TANGAZO


Wednesday, October 10, 2012

Rais wa Zanzibar, Dk. Shein azindua ulazaji waya wa pili wa umeme Ras Fumba


Meli kubwa yenye jina la FUKADA SALVAGE, ikifanyakazi ya kuutandaza waya mpya wa umeme utakaotokea Tanzania Bara mpaka Zanzibar, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa utandikaji wa waya huo, iliyofanyika Fumba, Wilaya ya Magharibi Unguja. (Picha zote na Yussuf Simai-Maelezo, Zanzibar)




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein (wamwanzo kulia), akisikiliza maelezo ya kitaalamu kutoka kwa Naibu Mkurugenzi wa Mradi ambaye pia ni Mshauri Mwelekezi, Johan Swan (kushoto), katika hafla ya Uzinduzi wa utandikaji wa waya mpya wa umeme, iliofanyika Fumba, Wilaya ya Magharibi Unguja. Katikati ni Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhart.



Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhart akitoa hotuba katika hafla ya Uzinduzi wa utandikaji wa waya mpya wa umeme, iliyofanyika Fumba, Wilaya ya Magharibi Unguja. Kulia ni Rais wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein na kushoto ni Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idi.


Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdulla Shaaban, akitoa hotuba  yake katika hafla ya uzinduzi wa utandikaji wa waya mpya wa umeme, iliyofanyika Fumba, Wilaya ya Magharibi Unguja.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akitoa hotubia yake kwa wananchi pamoja na viongozi mbalimbali, waliohudhuria katika hafla ya uzinduzi wa utandikaji wa waya mpya wa umeme, iliyofanyika Fumba Wilaya ya Magharibi, Unguja. Kushoto ni Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Alfonso Lenhart na kulia ni Waziri wa Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati, Ramadhan Abdulla Shaaban.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Oktoba 10, 2012.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein amezindua ulazaji wa waya  wa pili wa umeme kutoka Ras Fumba Zanzibar hadi Ras Kiromoni Dar-es-Salaam  na kusema kuwa sasa mwelekeo wa kuwa na  umeme wa uhakika hapa Unguja umetia sura.

Hafla hiyo iliyofanyika huko Fumba, Wilaya ya Magharibi, Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama na serikali pamoja na wananchi kutoka maeneo mbali mbali ya Zanzibar ambapo pia, katika hafla hiyo Makamu wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad na Makamu wa Pili wa Rais Balozi Seif Ali Idd walihudhuria.

Dk. Shein alisema kuwa Serikali inathamini sana na kupongeza ustahamilivu wa wananchi katika kipindi chote cha tatizo la umeme na kutoa nasaha zake kwa wananchi kuendelea kuwa wastahamilivu kwa kipindi kifupi kilichobaki.

Aliwaeleza wananchi kuwa wakati Serikali ilipofanya maamuzi ya kuchukua hatua za dharura za kuwa na umeme wa mgao, ilifikia maamuzi ya kuzidisha jitihada zake ilizokuwa imezianzisha za kutafuta ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hilo kwa lengo la kuimarisha uchumi na ustawi wa wananchi.

Dk. Shein alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Shirika lake la umeme, kwa kushirikiana na washirika wa maendeleo ilifikia maamuzi ya kutekeleza kwa haraka miradi mbali mbali ukiwemo waya mpya wa umeme.

Alieleza kuwa waya huu mpya uliolazwa hivi leo una uwezo mkubwa zaidi ya ule mkongwe unaotumika hivi sasa, na kueleza kuwa kwa mujibu wa wataalamu waya huo mpya utakuwa na uwezo wa kusafirisha umeme wa  Megawati 100.

Dk. Shein alieleza kuwa kiwango hicho ni zaidi ya mara mbili ya uwezo wa waya wa zamani, na bila shaka ni mara mbili zaidi ya mahitaji ya umeme wa hivi sasa, na kusisitiza kuwa waya unaotumika hivi sasa bado utaendelea kutumika pindi ukihitajika hivyo ipo haja ya kuutunza na kuishughulikia miundombinu yake.


Pia, Dk. Shein alitoa pongezi na shukurani kwa Serikali ya Marekani kupitia Shirika la Changamoto la Milenia la Marekani (MCC) na MCAT kwa ushirikiano mkubwa katika kufanikisha mradi huu.

Dk. Shein alitumia fursa hiyo kuipongeza Serikali ya Japan kwa juhudi zao mbali mbali katika kuiendeleza sekta ya nishati hapa Zanzibar kupitia Shirika lake la JICA pamoja na kutoa shukurani kwa watendaji wa Kampuni ya VISCAS CORPORATION ya Japan, KALPATARU Power Transmission Ltd ya India na SYMBION-ARENA ya Marekani na Ufaransa kwa juhudi zao katika kufanikisha mradi huo

Aidha, Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar siku zote inahakikisha kuwa Zanzibar inaenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia yanayotokea duniani katika sekta ya habari na mawasiliano.

Dk. Shein alisema kuwa ndani ya bomba linalobeba waya wa umeme, utapitishwa waya wa mawasiliano ambapo ni muhimu sana katika kuimarisha mawasiliano kwa ajili ya mitandao, simu na pia katika kuimarisha huduma za redio na televisheni na kueleza kuwa mradi huo pia utasaidia kuimarisha Shirika la ZBC hapa nchini.

 Aidha, Dk. Shein alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo ni miongoni mwa jitihada za Serikali katika kutekeleza Mpango Mkuu wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) ambao sasa upo kwenye awamu ya pili.

Pamoja na hayo, Dk. Shein aliwataka wananchi kujiepusha na vitendo vya uharibifu na vya hatari kwa maisha ikiwa ni pamoja na kujenga karibu na miundombinu ya miradi hiyo na uchimbaji wa michanga karibu na nguzo za umeme.

Kadhalika, aliwataka wananchi kujiepusha na tabia ya kujenga karibu na maeneo yaliopita umeme au nyaya za mawasiliano na wawe wepesi wa kutoa taarifa kwa wahusika mara tu wanapobaini tukio linaloashiria uharibifu wa miundombinu hiyo.

Dk. Shein alitoa pongezi kwa Rais mstaafu wa awamu ya tatu Mhe. Bejamin Wilium Mkapa,  kwani wakati wa uongozi wake ndipo mazungumzo ya mradi huo yalipoanza pamoja na kutoa shukurani kwa Rais Kikwete kwa kuendeleza mchakato huo na hatimae kutia saini msaada wa fedha za mradi huo na mengineyo, Rais George Bush na Rais Obama wa Marekani kwa msaada wao huo kwa Zanzibar

Waziri wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati Mhe. Ramadhan Abdalla Shaaban katika hotuba yake fupi alieleza kuwa ukamilishaji wa mradi huo utasaidia sana kutimiza azma ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar  ya kuwapatia wananchi wake huduma bora ya umeme ili kuimarisha ustawi wa jamii, kuimarisha uchumi na kuwavutia wawekezaji.

Nae Balozi wa Marekani nchini Tanzania Mhe. Alfonso Lenhardt alieleza kuwa Marekani itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo na kusisitiza kuwa mradi huo ni hatua kubwa ya kukuza uchumi hapa nchini.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Makaazi, Maji na Nishati  Mwalimu Ali Mwalimu alisema  kuwa ni dhahiri kwamba Mradi huo utawanufaisha moja kwa moja Wazanzibari wote nchini na utahuisha mfumo wa mawasiliano ya kimtandao wakati huu ambapo Zanzibar inaingia katika mfumo wa Serikali Kimtandaop (e-Government).

Katibu Mwalimu alisema kuwa kama ulivyo ule waya wa umeme wa Pemba- Tanga, waya huu hautumii teknolojia ya mafuta kama huo uliopo hivi sasa, na kwa hivyuo changamoto zake za matengenezo ni ndogo mno kwa kulinganisha ambapo matarajio yake ni kuishi kwa muda wa miaka 40.

Alisema kuwa kwa mujibu wa ongezeko la matumizi ya umeme ya asilimia 7 kwa mwaka inategemewa kuwa waya huu utaweza kuhimili matumizi hadi mwaka 2024. Kampuni ya VISCAS ilianza rasmi kazi ya utengenezaji waya tarehe 19 Novemba mwaka 2010 na kukamilika tarehe 5 Aprili mwaka huu.

Mradi huo wa uwekaji wa njia ya pili ya umeme kutoka Ubungo Tanzania Bara hadi Mtoni Zanzibar umegharimu dola za Marekani 72,193,750.00 kati ya dola 206.5 milioni kwa sekta ya nishati Tanzania nzima, ambapo SMZ imechangia dola 1,465,625.00 kufidia mali za wananchi. Zoezi hilo litachukua siku 11 ambapo waya huo una urefu wa km 37.


No comments:

Post a Comment