Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini kutoka Wizara ya Habari Vijana Utamaduni na Michezo, Godlease Malisa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu utekelezaji wa azma ya Serikali kusaidia vijana. Jumla ya sh. bilioni 6.1 zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2013. Mkutano huo, umefanyika ukumbi wa Idara ya Habari jijini Dar es salaam leo. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa.
Mkurugenzi wa Idara ya Vijana kutoka Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Profesa Elisante Ole Gabriel, akibadilishana mawazo na waandishi wa habari katika mkutano huo jijini leo. (Picha zote na Hassan Silayo-Maelezo)
NDUGU waandishi wa Habari tunatambua kwamba hivi
karibuni Serikali ilipitisha bajeti yake kwa ajili ya maendeleo katika sekta
mbalimbali ikiwemo Vijana ambayo imekuwa na changamoto nyingi ikiwemo uhaba wa
ajira,hata hivyo Serikali imekuwa ikifanya jitihada za makusudi ili kuhakikisha
inamkwamua kutoka katika janga la umasikini.
Katika kutekeleza azma ya kusaidia Vijana, jumla ya shilingi Bilioni
6.1 zimetengwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2013/2013 ikiwa ni kwa ajili ya kusaidia
mfuko wa Maendeleo ya Vijana, ambapo Vijana watapatiwa mikopo yenye unafuu katika
riba na upatikanaji wake. Natoa
wito kwa vijana kuchangamkia fursa hii ambayo haimuhitaji mkopaji kuwa na dhamana isiyo hamishika bali kuwa
na uaminifu wa kurejesha mkopo huo na kujiunga kwenye SACCOS.
Ndugu Waandishi wa Habari, kwa kutambua umuhimu wa
vijana katika maendeleo ya taifa letu, Serikali iliamua kuanzisha Mfuko wa
Maendeleo ya Vijana mnamo mwaka 1993/94, chini ya Sheria Na. 21 ya mwaka 1961
kifungu cha 17(1), ukiwa na lengo
la kuwasaidia Vijana kupata mikopo yenye masharti nafuu na kuwajengea uwezo
kiuchumi ili waweze kuanzisha au
kuimarisha miradi yao kwa lengo la kuwawezesha kujitegemea na kukuza uchumi wa
nchi.
Takwimu zinaonyesha kuwa kuna jumla ya Vijana milioni
16,195,370 ambapo takribani vijana 1,200,000 humaliza elimu ya vyuo mbalimbali
kila mwaka na kati yao ni vijana 200,000 huajiriwa kwa mwaka. Ikumbukwe kuwa
Vijana wanachukua asilimi 68 ya nguvu kazi ya Taifa lakini takwimu zinaonyesha
kuwa upungufu wa ajira kwa Vijana ni asilimia 14.4.
Ndugu Waandishi wa Habari Wizara ya Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo ambayo ndiyo yenye dhamana ya kuendesha mfuko huu tayari imeshapeleke
muongozo mpya wa namna bora ya vijana kunufaika na mikopo katika Halmashauri
zote nchini. Hivyo Vijana mnashauriwa kujiunga katika vikundi na kufanya
mawasiliano na Maafisa Vijana katika Halmashauri zenu ili kujua taratibu za
kupata mikopo hiyo.
Ndugu Waandishi napenda kutumia fursa hii kuwapongeza
kwa kazi nzuri mnayoifanya ya kuhabarisha umma hasa katika matukio makubwa
yaliyotokea hivi karibuni nchini kwetu. Mmefanya kazi kubwa sana ya kutangaza
mabadiliko ya ratiba ya Bunge la Bajeti kutoka Juni – Agosti na kuwa Aprili
hadi Juni kila mwaka. Kadhalika mlitangaza ziara ya Rais Obama, ziara ya Rais
wa Sri Lanka, Mkutano wa Smart partnership na Maonyesho ya Sabasaba.
Ndugu waandishi wa Habari, Serikali imepokea kwa
msikitiko kifo cha mwandishi mkongwe marehemu David Majebele aliyefariki jana
alfajiri na msiba upo nyumbani kwake Sinza Plot Na. 262 Block E, Mtaa wa Lion
Hotel, ambapo mazishi yanatarajiwa kufanyika siku ya Alhamisi katika makaburi
ya Kinondoni. Wizara inatoa pole na salam za rambirambi kwa ndugu, jamaa na
familia ya Marehemu, Mungu ailaze roho ya marehemu mahali pema peponi AMINA.
Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo
ilianzishwa mwaka 2006. Wizara hii inaundwa na Idara nne za kisekta ambazo ni
Idara ya Habari, Idara ya Maendeleo ya Vijana, Idara ya Maendeleo ya Utamaduni
na Idara ya Maendeleo ya Michezo.
Imetolewa na
Bw. Godlease Malisa
Mkuu wa Kitengo Cha Mawasiliano Serikalini
15 Julai, 2013
No comments:
Post a Comment