Rais Jakaya Kikwete (katikati), akikata utepe kuzindua rasmi jengo la Hospitali ya Mbagala katika Manispaa ya Temeke liliojengwa kwa msaada wa Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Korea kusini (KOICA), jana jijini Dar es Salaam. Wengine katika uzinduzi huo, kutoka kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Saidi Meck Sadiki, Naibu Waziri wa Afya, Dk. Seif Rashid, Mke wa Rais, mama Salma Kikwete (wa tatu kushoto) na Mbunge wa Kigamboni Dk. Faustin Ndugalile.
Na Aron Msigwa - MAELEZO.
12/12/2012 , Dar es Salaam.SERIKALI imesema kuwa itaendelea na mpango wa kuboresha huduma za afya nchini kwa kujenga, kukarabati na kuzipandisha hadhi hospitali, zahanati na vituo vya afya vilivyopo kwa lengo la kujenga uwezo na kuondoa ulazima wa Watanzania kwenda nje kutibiwa na kufuata matibabu umbali mrefu hasa maeneo ya vijijini.
Hayo yalisemwa jana jijini Dar es Salaam na Rais Jakaya Kikwete
wakati akizindua majengo ya vituo vitatu vya afya kwa ajili ya utoaji wa huduma
za afya kwa akina mama na watoto vilivyojengwa kwa msaada wa Serikali ya Korea
ya Kusini chini ya Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Korea (KOICA) katika
manispaa za Ilala, Kinondoni na Temeke kwa gharama ya shilingi bilioni
6.7.
Alisema ujenzi na uboreshaji wa miundombinu na ujenzi wa vituo vya
kutolea huduma za afya hususan wodi za akina mama na watoto pamoja na maabara za
kisasa utaboresha huduma za afya na kupunguza kwa kiasi kikubwa msongamano wa
wagonjwa wanaokuja kupata huduma za afya katika vtuo husika na kupunguza vifo
vya akina mama na watoto wakati wa kujifungua.
"Ninayo furaha kubwa kuzindua majengo haya ya kisasa ya kutolea
huduma za afya hapa Mnazi mmoja, Sinza na Mbagala yatakayotoa huduma bora za
vipimo vya maabara, uchunguzi wa magonjwa mbalimbali na wodi za kujifungulia kwa
akina mama, naamini ile adha waliyokuwa wanaipata wananchi wa maeneo haya sasa
itapungua kutokana na ubora wa majengo na vifaa vya kisasa vilivyopo"
alisema.
Kwa upande wa wataalam hususani madaktari wa kuwahudumia wagonjwa alisema kuwa juhudi zinaendelea kukabiliana na tatizo hilo kuondoa uhaba uliopo wa daktari mmoja kuhudumia wagonjwa 30,000 na kufikia uwiano uliopo katika nchi zilizoendelea ambapo daktari mmoja anahudumia wagonjwa 600 mpaka 1000.
Alisema ili kukabiliana na tatizo la uhaba wa watalaam tayari
serikali imeshatenga eneo la Mloganzila lililokua mali ya Kiwanda cha nyama cha
Tanganyika Packers litumike kwa ajili ya ujenzi wa chuo cha MUHAS na na
hospitali ya kisasa ya itakayotoa huduma za afya pia kutumika kwa ajili ya
mafunzo kutokana na eneo linalotumika sasa la Muhimbili kutotosheleza mahitaji
yaliyopo.
Alifafanua kuwa ni muhimu kwa chuo cha Muhas kuhamishiwa kwenye
eneo lililopatikana lenye ukubwa wa ekari 3000 ili kiweze kujengwa chuo kipya na
cha kisasa kitachoweza kuzalisha madaktari 12000 kwa mwaka kitakachokamilika
kabla ya mwaka 2015.
Aidha Rais Kikwete alieleza kuwa serikali inajenga chuo kipya cha
Tiba Dodoma kitakachokua na uwezo wa kuzalisha madaktari 5000 kwa
mwaka.
Kwa upande wake mkuu wa mkoa wa Dar es salaam Saidi Meck Sadiki alisema kuwa ujenzi wa vituo hivyo katika manispaa zote tatu uliogharimu kiasi cha shilingi bilioni 6.7 ulianza mwaka 2008 kwa msaada wa shirika la KOICA kutoka Korea kusini na kutoa wito kwa wananchi na wafanyakazi wa vituo vilivyozinduliwa kutunza majengo,vifaa tiba, miundombinu na magari ya kubebea wagonjwa ili yaweze kutumika kwa kipindi kirefu.
Naye Balozi wa Korea ya Kusini Jung II alisema kuwa nchi yake
iliamua kuunga mkono juhudi za Tanzania na shirika la Umoja wa Mataifa kutimiza
malengo ya Mileania kwa nchi zinazoendelea na changamoto mbalimbali za kiafya na
mapambano dhidi ya vifo vya akina mama na watoto vinavyotokana na
uzazi.
Tangu mwaka 1992 Korea ya Kusini kupitia Shirika la Maendeleo na
Ushirikiano la Korea (KOICA) imekua ikishirikiana na serikali ya Tanzania
kusaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya huduma za maji, Kilimo na Afya hususani
upande wa majengo na vifaa.



No comments:
Post a Comment