Ofisa Habari Mkuu wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala
Bora, Germanus Kyafula (kushoto), akieleza kwa vyombo vya habari nchini kuhusu
mfumo mpya wa kupokea malalamiko kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani katika
mkutano uliofanyika katika ukumbi wa Idara ya Habari leo, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa, Wilfred Warioba.
Baadhi
ya waandishi wa habari wakifuatilia kwa makini taarifa inayotolewa na Maofisa
wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika mkutano uliofanyika ukumbi
wa Idara ya Habari Maelezo leo, jijini Dar es Salaam.
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa, Wilfred
Warioba (katikati), akifafanua jambo kwa waandishi wa habari kuhusu mfumo mpya wa
kupokea malalamiko kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani, Dar es Salaam leo. Kushoto ni Ofisa
Habari Mkuu wa Tume hiyo Germanus Kyafula na kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa
Idara ya Habari.
Mkurugenzi wa Idara ya Haki za Binadamu, Francis Nzuki
akiwaonesha waandishi wa habari kijitabu chenye sheria namba 7 ya mwaka 2001, iliyounda Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora katika mkutano uliofanyika
ukumbi wa Idara ya Habari Maelezo leo, jijini Dar es Salaam. Kulia ni Kaimu Mkurugenzi Elimu
kwa Umma na Mafunzo Alexander Hassan. (Picha zote na Frank Mvungi-Maelezo)
ILI kuboresha utoaji huduma kwa umma
hivi karibuni Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) imeanzisha utaratibu
wa kupokea malalamiko na taarifa kuhusu uvunjwaji wa haki za binadamu na
ukiukwaji wa misingi ya utawala bora kwa njia ya ujumbe wa simu ya kiganjani.
Utaratibu huu mpya unatarajia kupunguza
usumbufu na gharama kwa walalamikaji, hususan watokao pembezoni mwa nchi katika
kuwasilisha malalamiko yao ofisi za Tume na kupata mrejesho. Itakumbukwa kuwa
hapo awali baadhi ya wananchi walilazimika kuacha shughuli zao za kiuchumi na
kusafiri hadi zilipo ofisi za Tume ili kupata huduma.
Vilevile utaratibu huu utaharakisha mawasiliano
kati ya Tume na walalamikaji kwa upande mmoja na kati ya Tume na walalamikiwa, ukilinganisha
na njia iliyokuwa ikitumika awali ya barua ya posta ambayo ilikuwa ikichukua
muda mrefu na kukabiliwa na changamoto nyingi, ikiwemo kupotea kwa barua na wananchi
wengi kutokuwa na anuani za posta za uhakika.
Kwa utaratibu huu mpya mtu anaweza
kufungua malalamiko Tume pale ambapo ataona haki zake za msingi zimevunjwa au
misingi ya utawala bora imekiukwa kwa kuandika ujumbe mfupi wa simu ya
kiganjani kwenda namba 0754 460 259, naye
atapokea majibu ndani ya muda mfupi.
Utaratibu huu mpya siyo tu unampa
uhakika mlalamikaji wa lalamiko lake kufika Tume, bali pia unamwezesha kupata
ushauri wa kisheria juu ya lalamiko lake ndani ya muda mfupi.
Aidha, utaratibu huu utaisaidia Tume
kupata vidokezo (yaani ‘tips’) kuhusu matukio ya uvunjwaji wa haki za binadamu
na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora yanayotokea maeneo mbalimbali ya nchi
na hivyo kufanya ufuatiliaji kwa wakati.
Utaratibu huu mpya unatarajia kuongeza
idadi ya malalamiko yanayowasilishwa Tume kutoka wastani wa malalamiko 80 hivi
sasa hadi 200 kwa Mwezi. Tume imejipanga kikamilifu kuyashughulikia malalamiko yote
ndani ya muda mfupi. Hii inatokana na ukweli kwamba hivi sasa Tume inatumia
mfumo wa kielektroniki ujulikanao kwa lugha ya kigeni kama “Case Management
System,” katika
kushughulikia malalamiko yanayopokelewa.
Tunaomba vyombo vya habari vitusaidie
katika kuhakikisha utaratibu huu mpya unafahamika vizuri kwa umma na
kuwahamasisha wananchi wautumie kutoa taarifa mbalimbali zinazohusu masuala ya
uvunjifu wa haki za binadamu na ukiukwaji wa misingi ya utawala bora.
Jinsi ya kuwasilisha lalamiko kwa
simu ya kiganjani:
· Tuma
lalamiko lako ukianzia na neno 'REPORT' kwenda Na. 0754
460 259. Mfano: REPORT shule ya Msingi Kwetumbali, DSM
tunachapwa viboko zaidi ya kumi.
· Utapokea
ujumbe usemao lalamiko lako limepokelewa Tume, na utaelekezwa kama unayo
maelezo zaidi yatume kupitia barua pepe: chragg@chragg.go.tz
au simu Na. 22 2135747/8.
· Maafisa wa
Tume wanaweza kukupigia simu ili kupata maelezo zaidi kabla ya kuanza
kushughulikia lalamiko lako.
· Lalamiko
lako litakapoanza kushughulikiwa, utapata ujumbe wa simu kukujulisha Namba ambayo utaitumia kufuatilia lalamiko
lako. Namba hii itatumwa kwako kupitia namba ya simu uliyotumia kuwasilisha
lalamiko lako.
· Utaweza
kujua hatua ambazo maafisa wa Tume wamefikia kwa kutuma ujumbe wa simu pamoja
na Namba ambayo utakuwa umepewa baada ya lalamiko lako
kufunguliwa jalada.
Jinsi ya kufuatilia lalamiko lako:
· Tuma ujumbe
wako ukianza na neno 'STATUS' kwenda Na.0754 460 259. Mfano: STATUS 13024.
Utaratibu huu wa upokeaji wa taarifa na
malalamiko kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu ya kiganjani umefadhiliwa na Programu
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano kwa nchi zinazoendelea (SPIDER) ya
nchini Sweeden (au Swedish Program for ICT in Developing Regions).
Tunaomba ieleweke kuwa utaratibu huu
mpya haubadilishi taratibu zilizokuwa zikitumika awali za kuwasilisha
malalamiko Tume. Sambamba na uwasilishaji wa malalamiko kwa ujumbe mfupi wa
simu ya kiganjani, Tume itaendelea kupokea malalamiko ya wananchi kwa mlalamikaji
kuja mwenyewe kwenye ofisi zetu na kufungua lalamiko lake, na kwa kuandika na
kutuma barua kwa njia ya posta, barua pepe au nukushi (faksi.
THBUB ni
taasisi huru ya Serikali iliyoanzishwa kama taasisi ya kitaifa iliyo kitovu cha
kukuza na kulinda haki za binadamu na wajibu na misingi ya utawala bora. Ilianzishwa kwa mujibu wa Katiba ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya 1977 chini ya Ibara ya 129 (1) na Sheria Na.
7 ya Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora ya Mwaka 2001 na ilianza kazi rasmi
tarehe 1 Julai, 2001.
Tume ina
majukumu mengi, baadhi ya majukumu hayo ni: Kupokea na kuchunguza malalamiko yanayohusu uvunjwaji wa
haki za binadamu na ukiukwaji wa
misingi ya utawala bora na kutoa mapendekezo, kufanya utafiti na kutoa elimu
kwa umma kuhusu masuala ya haki za binadamu na utawala bora, na kutoa
mapendekezo kwa ajili ya kuboresha sheria na kanuni zilizopo au miswada ya
sheria na kanuni au taratibu za kiutawala ili kuhakikisha kuwa haki za binadamu
na utawala bora vinazingatiwa.
Tume inafanya kazi Tanzania Bara na
Visiwani Zanzibar. Kwa hivi sasa ina ofisi nne (4) zilizoko Dar es Salaam,
Zanzibar, Lindi na Mwanza.
Kwa taarifa zaidi, tafadhali wasiliana na:
Afisa Uchunguzi Mkuu, Bwana Germanus Joseph
Simu: +255 22 2135222/ 754 768 346.
Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa,
Bwana Wilfred Warioba
Simu: +255 22 2135747/8; 714 818 177.
No comments:
Post a Comment