TANGAZO


Monday, October 15, 2012

Naibu Katibu Mkuu Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk. Budeba afungua mkutano wa kutathmini Uvuvi, Wanyamapori, Misitu na Mifugo

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Yahana Budeba akifungua mkutano wa wadau kutathmini maendeleo ya Uvuvi, Wanyamapori, Misitu na Mifugo leo jijini Dar es Salaam. Mkutano huo uliowahusisha pia wadau kutoka nchi wafadhili wa miradi ya maendeleo na wadau kutoka asasi za kiraia, unalenga kuimarisha usimamizi wa maliasili na kupeleka madaraka ya usimamizi ngazi za vijiji. (Picha na Aron Msigwa – MAELEZO)

Washiriki wa mkutano wa tathmini ya maendeleo  ya sekta ya Uvuvi, Wanyamapori, Misitu na Mifugo wakijadili masuala mbalimbali kuhusu usimamizi endelevu wa maliasili  zilizopo katika maeneo mbalimbali nchini leo, jijini Dar es Salaam.

Washiriki wa mkutano kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, wadau kutoka asasi za kiraia zinazoshughulika na uhifadhi wa mazingira na washirika wa maendeleo wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya ufunguzi  wa mkutano huo, jijini Dar es Salaam leo.


Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dk. Yahana Budeba akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari, Dar es Salaam leo, kuhusu maendeleo ya Sekta ya Uvuvi, Misitu na Wanyamapori, pia hatua ya Serikali ya kupeleka madaraka ya usimamizi  wa maliasili katika ngazi ya kijiji.


Na Anna Nkinda- Maelezo
15/10/2012
SERIKALI imewataka wananchi kuendelea kutunza rasilimali za misitu, wanyamapori  na uvuvi ili ziweze kuwa na manufaa katika maeneo yao kwa  kuinua kipato na kupunguza umasikini katika jamii.

Hayo yamesemwa leo na Naibu Katibu Mkuu wa wizara yaMaendeleo ya Mifugo na Uvuvi Dkt. Yohana Budeba wakati akifungua mkutano wa mwaka wa wadau wa sekta ya maliasli uliofanyika katika chuo cha Taifa cha Utalii kilichopo jijini Dar es Salaam.

Dkt. Budeba alisema kuwa katika miaka ya nyuma jukumu la kutunza misitu, wanyamapori na uvuvi lilikuwa linafanywa na Serikali kuu lakini hivi sasa jukumu hilo limepelekwa katika ngazi ya vijiji na wilaya ambapo wananchi wanashiriki moja kwa moja katika utunzaji wa rasilimali husika.

“Serikali kuu inachokifanya ni kusimamia sera na miongozo ya maliasili ikiwa ni pamoja na kulipa fidia pale ambapo wanyama  watakapovamia makazi ya watu na kuleta uhalibifu”, alisema Dkt. Budeba.

Alisema kuwa Serikali itandelea kujenga na kuimarisha miundombinu ili kuwezesha wadau wa maliasili kufanya  kazi katika mazingira mazuri.

Aidha Dkt. Budeba aliviomba vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa jamii ili iweze kuona umuhimu wa kuhifadhi mazingira kwani Serikali peke yake haiwezi ni lazima  kushirikiana na wananchi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Sera na Mipango kutoka wizara ya Maliasili na Utalii Pingu Korongo alisema kuwa sera ya kuwashirikisha wananchi pamoja na wadau mbalimbali wa maliasili itasaidia katika utunzaji wa mazingira.

Alisema kuwa sera ya hiyo ilikuja ili kupunguza malalamiko kutoka kwa wananchi ambayo yalikuwa yanakwenda moja kwa moja Serikalini  jambo wanalolifanya hivi sasa ni kuangalia njia bora zaidi ya  kusimamia na kuona kuwa wadau pamoja na jamii wanafanya kazi vizuri.

Naye Mwenyekiti wa Ulinzi Shirikishi wa Maeneo ya Fukwe na Bahari kutoka wilaya ya Temeke Khatibu Abdala  alisema kuwa hatua zaidi zinatakiwa kuchukuliwa katika utunzaji wa  mazingira .

Abdala alisema kuwa tangu wameanza kushiriki katika zoezi la utunzaji wa mazingira hizi sasa  fukwe za bahari ni  safi na wanafanya kazi hiyo kwa kusimamiwa na Serikali ya mtaa wa Kizito Kimbiji.

Kuhusiana na watu wanaoharibu mazingira alisema kuwa wakiwamakata wanawapeleka katika uongozi wa Serikali ya mtaa ili hatua za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Mkutano huo wa siku mbili unahudhuriwa na wadau mbalimbali wa maendeleo na sekta ya mazingira  kutoka taasisi za Serikali na binafsi.


No comments:

Post a Comment