Wapigapicha wa vyombo vya habari waliokuwa wakifanya kazi zao kwenye kikao cha Bunge wakijadiliana jambo, mjini Dodoma kabla ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kulifunga Bunge leo jioni.
HOTUBA YA MHESHIMIWA MIZENGO PINDA (MB), WAZIRI MKUU
WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA WAKATI WA KUTOA HOJA YA KUAHIRISHA MKUTANO
WA KUMI WA BUNGE LA MUUNGANO, DODOMA TAREHE 08 FEBRUARI, 2013
UTANGULIZI
1.
Mheshimiwa Spika, tumekuwepo hapa Bungeni, Dodoma kwa takriban siku 11 ambapo
leo tunahitimisha shughuli zilizopangwa katika Mkutano wa Kumi wa Bunge lako
Tukufu. Nitumie nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu mwenye wingi wa Rehema kwa
kutufikisha salama siku ya leo.
2.
Mheshimiwa Spika, awali ya yote naomba nitumie nafasi hii kutoa pole kwa
Ndugu, Jamaa na Marafiki waliopoteza Wapendwa wao katika ajali mbalimbali
zilizotokea hapa Nchini, ikiwemo ajali ya Jahazi la Sunrise iliyotokea Wangwi katika
Bahari ya Hindi na Ajali ya Lori kule Mbarali ambapo Watu wamepoteza maisha na
kupata majeraha. Aidha, tunawapa pole Majeruhi wote na Abiria waliopoteza mali
katika ajali hizo. Kwa kipekee kabisa napenda kutoa pole kwa Ndugu, Jamaa na
Marafiki wa Askofu Thomas Laiser wa KKKT, Dayosisi ya Kaskazini Kati - Arusha
ambaye amefariki jana Mchana na Askofu Mstaafu Amedeus Msarikie wa Kanisa
Katoliki, Jimbo la Moshi ambaye
amefariki Usiku wa kuamkia leo huko Nairobi alikokuwa anapata matibabu. Wote
tunawapa pole sana!
SHUGHULI
ZA BUNGE
a)
Maswali
3.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu jumla ya Maswali 116 ya Msingi na 286 ya nyongeza yalipatiwa
majibu. Vilevile, Maswali 6 yaliulizwa na kujibiwa kwa utaratibu wa Maswali ya
Papo kwa Papo kwa Waziri Mkuu.
b) Miswada
4.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, Miswada ifuatayo ilisomwa kwa mara ya
Kwanza:
i)
Muswada wa Sheria ya Vyama vya Ushirika wa Mwaka 2013 [The
Cooperative Societies Bill, 2013]; na
ii)
Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2013 [The
Written Laws Miscellaneous Amendments, Bill 2013].
5.
Mheshimiwa Spika, Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali wa Mwaka 2012 [The
Written Laws Miscellaneous Ammendments (No. 3) Act, 2012] ulisomwa kwa mara ya
Pili na kupitia ngazi zake zote;
c) Hoja
Binafsi za Wabunge
6.
Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu, pia Waheshimiwa Wabunge walipata fursa ya kuwasilisha Hoja
Binafsi kama ifuatavyo:
i)
Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Mwigulu Lameck Nchemba, Mbunge wa Iramba
Magharibi ya kuitaka Serikali iwasilishe Bungeni Muswada wa Sheria ya
Uanzishwaji wa Mfuko wa Elimu ya Juu (The Higher Education Fund Act);
ii)
Hoja Binafsi ya Mheshimiwa James Francis Mbatia, Mbunge wa Kuteuliwa
kuhusu udhaifu ulioko katika Sekta ya Elimu Nchini;
iii)
Hoja Binafsi ya Mheshimiwa Dkt. Hamisi Andrea Kigwangalla, Mbunge wa
Nzega ya kuitaka Serikali ianzishe Mpango Maalum wa Kukuza Ajira kwa Vijana na
kuanzisha Mfuko wa Mikopo ya Vyama Wanaowekeza kwenye Kilimo na Viwanda vyenye
uhusiano wa moja kwa moja na Kilimo; na
iv)
Hoja Binafsi ya Mheshimiwa John Mnyika, Mbunge wa Ubungo juu ya
Kuboresha Upatikanaji wa Maji Safi na ushughulikiaji wa Maji Taka katika Jiji
la Dar es Salaam.
d) Maazimio
7.
Mheshimiwa Spika, vilevile, katika Mkutano huu, Waheshimiwa Wabunge waliweza
kujadili na kupitisha Maazimio Mawili yafuatayo:
i)
Azimio la Bunge la Kujiunga na Mkataba wa Kuzuia na Kuadhibu Uhalifu
Dhidi ya Watu wenye Kinga ya Kimataifa pamoja na Wakala wa Ki-Diplomasia (Convention
on The Prevention and Punishment of Crimes Against Internationally Protected
Persons Including Diplomatic Agents 1973); na
ii)
Azimio la Bunge la Kujiunga na Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Vitendo
vya Ugaidi wa Kutumia Nyuklia (International Convention for Suppression of Act of Neuclear Terrorism, 2009).
Ninawashukuru
Waheshimiwa Wabunge kwa kukamilisha Mijadala hiyo.
UJENZI
WA UMOJA WA KITAIFA
8.
Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee Taifa letu limejaliwa na Mwenyezi Mungu
kutimiza miaka zaidi ya 51 sasa ya
Uhuru likiwa bado linaendelea kudumisha Umoja wa Kitaifa. Umoja huu wa Kitaifa umejengwa kwenye nguzo na
misingi imara ya Amani, Utulivu na Mshikamano. Mimi naamini sote tunapaswa
kujivunia Umoja huu wa Kitaifa ambao ni Tunu kubwa na nguzo muhimu ya maendeleo
yetu. Msingi mkubwa wa Umoja wa Kitaifa tunaoshuhudia leo uliwekwa na malezi
mazuri ya Waasisi wa Taifa hili wakiongozwa na Baba wa Taifa, Mwalimu Julius
Kambarage Nyerere na Hayati Abeid Amani Karume. Aidha, Katiba ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania inasisitiza, pamoja na mambo mengine, kujenga Jamii
inayozingatia misingi ya Uhuru, Haki, Udugu na Amani. Ni jukumu la kila
Mwananchi kulinda Umoja huu ambao hauna mbadala.
9.
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu ina Makabila zaidi ya 120 ambayo kwa Mujibu wa
Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya Mwaka 2012 yamefikisha Idadi ya Watu Milioni
44.929. Aidha,
hivi sasa tuna Madhehebu ya Dini yaliyoandikishwa takriban 885 na Mashirika Yasiyo ya
Kiserikali zaidi ya 6,675 na tumejenga Demokrasia ya Vyama vingi vya Siasa ambapo hadi
sasa tuna Vyama vya Siasa 19 ambavyo vimepata Usajili wa Kudumu. Licha ya kuwepo
kwa Idadi kubwa ya Watu wa Makabila tofauti yenye desturi mbalimbali na makundi
mbalimbali ya Madhehebu ya Dini, Itikadi za Kisiasa na Watu wenye Rangi
mbalimbali, bado tunajivunia kwamba tunaheshimiana na hatubaguani kwa namna
yoyote ile. Hali hii ya amani imeipatia Nchi yetu sifa Kitaifa na Kimataifa na
mfano wa kuigwa.
10.
Kutokana na Demokrasi pana iliyopo, Wananchi wetu wana Uhuru mkubwa wa
kutoa maoni, kuanzisha na kujiunga na Vyama vya Siasa pamoja na kushiriki
katika kuchagua Viongozi wa Chama chochote wanachokipenda kwa kuzingatia
Misingi ya Katiba na Sheria za Nchi. Vilevile, Serikali imetoa uhuru mkubwa wa
kupata na kutoa habari kwa uwazi bila vikwazo vyovyote kwa kuzingatia Katiba,
Sheria na Kanuni mbalimbali na Maadili ya Vyombo vya Habari. Kutokana na Uhuru
huo, Idadi ya Vyombo vya Habari imeongezeka sana ambapo hadi sasa Idadi ya
Vituo 86 vya Redio vilivyopewa Leseni na vinafanyakazi, Vituo vya Televisheni 26
na
Magazeti 768 yaliyoandikishwa na yanayotolewa na Taasisi mbalimbali.
11.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo yanayodhihirika wazi, hivi karibuni
kumekuwepo na dalili za kupoteza sifa yetu nzuri ya Umoja wa Kitaifa na Amani
ambayo imedumu kwa miaka mingi. Tumeshuhudia Wananchi mmoja mmoja wakishindwa
kuvumiliana, japo kwa tatizo dogo tu miongoni mwao. Aidha, tumeshuhudia Vyama
vya Siasa vikionesha dalili ya kuhamasisha Wanachama wao kuingia kwenye malumbano ya Siasa baina yao
wenyewe kwa wenyewe au baina ya Chama kimoja cha
Siasa na Chama kingine. Baadhi ya Wanachama wameshikana mashati na kujeruhiana.
12.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwaasa Viongozi wa Vyama vya
Siasa kuepuka kutumia majukwaa ya Siasa kuvuruga Amani yetu na Utulivu uliopo. Waepuke
matamko ya vitisho na kuhamasisha Wanachama wao kuendeleza vitendo vya uvunjifu
wa amani na kujenga chuki na uhasama miongoni mwa Jamii na kwa Serikali halali
iliyopo madarakani. Pamoja na
kutofautiana kwa mawazo na Sera za Vyama vya Siasa, ni muhimu tujenge mazingira
ya kuvumiliana kwa hali ya juu katika kujenga Demokrasia ya kweli hapa Nchini.
Viongozi wa Vyama wanatakiwa kueleza Sera zao badala ya kutukanana, kubezana,
kushutumiana na kuzomeana. Tujenge Nchi yetu kwa Amani na Utulivu ndipo
tutapata maendeleo endelevu.
13.
Mheshimiwa Spika, tumeshuhudia pia kuibuka kwa choko choko za Kidini. Baadhi
ya Waumini wa Dini wamekuwa wakikashifu Dini nyingine kwa kejeli na vitendo
vingine visivyostahili. Aidha, baadhi ya Viongozi wa Madhehebu ya Dini wamekuwa
wakiwaingiza Waumini wao katika Migogoro isiyoisha, ikiwa ni pamoja na
kufungiana milango na kuzuia Waumini Wasiabudu siku za Ibada. Napenda kusisitiza
kuwa Madhehebu ya Dini yana nafasi kubwa ya kujenga Umoja wa Kitaifa, Amani na
mshikamano. Nawaomba Viongozi wa Madhehebu ya Dini kutatua kwa amani migogoro
iliyopo na kuelimisha Waumini wao kuthamini, kujenga na kuenzi Amani na Utulivu
uliopo Nchini. Serikali imetoa uhuru wa Wananchi wake Kuabudu, kila mtu kwa
Dini anayoitaka. Hivyo, hakuna sababu ya Dini moja kukashifu Dini nyingine. Aidha,
tupinge kwa nguvu zetu zote choko choko za Kidini ambazo zimeanza kujitokeza
katika sehemu mbalimbali Nchini.
14.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali baadhi yao
yamekuwa yakihusishwa kuwa mstari wa mbele katika kuwarubuni Wananchi kufanya
vurugu zinazolenga kuleta uvunjifu wa Amani. Napenda kusisitiza kuwa Mashirika
Yasiyo ya Kiserikali yana jukumu kubwa la kuelimisha Wananchi kuhusu umuhimu wa
kujenga Umoja wa Kitaifa. Viongozi wa Mashirika haya waepuke kutumiwa na baadhi
ya Viongozi kujenga mbegu mbaya kwa Wananchi kuvuruga Amani.
15.
Mheshimiwa Spika, nigusie pia Vyombo vya Habari, ambapo kumekuwa na kutiliana
mashaka kwa baadhi ya Vyombo hivyo kuandika habari za Uchochezi, hivyo
kuashiria Uvunjifu wa Amani na Mshikamano wa Kitaifa tuliojijengea. Vyombo vya
Habari vina wajibu mkubwa wa kuelimisha Umma na kuhabarisha kuhusu masuala
mbalimbali ya maendeleo, kama wafanyavyo wenzetu jirani, husan Vyombo vya
Habari vya Nchi ya Rwanda. Aidha, Vyombo hivi vina fursa nzuri ya kutumia uhuru
uliopo kudumisha Amani na Utulivu Nchini.
Tufanye Nini
16.
Mheshimiwa Spika, kutokana na changamoto zilizopo za baadhi ya Watu waotaka
kubomoa Umoja wa Taifa letu na kuhatarisha Amani na Utulivu Nchini, sisi kama
Taifa hatuna budi kufanya yafuatayo:
i)
Serikali, Wananchi na Wadau wote ikiwemo Vyama vya Siasa, Madhehebu ya
Dini, Vyombo vya Habari, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, n.k. tunapaswa tukae
chini tuzungumze na kutafakari kuhusu hali hii;
ii)
Tunapaswa kwa namna zote tuvumiliane na kuheshimiana kwa kuzingatia
Utamaduni wa Kitanzania na Misingi ya Amani na Utulivu tuliojijengea kwa muda
mrefu; na
iii)
Wananchi wote tuzingatie na kuheshimu Utawala Bora wa Sheria, Kanuni na
Taratibu zilizopo.
17.
Mheshimiwa Spika, napenda kutumia fursa hii kuwaomba sana Wananchi na
Watanzania wenzangu kuendeleza umoja
na mshikamano wa
Kitaifa ili kudumisha Amani na Utulivu uliopo Nchini. Ni vyema kutambua kuwa Amani na Utulivu uliopo Nchini ni mazingira
wezeshi ya kusaidia kila mmoja
wetu kufanya shughuli zake za kijamii na kiuchumi na kujiletea maendeleo. Bila Amani na Utulivu hakuna maendeleo
ya Watu. Kwa upande wa Serikali itahakikisha kwamba, Umoja tuliojijengea
unadumishwa. Taasisi mbalimbali za Serikali, zikiwemo Vyombo vya Dola ni lazima
zihakikishe kwamba, Wananchi wanaishi kwa Amani na Utulivu. Vilevile,
kuhakikisha kuwa, Umoja wa Kitaifa tulioujenga kwa miaka mingi haupotei. Naziomba
Taasisi zote zinazohusika na kusimamia Amani na Usalama kuhakikisha kuwa,
pamoja na Changamoto zilizopo, Umoja wa Kitaifa unadumishwa.
HALI YA
CHAKULA NCHINI
i)
Hali ya Mazao na Mvua
18.
Mheshimiwa Spika, tathmini iliyofanyika
hivi karibuni juu ya upatikanaji wa chakula Nchini na athari za mvua
zinazoendelea kunyesha, inaonesha kuwa maeneo mengi hasa, yale yanayopata mvua
za msimu kama vile Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Iringa, Tabora, na Mtwara mazao mengi
yapo katika hatua mbalimbali za ukuaji. Inatarajiwa kwamba, endapo mvua hizi
zitaendelea vema, upatikanaji wa chakula katika maeneo hayo utakuwa mzuri.
19.
Mheshimiwa Spika, pamoja na hali hiyo ya hewa, tathmini ya kina ya hali ya
chakula na lishe iliyofanyika mwezi Januari 2013 inaonesha upungufu wa chakula katika
Wilaya 47 zilizoko katika Mikoa 15 ambazo zitahitaji msaada wa chakula
katika vipindi tofauti. Inakadiriwa kuwa jumla ya Watu 1,615,445 watahitaji jumla ya Tani
32,870
za chakula.
ii) Hatua
Zinazochukuliwa na Serikali
20.
Mheshimiwa Spika, kutokana na matarajio hayo ya uhaba wa Chakula, Serikali
itahakikisha kuwa Kitengo cha Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA) kinaendelea
kusambaza mahindi katika maeneo yenye uhaba wa chakula. Hadi sasa jumla ya Tani
20,000
zilishatolewa kwa Mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida,
Morogoro, Lindi, Tanga, Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga,
Simiyu, Mara na Tabora. Aidha, Kitengo hicho (NFRA) kitaendelea kununua nafaka
mapema baada ya mavuno ili kuhakikisha kuwa Serikali ina hifadhi ya kutosha ya
chakula kwa ajili ya kusambaza katika maeneo yatakayokuwa na uhaba wa chakula.
Hadi tarehe 6 Februari 2013 Ghala la Taifa la Chakula lilikuwa na jumla ya Tani
68,712.9 za mahindi pamoja na Tani 3,335.989 za Mtama.
21.
Serikali itaendelea kufuatilia kwa karibu hali ya upatikanaji wa chakula Nchini na
kuhakikisha kuwa hakuna Mwananchi atakayepoteza maisha kutokana na njaa. Nitoe
wito kwa Wananchi kuendelea kuweka utaratibu wa kuhifadhi sehemu ya mavuno yao
baada ya kuvuna kwa ajili ya akiba ya baadaye badala ya kuuza mavuno yao yote.
MAPAMBANO DHIDI YA UGONJWA WA MALARIA NCHINI
i)
Hali Halisi ya Ugonjwa wa Malaria Nchini
22.
Mheshimiwa Spika, Nchi yetu inayo changamoto kubwa ya kukabiliana na Magonjwa
makubwa Duniani, yakiwemo Malaria, Kifua Kikuu, UKIMWI, Saratani, n.k. Niruhusu
leo katika Hotuba yangu nizungumzie kidogo kuhusu Ugonjwa wa Malaria. Ugonjwa
wa Malaria bado unaongoza kuwa sababu kubwa za Wagonjwa wengi wanaohudhuria
katika Vituo vya huduma za Afya Nchini. Aidha, ugonjwa huu unaongoza kwa
kusababisha vifo, hasa kwa Watoto walio chini ya umri wa miaka Mitano. Takwimu
kutoka Vituo vya kutolea huduma ya Afya Nchini zinaonesha kuwa, takriban
Wagonjwa Milioni 11 hadi 12 huhudhuria katika Vituo vya huduma za Afya kwa sababu ya
ugonjwa wa Malaria. Vilevile, tafiti zilizofanyika katika Jamii [Tanzania
HIV/Malaria Indicator Survey (THMIS) 2011/2012] zinaonesha kuwa Asilimia 10 ya Watoto katika Kaya
wana maambukizi ya vimelea vya ugonjwa wa Malaria.
ii) Jitihada
za Serikali katika kumaliza tatizo la Malaria Nchini
23.
Mheshimiwa
Spika, ili kukabiliana na tatizo hili katika kuhakikisha
Wananchi wanaendelea kujikinga na maambukizi dhidi ya ugonjwa wa Malaria,
Serikali imefanya mambo muhimu yafuatayo:
Moja: Kutekeleza Mpango Mkakati wa Taifa wa
Mapambano Dhidi ya Ugonjwa wa Malaria wa Miaka Mitano (2008-2013) ambao una
lengo la kupunguza vifo kwa Asilimia 80 ifikapo mwaka 2013 mwishoni.
Utekelezaji wa Mpango huu unafanyika kwa kushirikiana na Mikoa, Wilaya na Wadau
mbalimbali hadi katika ngazi ya Jamii;
Pili: Kusambaza
na kuongeza matumizi ya vyandarua vyenye viuatilifu vya muda mrefu katika Kaya.
Hadi sasa zaidi ya vyandarua Milioni 26 vimesambazwa
kupitia Kampeni iliyolenga Watoto wenye umri chini ya miaka Mitano;
Tatu: Kutekeleza
Mpango wa Hati Punguzo unaolenga kuhakikisha Akina Mama Wajawazito na Watoto
wanaozaliwa wanaendelea kupata vyandarua hivyo na kujikinga dhidi ya ugonjwa wa
Malaria;
Nne: Kuendeleza
Mpango wa kunyunyizia dawa ya ukoko majumbani ili kutokomeza mazalia ya Mbu.
Mpango huo unaendelea kutekelezwa katika Mikoa ya Kagera, Mwanza na Mara ambapo
zaidi ya Kaya 1,440,000 sawa na Asilimia 90 katika
Wilaya za Mikoa hiyo zitanyunyiziwa viuatilifu. Kutokana na Mpango huo, zaidi
ya Watu 6,500,000 wameendelea kukingwa dhidi ya
maambukizi ya ugonjwa wa Malaria;
Tano: Kuendeleza
Mpango wa kuangamiza viluwiluwi vya Mbu kwa kutumia njia za Kibaiolojia. Mpango
huu ambao unafanywa na Serikali kwa ushirikiano na Serikali ya Nchi ya Cuba
unatekelezwa katika Jiji la Dar es Salaam kuanzia mwaka 2011;
Sita: Kutumia
Mwongozo wa kutibu ugonjwa wa Malaria isiyo kali kwa kutumia Dawa ya Mseto ya Artemether/Lumefantrine
(ALu). Mwongozo huu unaendelea kutumika katika Vituo vyote vya
Umma vya kutolea huduma za Afya; na
Saba: Kusambaza
kipimo cha haraka cha kutambua na kuthibitisha uwepo wa vimelea vya Malaria
kwenye damu katika Vituo vyote vya Umma vya kutoa huduma za afya Nchini.
iii) Changamoto
24.
Mheshimiwa Spika, pamoja na mafanikio hayo makubwa yaliyopatikana, bado kuna
changamoto ambazo zinahitaji kufanyiwa kazi. Changamoto hizo ni pamoja na:
Moja: Kujitokeza
kwa usugu wa mbu dhidi ya viuatilifu vya aina ya “pyrethroids” vinavyotumika katika
vyandarua na unyuziaji dawa ya ukoko majumbani;
Pili: Kupata
vyanzo zaidi vya fedha za ndani za kuendeleza mkakati wa unyunyiziaji dawa ya
ukoko majumbani;
Tatu: Uwezo
mdogo wa uzalishaji wa dawa za kuangamiza viluwiluwi vya Mbu na kuanza
kuangamiza Viluwiluwi hivyo katika Jiji la Dar es Salaam; na
Nne: Kuendeleza
uhamasishaji Wananchi kutumia nyenzo na kushiriki katika mikakati iliyopo, hasa
inayohitaji ushiriki wao wa moja kwa moja, kama kuharibu mazalia ya Mbu.
iv) Matarajio
ya Mkutano wa United Against Malaria – Afrika Kusini
25.
Mheshimiwa Spika, katika juhudi za kupambana na Malaria Duniani, Shirika la Roll
Back Malaria Partnership wakishirikiana na Wizara ya Afya ya Afrika Kusini
wanatarajia kufanya Mkutano mkubwa unaohusu mapambano dhidi ya Malaria kwa Nchi
za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuanzia tarehe 9 - 11
Februari, 2013. Mkutano huo unatarajia kukutanisha Viongozi wa ngazi ya juu
kutoka Nchi za SADC ikiwa ni pamoja na baadhi ya Marais, Mawaziri Wakuu, Mawaziri wa Afya na Mawaziri wa
Michezo katika Nchi hizo. Mkutano huo pia utajumuisha Viongozi wa juu wa
Makampuni mbalimbali ya Sekta Binafsi.
26.
Mheshimiwa Spika, lengo la Mkutano huo ni kukutanisha Viongozi mbalimbali kwa
lengo la kuendesha mjadala kuhusu janga la Malaria katika Nchi za Afrika;
ikizingatiwa kuwa ufadhili wa utekelezaji wa mikakati mbalimbali unazidi
kupungua. Mkutano huo unategemewa kuwa chachu kwa Viongozi kuongeza Bajeti za
udhibiti wa Malaria Nchini mwao na kuongeza ushirikiano na Sekta Binafsi pamoja
na Sekta ya Michezo, hususan katika Mpira wa Miguu katika dhana nzima ya
Mpango wa “Safe Companies”. Aidha, Mkutano huo unatarajiwa kuongeza kasi ya Kupambana
dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika Nchi hizo.
27.
Ni matumaini yangu kuwa, Mkutano huo utakuwa wa mafanikio makubwa kwa
Nchi za Kusini mwa Afrika katika vita dhidi ya ugonjwa wa Malaria. Vilevile,
utatupatia uzoefu kwa Nchi yetu katika kupambana na Ugonjwa huu wa Malaria.
v) Jitihada
za Chama cha Wabunge cha Kupambana na Malaria
28.
Mheshimiwa Spika, katika jitihada za kupambana na Malaria Nchini, Muungano wa Wabunge wa Bunge la
Jamhuri ya Muungano ya Tanzania walianzisha Asasi inayojulikana kama Tanzania
Parliamentary Against Malaria (TAPAMA). Lengo la kuanzishwa kwa Asasi hii
ni kuongeza utashi wa Kisiasa katika kushiriki na kutekeleza Mpango na Sera ya Taifa ya kutokomeza
Ugonjwa wa Malaria Nchini. Asasi hii ilisajiliwa mwaka 2008 na hadi sasa
imetekeleza masuala mbalimbali katika jitihada zake za kupambana na Malaria
Nchini kama ifuatavyo:
Moja: Ugawaji wa Vyandarua kwa Watoto
wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi kwa Mikoa ya Ruvuma, Kilimanjaro
na Mwanza ambapo zaidi ya Watoto 2,500 walifaidika na huduma hii;
Pili: Kufanya mazungumzo na Wawakilishi wa
Bunge la Jumuiya ya Ulaya mwaka 2009 waliotembelea Tanzania na kuona uwezekano
wa Jumuiya ya Ulaya kusaidia zaidi Mapambano dhidi ya Malaria Tanzania. Aidha,
walifanya mazungumzo na Viongozi na Wawakilishi wa Asasi ya Malaria No
More
ya Marekani, ambao waliongozwa na Balozi Mark Green na kuwezesha kuanza kwa
Mradi wa Zinduka, Malaria Haikubaliki;
Tatu: Kushiriki Kikao cha Nchi za Jumuiya ya Ulaya Nchini Ufaransa mwaka
2009 ili kujadili juhudi za Viongozi wa Kisiasa katika Kupamabana na Malaria
Nchini;
Nne: Kushiriki kutayarisha Mwongozo (Advocacy
Guideline)
utakaotumiwa na Wabunge, Madiwani na Viongozi wengine wa Kisiasa na Kijamii
katika Utekelezaji na ushawishi wao katika kutokomeza Malaria Tanzania.
29.
Mheshimiwa Spika, nachukua fursa hii kuwapongeza Wajumbe wote wa TAPAMA chini
ya Uongozi wa Mheshimiwa Riziki Said Lulida, Mbunge wa Viti Maalum kwa juhudi
zao za kuhakikisha kuwa wanaungana na Wadau wengine Nchini na Duniani katika
kutokomeza ugonjwa wa Malaria. Nazipongeza pia Taasisi Zisizo za Kiserikali kwa
ujumla wao ambazo zimejitokeza katika Mapambano dhidi ya Magonjwa mbalimbali,
yakiwemo UKIMWI, Kifua Kikuu, Saratani, n.k. Tunawaomba Waheshimiwa Wabunge
zaidi wazidi kujiunga na Asasi hizi na hasa za Magonwa ili kuweka hamasa kwa
Wananchi katika Kupambana na Maradhi hayo. Aidha, natoa wito kwa Wananchi wote
kwa ujumla kuunganisha nguvu za Kupambana na Ugonjwa huu wa Malaria ili
kunusuru nguvukazi ya Watanzania. Suala kubwa ni kuzingatia masharti ya
Wataalam kuanzia katika kutunza mazingira yetu na kutumia Vyandarua kama kinga
iliyo ya uhakika.
LISHE
30.
Mheshimiwa Spika, wakati nikitoa hoja ya kuahirisha Mkutano wa Tisa wa Bunge, mwezi Novemba, 2012 nilieleza
kwa kifupi utekelezaji wa Mkakati wa Taifa wa Lishe wa Mwaka
2011/2012 – 2015/2016. Pamoja na mambo mengine nilionesha hatua ambazo Serikali
inachukua kuondokana na tatizo la Lishe Nchini. Jambo
kubwa na la msingi katika kupambana na tatizo la Lishe ni kutoa elimu kwa Jamii
ili kula vyakula vyenye Virutubisho muhimu hasa kwa Mama Wajawazito na Watoto
Wachanga. Jitihada za Serikali za kuwashirikisha Wadau mbalimbali katika kutoa
Elimu ya Lishe Nchini zimeleta mwamko mzuri ambapo Wadau mbalimbali wakiwemo
Mamlaka za Serikali za Mitaa, Mashirika Yasiyo ya Kiserikali na Wadau wa
Maendeleo sasa wanashiriki kikamilifu katika utoaji elimu na kukuza kilimo cha
mazao yenye virutubisho muhimu ili kuongeza vyakula vyenye virutubisho.
31.
Mheshimiwa Spika, katika kuunga mkono
jitihada za Serikali za kupambana na tatizo la Lishe Nchini, hivi karibuni
Waheshimiwa Wabunge chini ya Uenyekiti wa Mheshimiwa Lediana Mafuru Mng’ong’o
Mbunge wa Viti Maalum wameunda Kikundi cha kuongeza hamasa na kuzidisha chachu
ya kutoa elimu kuhusu Lishe Bora hapa Nchini. Nimearifiwa kwamba, Kikundi hicho
cha Wabunge kimekutana tarehe 10 hadi 12 Januari, 2013 na kukubaliana kuhusu
kazi ambazo watafanya ili kuongeza sauti yao kwenye jamii juu ya umuhimu wa
Lishe Bora. Kikundi pia kimeandaa
Mpango Mkakati wa Miaka Mitatu (2013-2015) wenye malengo ya kukuza uelewa wa
Umma juu ya Lishe, Chakula na Haki za Watoto. Aidha, kikundi hicho kiliazimia
kushawishi uwekaji wa vipaumbele vya Lishe katika Mipango ya Maendeleo na
Bajeti za Wizara, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa na kuingiza masuala ya
Lishe, Chakula na Haki za Watoto katika Sera na Mikakati mbalimbali ya
Serikali. Azimio lingine ni kuimarisha usimamizi wa kazi za Bunge kuhusu Lishe,
Chakula na Haki za Watoto.
32.
Mheshimiwa Spika, napenda kuchukua fursa
hii kukishukuru kwa dhati kikundi hiki ambacho kimeona umuhimu wa kuunga mkono
juhudi za Serikali za kupambana na tatizo la Lishe, ikiwemo Utapiamlo. Nitumie
fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge kwa kuanzisha kikundi hiki.
Niwashukuru kwa kuona umuhimu wa kusimamia tatizo hilo ili kupata suluhu ya
kudumu. Ninatambua pia umuhimu wa Waheshimiwa Wabunge kuhamasisha masuala ya
Lishe kwa Wananchi wa Majimbo yao. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge wengine wote
kushiriki kutoa msukumo wa pekee kwa Wananchi wa Majimbo yenu katika Mapambano
dhidi ya Utapiamlo ili kwa pamoja tujenge Taifa lenye Watu walio na Lishe Bora.
Lengo ni kuwawezesha kuchangia zaidi katika uzalishaji mali na ukuaji wa uchumi
wa Nchi kwa ujumla.
MCHAKATO
KUELEKEA KATIBA MPYA
33.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa, Tume ya Mabadiliko ya
Katiba imetangaza kumaliza kazi ya kukusanya maoni binafsi ya Wananchi mmoja
mmoja kama mchango wao kwa ajili ya kuandika Katiba Mpya. Aidha, imekamilisha
kazi ya kukutana na Makundi Maalum, Viongozi wa Kitaifa Wastaafu na Viongozi wa
Kitaifa waliopo Madarakani. Kwa maana hiyo, Tume sasa imekamilisha kazi ya
ukusanyaji maoni kama ilivyopangwa. Hivi sasa Tume inaendelea na kazi za
uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na Wananchi na yale yaliyotolewa na Makundi
Maalum ili baadaye kutayarisha Rasimu
ya Katiba ambayo itawasilishwa katika Mabaraza ya Katiba yatakayoitishwa na Tume
Nchini kote.
34.
Kulingana na Ratiba, Mikutano ya Mabaraza ya Katiba itafanyika kuanzia
mwezi Juni, 2013 na itajumuisha Wajumbe watakaochaguliwa na Wananchi wenyewe
kuanzia ngazi ya Kijiji. Wajumbe hao ndio watapaswa kuwasilisha maoni ya
Wananchi katika Mikutano ya Mabaraza.
35.
Mheshimiwa Spika, nimearifiwa kuwa Tume imeandaa Rasimu ya Mwongozo wa namna
bora na ya Kidemokrasia ya kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ambao
unaendelea kusambazwa Nchi nzima. Mwogozo huo tayari umetangazwa katika Vyombo
vya Habari ili Wananchi waufahamu na kutoa maoni kuhusu namna ya kuuboresha.
36.
Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa Rasimu hiyo ya Mwongozo, katika Mikoa ya
Tanzania Bara ukiondoa Mkoa wa Dar es Salaam, kila Kata itawakilishwa na
Wajumbe wanne (4) watakaochaguliwa kutoka miongoni mwa Wakazi wa Vijiji
vilivyopo kwenye Kata ambao wataungana na Madiwani wa Kata na Madiwani wa Viti
Maalum kuunda Baraza la Katiba la Wilaya. Kwa Mkoa wa Dar es Salaam, Tume
imeandaa utaratibu tofauti wa kuwapata Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya
ambapo kila Kata watatoka Wajumbe wanane (8) ambao wataungana na Madiwani wa
Kata na Madiwani wa Viti Maalum. Kwa msingi huo, kutakuwa na jumla ya Wajumbe 18,169 watakaohudhuria Mabaraza
ya Katiba ya Wilaya Kwa Tanzania Bara.
37.
Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Zanzibar, kutakuwa na Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa 13. Kila Shehia itawakilishwa na Wajumbe watatu (3), ambao
wataungana na Madiwani wa Wadi, Madiwani wa Viti Maalum na Madiwani wa
kuteuliwa waliopo kazini kwa sasa. Kwa msingi huo, Wajumbe wote wa Mabaraza ya
Katiba kwa Zanzibar watakuwa 1,198.
38.
Wananchi wanaopenda kuwa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba ya Wilaya
watatakiwa kuwasilisha majina yao
kwa Maafisa Watendaji wa Vijiji na
Mitaa kwa Tanzania Bara na kwa upande wa Tanzania Zanzibar watawasilisha kwa
Sheha kwa tarehe itakayoelekezwa na Tume ya Mabadiliko ya Katiba hapo baadaye.
39.
Mheshimiwa Spika, napenda kutoa wito kwa Viongozi wote katika ngazi za Wilaya
na Serikali za Mitaa kusimamia kikamilifu utaratibu ambao umewekwa na Tume. Kwa
kufanya hivyo, Wajumbe ambao watashiriki katika Mabaraza ya Katiba watapatikana kwa njia za
Kidemokrasia na hivyo, kufanikisha Vikao vya
Mabaraza ya Katiba. Ni matumaini yangu kuwa Wananchi watausoma Mwongozo huo, na
baadaye kuwasilisha mapendekezo na maoni yao kwa Tume kabla ya kazi ya uchaguzi
wa Wajumbe wa Mabaraza ya Katiba kuanza rasmi.
40.
Nitumie fursa hii kuwaomba Wananchi wote kushiriki kikamilifu kutoa
maoni kuhusu Mwongozo huo na pia katika kuwapata Wajumbe watakaoshiriki katika Mabaraza
ya Katiba kwa mujibu wa Sheria, na vilevile Wajumbe hao washiriki kikamilifu
katika Vikao vya Mabaraza ya Katiba na kutoa maoni kwenye Rasimu ya Katiba.
RIPOTI YA TATHMINI YA UTAWALA BORA AFRIKA (APRM)
41.
Mheshimiwa Spika, katika kuendeleza
dhamira ya uwazi na ujenzi wa pamoja wa utawala bora nchini kwa kuwashirikisha
Wananchi, Nchi yetu imekuwa miongoni mwa Nchi 33 za Umoja wa Afrika zilizoamua
kwa hiari yake kujiunga na Mpango wa Bara la Afrika wa Kujitathmini Kiutawala
Bora (The African Peer Review Mechanism - APRM). Tanzania ilijiunga na mchakato
huo mwaka 2004, na Bunge liliuridhia mwaka 2005.
42.
Mheshimiwa Spika, Mpango huu wa
kujithamini Kiutawala Bora ni muhimu kwetu na unaakisi Sera zetu na za Waasisi
wa Taifa hili juu ya Kujikosoa na Kujisahihisha. Aidha, unahusisha Viongozi wa
Afrika na unatoa fursa kwa Wananchi kutathmini hali ya Utawala Bora katika Nchi
zao na kuainisha kwa pamoja mambo mazuri yanayopaswa kuendelezwa na yale yenye
changamoto za kufanyiwa kazi. Miongoni mwa sababu za Nchi yetu kujiunga na
Mpango huu ni kutokana na ukweli kwamba Watanzania tuna mengi ya kuifundisha
Afrika na Watu wake kuhusu Utawala Bora na sisi pia kujifunza kutoka kwa
wenzetu.
43.
Mheshimiwa Spika, ninayo furaha kulifahamisha Bunge lako Tukufu kuwa baada ya
zoezi la muda mrefu la kukusanya maoni Nchi nzima kuhusu Mpango huu ambapo
Waheshimiwa Wabunge nao walishiriki kutoa maoni yao kuhusu Utawala Bora, sasa
hivi Nchi yetu, imefikia hatua muhimu katika Mchakato huo wa kujitathmini
kiutawala bora.
44.
Tarehe 26 Januari 2013, Ripoti ya Hali ya Utawala Bora hapa nchini
iliwasilishwa mbele ya Wakuu wa Nchi za APRM Addis Ababa, Ethiopia ambapo
Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wetu alipata fursa ya kuzungumzia
mwelekeo wa Nchi yetu katika kujenga Taifa imara zaidi katika kipindi cha miaka
50 ijayo.
45.
Mheshimiwa Spika, katika Ripoti hiyo ambayo itatumika kama rejea,
zimeainishwa juhudi zetu kubwa za kulinda amani Nchini. Pamoja na kuimarisha
Utawala Bora wa Sheria na Haki za Binadamu. Aidha, kupitia Ripoti hiyo, wenzetu
katika masuala ya kuendesha Utawala Bora, Barani Afrika na Duniani kwa ujumla
wametambua jitihada zetu pamoja na mambo mengine katika kuulinda Muungano,
kuimarishwa kwa mapambano dhidi ya Rushwa na zaidi ya yote wamejua sura ya
Tanzania katika ukombozi na utetezi wa amani Afrika ambao Nchi yetu imepongezwa
sana kwa juhudi zake.
46.
Ripoti hiyo pia imeainisha
changamoto ambazo wenzetu wa Afrika wanadhani tunapaswa kuzifanyia kazi zaidi.
Changamoto hizo ni pamoja na suala la kushughulikia Kero za Muungano,
kuimarisha zaidi juhudi za kuondoa umaskini na kuilinda amani ya Nchi yetu hasa
kutokana na chokochoko za Kidini zilizoanza kujitokeza. Tumeaswa kuutumia vyema
mchakato wa sasa wa Mabadiliko ya Katiba kuijenga Tanzania bora zaidi katika
miaka 50 ijayo.
47.
Mheshimiwa Spika, kuwasilishwa kwa Ripoti hiyo ya APRM kwa Wakuu wa Nchi wa
Mpango huu ndio mwanzo sasa wa Serikali yetu ya kuimarisha maeneo yaliyoonekana
kuwa tunafanya vyema. Pia hatua hiyo inatoa fursa ya kuanza kutekeleza
Mpangokazi wa Miaka Mitano ambao umeainisha namna gani ya kuyafanyia kazi
maeneo ambayo wananchi waliyaona kuwa yanapaswa kufanyiwa kazi zaidi. Suala
hili liliwekewa msisitizo na Mheshimiwa Rais katika Hotuba yake ya Mwisho wa
Mwezi Januari 2013 aliyoitoa kwa Taifa.
48.
Mheshimiwa Spika, kutokana na manufaa ya APRM kama daraja kati ya Serikali na
Wananchi wa kutatua matatizo yetu kwa pamoja, Serikali itaendelea kuiimarisha
Taasisi ya APRM hapa Nchini ili iweze kuwa kitovu chetu cha fikra (think
tank)
katika kushauri kuhusu masuala ya Utawala Bora Nchini. Vilevile, kuiwezesha
Taasisi hii kuendelea kuwa kiungo kati ya Serikali yetu na Wananchi wake katika
kutathmini na kutupatia mrejesho juu ya mipango na Sera zetu za maendeleo.
49.
Aidha, Serikali itaendelea kufadhili shughuli za APRM, kuiimarisha
Taasisi kwa raslimali watu na fedha kwa ajili ya kazi pana zaidi za kutoa
ushauri, kuunganisha Wadau mbalimbali na kuendelea kuratibu tathmini nyingine
katika siku zijazo kwa lengo la kujipa nafasi ya kujikosoa ili kujisahihisha.
Napenda kuwashukuru Wajumbe wa Kamati ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama
wakishirikiana na Sekretariati ya APRM Tanzania kwa kazi nzuri waliyoifanya
ambayo imetuwezesha kufikia mafanikio hayo.
UANZISHAJI
WA MAENEO MAPYA YA UTAWALA
i)
Uanzishaji wa Mikoa na Wilaya
50.
Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge watakumbuka kuwa, mwezi Machi 2012, Mheshimiwa
Rais aliridhia kuanzisha Mikoa Mipya Minne (4) na Wilaya 19. Napenda
kulijulisha Bunge lako Tukufu kwamba, Serikali sasa imekamilisha mchakato wa
kuanzisha maeneo hayo Mapya ya Utawala, kwa kuanzisha Mikoa Minne ya Geita,
Simiyu, Njombe na Katavi. Aidha, imekamilisha uanzishwaji wa Wilaya 19 za
Buhigwe, Busega, Butiama, Chemba, Gairo, Ikungi, Itilima, Kakonko, Kalambo,
Kaliua, Kyerwa, Mbogwe, Mkalama, Mlele, Momba, Nyang’wale, Nyasa, Uvinza na
Wanging’ombe. Mikoa na Wilaya hizo tayari zimeshaanza kufanya kazi na kutoa
huduma mbalimbali kwa Wananchi. Vilevile, Mheshimiwa Rais alishafanya Uteuzi wa
Viongozi Wakuu wa Mikoa na Wilaya Mpya. Serikali imeendelea kupeleka Watumishi
na kuanza kujenga miundombinu muhimu katika maeneo husika. Hata hivyo, pamoja
na dhamira njema ya Serikali ya kuanzisha maeneo hayo, bado zipo changamoto nyingi,
ikiwemo kupata Watumishi wa kutosha ambazo Serikali inaendelea kuzitatua.
ii)
Uanzishaji wa Halmashauri
51.
Mheshimiwa Spika, ili kupeleka huduma karibu zaidi kwa Wananchi, Serikali pia
iliazimia kuanzisha Halmashauri Mpya 37. Uanzishaji wa Halmashauri hizo
unaendelea na upo katika hatua mbalimbali kwa kuzingatia makundi yafuatayo:
Kundi
la Kwanza,
linahusu Halmashauri Mpya 8 za Manispaa, Miji na Jiji pamoja na Halmashauri
Moja (1) ya Wilaya ambazo mchakato wa uanzishaji wake tayari umekamilika
Kisheria na zimeanza kufanya kazi. Kundi hili linajumuisha Halmashauri za Jiji
la Arusha, Manispaa ya Ilemela, Manispaa ya Lindi, Halmashauri ya Mji wa
Kahama, Halmashauri ya Mji wa Masasi, Halmashauri ya Mji wa Makambako, Halmashauri
ya Mji wa Geita, Halmashauri ya Mji wa Bariadi na Halmashauri ya Wilaya ya
Busokelo. Halmashauri hizo tayari zimepata Hati na kupangiwa Wakurugenzi.
Kundi la Pili, linajumuisha Halmashauri
Kumi (10) ambazo mchakato wa kuzianzisha umekamilika na tayari zimetangazwa katika
Gazeti la Serikali la tarehe 23 Novemba 2012. Halmashauri hizo ni Kalambo, Nsimbo,
Mlele, Bumbuli, Ushetu, Msalala, Mbogwe, Busega, Momba na Kyerwa. Halmashauri
hizo kwa sasa zinaandaliwa Hati ili zianze.
Kundi
la Tatu,
ni Halmashauri za Wilaya Kumi (10) ambazo mchakato wa uhakiki wake umekamilika
na Amri za Uanzishaji zimeshasainiwa na wakati wowote zitatangazwa katika
Gazeti la Serikali. Kundi hili linajumuisha Halmashauri za Wilaya za Buhigwe,
Kaliua, Nyang’hwale, Wanging’ombe, Chemba, Mkalama, Gairo, Nyasa, Itilima na Kakonko. Aidha, zipo
Halmashauri nyingine Nne (4) katika kundi hili ambazo Amri zake zinakamilishwa
na hatimaye zitasainiwa hivi karibuni. Halmashauri hizo ni Butiama, Tarime,
Uvinza na Ikungi.
Kundi
la Nne,
linajumuisha Halmashauri Nne ambazo Mchakato wa uanzishaji wake umekamilika
isipokuwa taratibu za Kisheria haziwezi kuanza kwa sababu baadhi ya Kata katika
Halmashauri hizo ni mpya, hivyo hakuna Madiwani. Halmashauri hizo Nne (4) ni za
Miji ya Kasulu, Handeni, Tunduma na Nzega. Mathalani, katika Halmashauri ya
Mji wa Kasulu kuna Kata 14, na kati ya hizo, Kata 6 ni mpya na hazina Madiwani.
Kwa upande wa Halmashauri ya Mji wa Handeni ina jumla ya Kata 12, kati ya hizo 9 ni mpya na hazina Madiwani. Aidha,
Halmashauri ya Mji wa Tunduma ina Kata 5 mpya na zote hazina Madiwani na
Halmashauri ya Mji wa Nzega ina Kata 10, na kati ya hizo Kata 3 ni mpya na hazina
Madiwani.
52.
Mheshimiwa Spika, lengo la kuanzisha maeneo hayo mapya ni kuwawezesha Wananchi
kupata huduma karibu zaidi kwa Wananchi. Nitoe wito kwa Wakuu wa Mikoa, Wilaya
na Watendaji wote kuwaongoza Wananchi kutumia fursa hiyo ya kuanzishwa kwa
maeneo hayo katika kujiletea maendeleo. Serikali itaendelea kupeleka huduma
zaidi karibu na Wananchi ili kuongeza kasi ya maendeleo katika maeneo hayo.
Aidha, Serikali itaweka utaratibu wa kuzipatia Halmashauri zinazoanzishwa
Watumishi hatua kwa hatua.
HATUA ZILIZOCHUKULIWA
NA SERIKALI DHIDI YA WATANZANIA WALIOFICHA FEDHA HARAMU NJE YA NCHI
53.
Mheshimiwa Spika, tarehe 9 Novemba, 2012, Bunge lilipitisha Azimio Na. 9/2012
kuhusu kuitaka Serikali kuchukua hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha
haramu nje ya Nchi kufuatia Hoja Binafsi iliyowasilishwa na Mheshimiwa Zitto
Kabwe (Mb). Azimio hilo linahitaji, pamoja na mambo mengine, Serikali
iwasiliane na Benki ya Dunia kupitia Kitengo cha Asset Recovery Unit ili mabilioni
yanayomilikiwa na Watanzania katika Mabenki nje ya Nchi ambapo hufichwa kwa
kukwepa kulipa kodi yarudishwe na kwamba Watanzania wote wenye akaunti za fedha
nje ya Nchi waeleze wamezipataje ili TAKUKURU wachukue hatua za Kisheria dhidi
ya watu wote wenye kumiliki fedha na mali kinyume na mapato yao halali. Aidha,
iliazimiwa na Bunge na Serikali ikakubali kwamba, katika Mkutano wa Bunge wa 11
italeta Taarifa ya hatua iliyochukuliwa ili kuziba mianya ya utoroshaji wa
fedha nje ya Nchi.
54.
Mheshimiwa Spika, tarehe 31 Desemba, 2012, Mheshimiwa Rais aliridhia kuundwa
kwa Kamati Maalum ya Kitaifa kushughulia hoja hiyo ya kuitaka Serikali kuchukua
hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu nje ya Nchi. Kamati hiyo
inaundwa na Wajumbe wanane wanaotoka katika Taasisi za Kitengo cha Kudhibiti
Fedha Haramu; Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa; Jeshi la Polisi; Benki
Kuu ya Tanzania; Usalama wa Taifa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kazi za Kamati hiyo ni:
(i)
Kuchunguza na kubaini majina ya Watanzania wanaodaiwa kuficha fedha nje
ya Nchi kinyume na Sheria na Kanuni za Nchi;
(ii)
Kuchunguza iwapo fedha hizo ni haramu au la;
(iii)
Kutambua Mabenki na Nchi zilizofichwa fedha hizo;
(iv)
Kuandaa mashtaka dhidi ya Watanzania watakaobainika kuficha fedha haramu
nje ya Nchi; na
(v)
Kuishauri Serikali jinsi ya kuzuia uhalifu wa makosa ya fedha.
55.
Mheshimiwa Spika, Kamati hii imeanza kazi zake rasmi tarehe 9 Januari 2013 kwa
kupanga namna ya kutekeleza kazi zake ikiwemo kukusanya taarifa kuhusu
Watanzania wanaodaiwa kutorosha fedha haramu nje ya Nchi na kuangalia namna ya
kupata taarifa muhimu nje ya Nchi. Kamati hiyo inaratibiwa na Mwanasheria Mkuu
wa Serikali.
56.
Ili kuiwezesha Kamati hii kufanya kazi yake kwa ufanisi ni wazi kwamba
itahitaji kupata ushirikiano mkubwa kutoka kwa Wananchi kwa kutoa taarifa
mbalimbali kuhusu suala hili. Hivyo, natoa wito kwa Wananchi wote wenye taarifa
sahihi na za ukweli zinazoweza kuisadia Kamati kutekeleza kazi hii wanahimizwa
wajitokeze kutoa maoni yao kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na
kushirikiana kwa karibu na Kamati iliyoundwa na Serikali. Aidha, nawaomba
Waheshimiwa Wabunge nao kutoa ushirikiano wa kufanikisha kazi za Kamati hii.
HITIMISHO
57.
Mheshimiwa Spika, kwa kumalizia napenda niwashukuru wote waliofanikisha
Mkutano huu wa Kumi wa Bunge. Kipekee nikushukuru wewe binafsi Mheshimiwa Spika
kwa kutuongoza vizuri ndani ya Bunge lako Tukufu. Nimshukuru vilevile, Naibu
Spika na Wenyeviti wa Bunge kwa kuendesha Vikao vya Bunge kwa ufanisi. Aidha, niwashukuru
Waheshimiwa Wabunge kwa michango yenu. Nimshukuru Katibu wa Bunge na Wasaidizi
wake kwa huduma nzuri walizozitoa wakati wote tukiwa hapa. Niwashukuru Watendaji
wa Serikali na Taasisi mbalimbali
kwa kutekeleza majukumu yao vizuri ili kufanikisha shughuli za Bunge
zilizopangwa. Niwashukuru Waandishi wa Vyombo vya Habari kwa kutufikishia
habari kwa Wananchi yale yaliyojiri hapa Bungeni na kwa wakati. Vilevile,
navishukuru Vyombo vya Ulinzi na Usalama kwa kazi yao nzuri na Madereva wote
kwa huduma zao kwa Washiriki wa Bunge hili.
58.
Mheshimiwa Spika, baada ya kusema hayo, naomba niwatakie Safari Njema na sasa
natoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu liahirishwe hadi Siku ya Jumanne tarehe 9
Aprili, 2013 Saa 3:00 Asubuhi kwenye Ukumbi huu hapa Dodoma.
59.
Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.


No comments:
Post a Comment