani, vita
inayoimarika dhidi ya rushwa, Tanzania kukubali kushtakiwa Mahakama ya Haki za
Binadamu ya Afrika. Changamoto: Kero za Muungano, vita dhidi ya rushwa,
uchumi kukua lakini bado watu wengi ni masikini, mauaji ya albino, ubora wa
huduma za afya, elimu n.k.
No comments:
Post a Comment