TANGAZO


Monday, January 28, 2013

Mahafali ya Chuo cha TRA, Naibu Waziri Fedha, Saada Mkuya Salum, awa mgeni rasmi


Mhitimu akipeana mkono na Kamishna Mkuu wa TRA,
Harry Kitilya, baada ya kukabidhiwa cheti chake na Naibu Waziri Fedha (Saada Mkuya Salum (wa pili kushoto) mwishoni mwa wiki. (Picha zote na Kassim Mbarouk, Dotto Mwaibale)

Mhitimu aliyefanya vizuri na kushika nafasi ya kwanza katika Stashahada ya usimamizi wa Kodi (PGDT), Eunice Liheluka, akienda kutunukiwa cheti na zwadi yake.

Eunice Liheluka, akipeana mkono na Kamishna Mkuu wa TRA Herry Kitilya.
Eunice akipongezwa na mume wake Hangi Kiloba
 
Na Dotto Mwaibale
CHUO cha Kodi Tanzania (ITA), kinahitaji sh.bilioni 70
kwa ajili ya ujenzi wa kampasi mpya ili kukabiliana na
ongezeko la wanafunzi chuoni hapo ambapo tayari ombi hilo limewasilishwa Serikalini.

Hayo yalibainishwa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Profesa Palamagamba Kabudi wakati akitoa taarifa fupi kwa mgeni rasmi wa mahafali ya tano ya chuo hicho Naibu Waziri wa Fedha Saada Mkuya Dar es Salaam juzi.

Kabudi alisema,idadi ya wahitimu imeongezeka kutoka 191,mwaka 2008-2009,hadi kufikia 435,mwaka 2011-2012.

Alisema katika kipindi cha miaka minne chuo hicho kimepata faida ya kuongeza mapato yake kutoka shilingi mil.265, mwaka 2008-2009, hadi kufikia bilioni 3, kwa mwaka 2011-2012.

Akihutubia katika mahafali hayo Naibu Waziri wa Fedha Saada Mkuya alisema Serikali itashirikiana na uongozi wa chuo hicho katika kuteleza mpango kazi wa kukamilisha ujenzi wa kampasi hicho kwa lengo la kuongeza idadi ya wanafunzi wanaojifunza masomo hayo ili kupanua wigo wa mapato kwa serikali.

Waziri Mkuya alisema ujenzi wa kampasi hiyo utasaidia kuongeza idadi ya wanafunzi ambao kwa asilimia kubwa watakuwa na uwezo wa kutoa alimu ya ulipaji kodi wa hiyari kwa wananchi.

Alisema kutokana na kuwa na ongezeko kubwa la ukwepaji wa kulipa kodi wasomi hao wataweza kushirikiana na mamlaka husika kuweza kuendelea kutoa elimu hiyo kwa wananchi wote.

Kutokana na jambo hilo , Waziri Mkuya aliitaka Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), kubuni njia mbadala za kuwawezesha wananchi kupata elimu sahihi juu ya ulipaji kodi wa hiyari kwa kuzingatia mabadiliko ya mfumo wa teknolojia ya habari uliopo kwa wakati huu.

Waziri Mkuya alisema kuwa kutokana na hali halisi ya mabadiliko ya kiteknolojia mamlaka hiyo ni lazima kuziboresha njia walizokuwa wakizitumia zamani katika kutoa elimu hiyo.

“Kuna ukwepaji mkubwa wa ulipaji kodi ambao kwa kiasi kikubwa inaonekana bado raia hawajapata uelewa wa kulipa kodi kwani hawajui kuwa maendelo ya nchi yanatokana na kodi zao,”alisema Waziri Mkuya.

Mkuya alisema kwamba,TRA, wanatakiwa kuimarisha vyanzo vya ndani vya mapato ili kuongeza mapato kwa serikali jambo ambalo litasaidia kuacha utegemezi wa misaada kutoka kwa wafadhili.

Alisema siku zote mafanikio ya kukusanya kodi na kuvuka lengo yanatokana na umahiri wa utendaji wa mamlaka na wafanyakazi kwa ujumla,jambo linaloleta faraja ya kuendelea kupambana na wakwepaji wa kodi ili kuendelea kuongeza mapato.

Mahafali hayo yaliyoenda sambasamba na uzinduzi wa kitabu cha toleo la kwanza la jarida la kitaaluma, kilichoandaliwa na kufanyiwa utafiti na watafiti wa chuo hicho na kuhudhuriwa na Kamishna Mkuu wa Mapato wa nchi ya Botswana Kenailwe Morris ambao wanafunzi kutoka nchi hiyo wanasoma katika chuo hicho cha Kodi cha hapa nchini.

No comments:

Post a Comment