![]() |
Baadhi ya Makadhi wa walioalikwa katika Maadhimisho ya Siku ya Sheria, Uwanja wa Bustani ya Victoria Garden, wakifuatilia kwa makini harakati za maadhimisho hayo, zilivyokuwa zikiendelea na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali.
|
![]() |
Baadhi ya wanafunzi waliohudhuria katika kilele cha maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, sherehe zilizofanyika leo, Viwanja vya bustani ya Victoria, Mjini Zanzibar, wakifuatilia matukio mbalimbali yaliyokuwa yakitendeka. Mgeni rasmi katika maadhimisho hayo, alikuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein.
|
![]() |
Mkurugenzi wa Mashtaka Zanzibar, Ibrahim
Mzee, alipokuwa akizungumza wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, zilizofanyika leo, Viwanja vya Victoria Garden, Mjini Zanzibar, ambapo ujumbe wa mwaka huu unasema
"Kutokomeza Unyanyasaji Kijinsia".
|
![]() |
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akionesha jarida la Mahakama baada ya kulizindua, wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, zilizofanyika leo, Viwanja vya Victoria Garden,
Mjini Zanzibar. Kushoto ni Kaimu Waziri wa Katiba na Sheria, ambaye pia ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui na kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu.
|
![]() |
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na wananchi pamoja na Wanasheria, wakati wa
sherehe za maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, zilizofanyika leo, Viwanja vya Victoria Garden, Mjini
Zanzibar. Kushoto ni Kaimu Waziri wa Katiba na Sheria, ambaye pia ni Waziri wa Biashara, Viwanda na Masoko, Nassor Ahmed Mazrui na kulia ni Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu.
|
Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar.
7.2.2013
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuviripoti vitendo vya unyanyasaji wa kijinsia katika vyombo vinavyohusika ili sheria iweze kuchukua mkondo wake.
Hayo ameyasema leo, Rais Dk. Shein, wakati akihutubia katika maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar, huko katika viwanja vya Victoria Garden, mjini Zanzibar.
Katika maelezo yake, Dk. Shein alisema kuwa kuna vitendo ambavyo vimekuwa vikitokea kila siku katika jamii lakini kwa bahati mbaya kutokana na suala la utamaduni na mila ziliopo haviripotiwi kwenye vyombo vinavyohusika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua.
Alisema kuwa kuna vitendo vya unyanyasaji wa majumbani vinavyotokea kwa watu wa mila, rangi, dini na makabila yote na kusisitiza lazima kuwepo na ujasiri wa kuviripoti vitendo vya aina hiyo ili sheria iweze kuchukuliwa.
Dk. Shein alieleza kuwa vipo vitendo wanavyofanyiwa baadhi ya akina mama vikiwemo vipigo vya kuidhuru miili yao na pia, kutelekezwa pamoja na watoto wao, vitendo ambavyo hufanywa na waume wasiojali thamani na haki za akina mama ingawa ni kinyume na mafundisho ya dini zote.
Aidha, Dk. Shein alisem akuwa inasikitisha kusikia kuwa baadhi ya matukio yanayoripotiwa yanawajumuisha wafanyakazi wa ndani na watoto wa kambo ambao wananyanyaswa na kupigwa, kufanywa vitendo viovu, kunyimwa mishahara na udhalilishaji wa aina nyengine.
Alisisitiza kuwa hayo si mambo mazuri na hayatakiwi yaendelee kutokea katika jamii hii ya Kizanzibari ambayo watu wake ni waumini wa dini iliyonyooka.
Alieleza kuwa tafiti zilizofanywa na taasisi mbali mbali za Kimataifa zimethibitisha kuwa tatizo la unyanyasaji kijinsia n I tatizo lililoenea duniani kote ambapo waathirika wakubwa wa vitendo vya unyanyasaji ni wanawake na watoto.
Hivyo, Zanzibar ikiwa ni sehemu ya dunia nayo inakabiliwa na tatizo hilo.
Dk. Shein alisema aliwataka wananchi kuwa na imani na taasisi zao na kuweza kujitokeza bila ya woga katika kutoa maelezo yatakayosaidia kupatikana kwa ithibati itakayosaidia kupata ukweli.
Alisema kuwa umefika wakati kwa vyombo vya sheria ikiwemo Mahakama, waendeshaji mashtaka, polisi na wananchi kwa ujumla kuwa pamoja na kujenga ushirikiano ulio imara zaidi kwa lengo la kuutokomeza unyanyasaji wa kijinsia.
Dk. Shein alieleza imani yake kubwa kuwa iwapo kutakuwa na dhamira ya kweli, jambo hilo litawezekana na kusisitiza kuwa ili mafanikio yaweze kupatikana ipo haja ya kuangalia sababu zilizopelekea kuwepo kwa tatizo hilo.
“Wito wangu ni kuwa tubadilike, tuache muhali na tufuate sheria”,alisisitiza Dk. Shein.
Aidha, Dk. Shein alikiri kuwa kauli mbiu ya mwaka huu “Kutokomeza unyanyasaji wa Kijinsia”, kuwa nayio ni muhimu sana na ni kauli mbiu nzito ambayo tokea alipokabidhiwa madaraka amekuwa akieleza dhamira na jitihada za Serikali anayoiongoza katika kupambana na kulitokomeza suala la unyanyasaji wa kijinsia.
Nae Jaji Mkuu wa Zanzibar, Mhe. Omar Othman Makungu alieleza juhudi zinazochukuliwa na Mahakama katika kuhakikisha haki inatendeka tena bila ya ubaguzi.
Mapema Rais wa Chama cha Wanasheria Zanzibar Awadh Ali Said alisema kuwa dhana ya unyanyasaji wa kijinsia ni dhana iliyo pana ikiwa inajumuisha matendo yote yanayolenga kumdhalilisha na kumdumisha mtu na utu wake na kusisitiza kuwa juhudi za kutokomeza zichukuliwe kutuatana na upana wake.
Alisema kuwa athari za matendo ya unyanyasaji wa kijinsia haziishii kwa matokeo yaliyo dhahiri ya kimwili na kiheshima tu bali pia, huambatana na athari za muda mrefu za kisaikolojia ambazo huwa ni jinamizi linalomuandama muathirika na hata familia yake.
Alisisitiza kuwa unyanyasaji wa kijinsia si uovu mpya katika jamii bali ni vitendo ambavyo ni vikongwe kama ilivyo jamii yenyewe.
Rais huyo wa Chama Cha Wanasheria Zanzibar alieleza kuwa mwaka 2010 kesi za unyanyasaji wa kijinsia 50 zilifunguliwa Mahkamani na kati ya hizo 32 zimetolewa maamuzi ambapo katika hizo ni kesi 2 tu ndizo washtakiwa wametiwa hatiani.
Sambamba na hayo, aliendelea kueleza mifano hiyo ambapo kwa mwaka 2011 kesi 77 zilifunguliwa. Kesi 34 zimetolewa uamuzi na katika hizo ni kesi moja tu ambayo mshtakiwa ametiwa hatiani.











No comments:
Post a Comment