Mkuu wa Jeshi la Misri amewataka wananchi kujitokeza kuandamana siku ya Ijumaa dhidi ya kile anachokiita ugaidi.
Abdel Fattah al-Sisi amesema anawataka watu kuunga mkono jeshi na kulikabidhi jukumu la kukabiliana na ghasia pamoja na ugaidi.
Wafuasi wa Mohammed Morsi aliyeondolewa mamlakani na jeshi, wamekuwa wakiandamana dhidi ya jeshi ambalo lilimuondoa mamlakani tarehe 3 mwezi Julai.
Lakini Generali Sisi alisema wito wake sio wa ghasia bali anataka kuwepo maridhiano ya kitaifa.
"Ninawasihi watu kuandamana Ijumaa hii kuthibitisha kuwa wananipa mamlaka mimi na jeshi langu kukabiliana na ghasia pamoja na ugaidi,'' alisema Generali Sisi ambaye pia ni waziri wa ulinzi katika serikali mpya.
Alikuwa anazungumza katika sherehe za wanafunzi kufuzu chuo kikuu.
Alipinga madai ya migawanyiko jeshini. ''Ninaapa kwa Mungu kuwa jeshi lina msimamo mmoja,'' alisema Sisi.
Akigusia hoja ya jeshi kumwondoa mamlakani Morsi, alisema kuwa : '' nilimshauri Morsi kuwa rais wa wamisri wote.''
Na akikumbuka uchaguzi wa urais wa mwaka 2012, wakati Morsi alipochaguliwa, alisema kuwa aliwashauri wanachama wa chama cha Brotherhood kutogombea uchaguzi huo, lakini wakampuuza.
No comments:
Post a Comment