TANGAZO


Friday, June 28, 2013

Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba alitaka JWTZ kuwaachia huru viongozi wao wanaowashikilia, Pia Serikali kuuondoa utawala wa Kijeshi mkoani Mtwara


Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni Dar es Salaam leo, kuhusu kudai kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wao na pia kubakwa kwa binti mmoja mkoani Mtwara na alidai kuwa ni Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), mkoani humo. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Julias Mtatiro. (Picha zote na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)
Baadhi ya waandishi wa habari, wakimsikiliza Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni Dar es Salaam leo, kuhusu kile alichodai kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wao na pia kubakwa kwa binti mmoja mkoani Mtwara na aliosema kuwa ni Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), mkoani humo.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akizungumza na waandishi wa habari, Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni Dar es Salaam leo, kuhusu kile alichodai kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wao na pia kubakwa kwa binti mmoja mkoani Mtwara na aliosema kuwa ni Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), mkoani humo. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Julias Mtatiro.
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, akifafanua jambo kwa waandishi wa habari, Makao Makuu ya chama hicho, Buguruni Dar es Salaam leo, wakati alipokuwa akizungumza nao, kuhusu kile alichodai kukamatwa kwa baadhi ya viongozi wao na pia kubakwa kwa binti mmoja mkoani Mtwara na aliosema kuwa ni Askari wa Jeshi la Wananchi (JWTZ), mkoani humo. Kushoto ni Naibu Katibu Mkuu Bara, Julias Mtatiro na kulia ni Mwenyekiti wa CUF, Wilaya ya Ilala, Said Ricco.

Na Hamisi Magendela 
MWENYEKITI wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba amelitaka Jeshi la Wananchi Tanzania  (JWTZ) kuwaachia huru viongozi watatu wa chama hicho na dereva mmoja wanaodai kushikiliwa na jeshi hilo katika kambi ya Liendeli, mkoani Mtwara.

Akizungumza Dar es Salaam leo, Profesa Lipumba, alisema kuwa viongozi hao wanadaiwa kutekwa, kupigwa na wanajeshi wanaolinda usalama mkoani Mtwara wakati wakitokea Msimbatu walikokwenda kwa ajili ya kupata ufafanuzi wa binti anayedaiwa kubakwa na askari hao.

Alifafanua kuwa wakiwa njiani katika eneo la Mangamba walikuta lori la Jeshi likiwa limekata barabara na nyuma yao, wakifuatwa na Landlover ya JWTZ na kulisimamisha gari hilo na kuwashusha na kisha kuwapa kipigo na baadaye kuwaingiza kwenye lori na kuondoka nao katika kambi ya Liendeli.

Lipumba aliwataja wanaodaiwa kutekwa kuwa ni Naibu Mkurugenzi wa Mipango, Uchaguzi na Siasa, Shaweji Mketo, Said Kulega na Mjumbe wa Kamati ya Mkoa wa Mtwara ambaye jina lake bado halijapatikana pamoja na dereva wa gari lao, Kashinde Kalungwana.

"Nilipata taarifa za kutekwa viongozi saa 3, usiku baada ya kutaarifiwa na Naibu Katibu Mkuu Bara, Julius Mtatilo na nilipompigia simu Mketo kwa kutaka kujua zaidi sababu za wao kutekwa ndipo simu ikapokelewa na mtu mwingine na kunijibu vibaya na akakata simu," alisema.

Lipumba alifafanua kuwa licha ya Mketo kuwa na kutaka kulishughulikia suala na binti aliyebakwa lakini kikubwa kilichompeleka ni kufuatilia kesi ya baadhi ya viongozi wanaoshikiliwa huko na walitakiwa kupandishwa Mahakamani juzi na kesi yao kuahirishwa.

Alisema wakati wakiwa katika jukumu hilo, ndipo walipopewa taarifa na wananchi wa huko kuwa kuna vitendo viovu vinavyodaiwa kufanywa na baadhi ya wanajeshi wanaolinda usalama mkoani Mtwara likiwemo la kubakwa kwa binti na kusababishiwa majeraha makubwa.

Aliongeza kuwa baada ya binti huyo, kubakwa alitoa taarifa katika kituo cha Polisi Msimbati lakini hakuna hatua zozote zilizochukuliwa hali iliyofanya Mketo pamoja na viongozi wengine kufanya kikao cha ndani ili kupata taarifa kamili za tukio hilo na wakati wanarudi ndipo walipokamatwa.

Mwenyekiti huyo wa CUF, alihoji uhalali wa JWTZ kuwakamata viongozi akidai ni kinyume na sheria na taratibu za nchi, mwanajeshi kukamata raia wakati jukumu hilo liko chini ya Jeshi la Polisi.

Hata hivyo Lipumba aliitaka Serikali kuondoa utawala wa kijeshi uliopo mkoani Mtwara na kurudisha utawala wa kiraia kwani haiwezekani kujenga amani ya kweli huku wanajeshi wakiendelea kuikalia Mtwara.

Lipumba alitoa mwito kwa asasi za kiraia kufutilia vitendo viovu vinavyodaiwa kufanywa na wanajeshi mkoani Mtwara pamoja na kulishughulikia suala la binti aliyebakwa.

Pia alilitaka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kualichia gari lao aina ya Nisan Patrol lenye namba T 866 BGW, nyeupe wanalolishikiliahadi sasa.

No comments:

Post a Comment