Kiongozi wa kanisa katoliki, Baba mtakatifu Francis, amekosoa vikali mipango ya kutaka kuhalalisha madawa ya kulevya Amerika ya Kusini.
Aliyasema hayo wakati alipotembelea klikini mpya ya kuwatibu waraibu wa dawa za kulevya mjini Rio de Janeiro.
Uruguay inakaribia kuidhinisha uuzaji wa Marijuana au Bhangi huku baadhi ya nchi katika kanda hiyo zikitafakari hatua sawa na hiyo.Vyanzo vya matumizi mabaya ya madawa ya kulevya lazima vitatuliwe, alisema papa katika siku ya tatu ya ziara yake nchini Brazil.
Awali Papa Francis mzaliwa wa Argentina alishiriki misa yake ya kwanza katika ziara yake katika kanisa la Our Lady of Aparecida.
Aliwaonya maelfu ya waumini dhidi ya kukumbatia sana pesa, mamlaka na raha za dunia.
Baada ya ziara yake eneo la Aparecida, nchini Brazil Papa alirejea mjini Rio de Janeiro.
Wakati wa ufunguzi wa kliniki ya kutoa matibabu kwa waraibu wa madawa ya kulevya, aliwakumbatia waliokuwa watumizi wa dawa hizo, huku akiwasikiliza wakisimulia yaliyowakumba wakati wa uraibu wao.
"ni muhimu kukabiliana na vyanzo vya matumizi mabaya ya madawa ya kulevya, kuhakikisha haki na kuwafunza vijana kuhusu umuhimu maadili mazuri katika jamii, kuwasaidia wanaokabiliwa na matatizo na kuwapa matumaini,'' alisema Papa.
Papa Francis pia alionya dhidi ya mipango ya kuhalalisha madawa ya kulevya katika kanda ya Amerika ya Kusini huku akiwalaani walanguzi wa madawa hayo.
No comments:
Post a Comment