Mlipuko mkubwa umetikisa katikati ya mji mkuu wa Syria, Damascus, vyombo vya habari vya serikali vimetangaza.
Kwa mujibu wa Taasisi Inayofuatilia Haki za Binadamu Nchini Syria (SOHR) yenye makao yake Uingereza, watu watano wameuawa katika mlipuko huo uliotokea katika wilaya ya kati ya Marjeh.
Haijafahamika mlipuko huo umesababishwa na nini. Milio ya risasi ilisikika katika eneo hilo mara baada ya mlipuko kutokea.
Jumatatu, wiki hii Waziri Mkuu wa Syria, Wael Al – Halqi, alinusurika kuuawa baada ya mlipuko kulenga msafara wake wa magari.
Taarifa zinasema, mlipuko huo wa sasa umetokea karibu na jengo la wizara ya mambo ya ndani.
Taasisi hiyo inafuatilia ukiukwaji wa haki za binadamu kutoka pande zote zinazohusika kwenye mgogoro kupitia mitandao mbalimbali ya mawasiliano kote nchini Syria.
Inakadiriwa kuwa mwezi Machi mwaka huu ulishuhudia umwagaji damu mkubwa ambapo zaidi ya watu 6,000 waliuawa, theluthi yao wakiwa ni raia.
Zaidi ya watu 70,000 wameuawa tangu kuzuka kwa mapigano kati ya vikosi vya serikali ya Syria na waasi Machi 2011.
No comments:
Post a Comment