Wahudumu wawili wa shirika la madaktari wasio na mipaka - MSF wameachiliwa huru na wapiganaji wa Al Shabaab.Wahudumu hao walitekwa nyara mwaka 2011 katika kambi ya wakimbizi wa Kisomali kaskazini mwa Kenya.
Shirika la Medecins Sans Frontieres limesema kuwa wafanyakazi hao wawili wote wako salama na wenye afya na wanatazamia sana kujiunga na jamaa zao.
Montserrat Serra na Blanca Thiebaut walitekwa nyara kutoka kambi ya wakimbizi ya Dadaab mwezi Oktoba mwaka 2011.
Kufuatia kutekwa nyara kwao pamoja na mateka wengine wa Kenya, nchi hiyo ililazimika kutuma vikosi nchini Somalia kupambana na wanamgambo wa al-shabaab.
Katika taarifa ya shirika hilo, ni afueni kubwa kwa shirika hilo kuweza kuthibitisha kuachiliwa kwa wanawake hao.
Wanawake hao walitekwa nyara tarehe 13 mwezi Oktoba mwaka 2011 na watu waliokuwa wamejihami kwa bunduki na ambao walifyatulia risasi gari la wanawake hao huku wakimjeruhi dereva aliyekuwa raia wa Kenya.
Kambi hiyo ya Dadaab ambayo ndiyo kambi kubwa zaidi duniani ya wakimbizi, inawahifadhi wakimbizi laki tano ambao wametoroka vita vya miaka mingi na njaa nchini Somalia ambayo inapakana na Somalia.
Bi Serra, ambaye ni mwalimu kutoka , Girona nchini uhispania, alikuwa mfanyakazi nchini Kenya kwa miezi miwili alipotekwa nyara. Alikuwa amefanya kazi na mashirika mengione ya misaada Amerika ya kusini na Yemen.
Mwanamke mwingine Thiebaut ambaye ni mhandisi wa kilimo, kutoka Madrid alikuwa ndio amekamilisha tu masomo yake ya digri katika chuo cha mafunzo ya uchumi mjini London alipotekwa nyara.
Kenya ililituhumu kundi la al-Shabab kwa kuhusika na utekaji nyara huo pamoja na matukio mengine sawa na hilo mwaka 2011 na hivyo kutishia usalama wa nchi.
Ilituma vikosi vyake nchini Somalia kuweza kupambana nao na kisha kuteka maeneo mengi ya nchi hiyo kutoka kwa kundi la al-Shabab.
Wanajeshi wake nchini Somalia sasa wamejiunga na kikosi cha jeshi katika muungano wa Afrika ambao wanasaidia serikali dhaifu ya Somalia.
No comments:
Post a Comment