Meneja wa Baraza la Habari Tanzania Ofisi ya Zanzibar (MCT), Suleiman Seif akiuliza maswali kwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Maalim Seif Shariff Hamad, alipokutana na Waandishi wa Habari kuzungumzia masuala ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Saba pamoja na mambo mengine yanayohusu Zanzibar, katika Hoteli ya Grand Palace Malindi mjini Zanzibar leo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamadi akifafanua jambo wakati alipokutana na Waandishi wa Habari kuzungumzia masuala ya utendaji wa Serikali ya Awamu ya Saba pamoja na mambo mengine yanayohusu Zanzibar, katika Hoteli ya Grand Palace Malindi mjini Zanzibar leo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamadi (wakatikati)akiwa katika Picha ya pamoja na Mawaziri na watendaji wa Sekta mbalimbali hukokatika Hoteli ya Grand Palace Malindi Zanzibar. (Picha zote na Yussuf Simai- Maelezo Zanzibar)
Na Fakih Haji, Maelezo Zanzibar
6/10/2012
6/10/2012
MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka wananchi kuacha tabia ya kufanya vurugu kwa lengo la kuvunja amani na utilivu Zanzibar.
Amesema bado liko kundi la watu ambao wanazembea hatua ya amani na utulivu uliopo Zanzibar na kujaribu kutaka kuleta machafuko katika nchi.
Maalim Seif ameyaeleza hayo leo, huko Hoteli ya Grand Palace iliyoko Malindi mjini Zanzibar wakati akizungumza na waandishi wa Habari.
Amesema, Serikali iliopo sio kama haiwezi kuchukuwa hatua kali bali inafanyakazi kwa utaratibu maalum ili kuepuka utumiaji wa nguvu.
Ameongeza kuwa pindi Serikali ikichukuwa hatuwa kali watu wataanza kupiga kelele na kusema kuwa wanaonewa na zinakiukwa haki za kibinaadamu.
Hivyo, aliwaonya wenye tabia hiyo kuacha mara moja tabia hiyo ya kuleta vurugu na fujo kwani hali ikiwa mbaya hakuna mtu atakaefaidika na kitu.
Maalim Seif ambaye ni Makamo wa Rais wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, alisema wapo baadhi ya watu ambao hudhani pakiwa na fujo na ghasia wanafaidika, jambo hilo sio kweli kwani kukitokea vurugu na Serikali kuchukuwa hatua kali hakuna atakaefaidika bali itakuwa hasara kwa wananchi.
Hivyo, aliwasihi wananchi kuacha tabia hiyo na kuendelea kudumisha Amani na Utulivu ambao ni jambo la kujivunia.
Makamo wa Kwanza wa Rais wa Serikali ya Zanzibar alitoa mfano wa nchi zenye mizozo na kusema hakuna maendeleo yanayopatikana na watu wanaishi katika hofu na wasiwasi.
Akizungumzia suala la uchumi wa Zanzibar, MaalimSeif amesema uchumi wa Zanzibar unakuwa kwa kiasi, kwani mwaka 2011, ukuwaji wa uchumi ulikuwa ni 6.8 na unatarajia kuongezeka mwaka 2012/2013 na unatarajia kufikia asilimia 7.5 wakati pato la Mzanzibari linakuwa kutoka Tshs. 782,000 kwa mwaka hadi kufikia Tshs. 960,000 ambazo ni sawa na Dolla za Kimarekani 615 kutoka 560 mwaka 2010.
Ameongeza kuwa lengo la Serikaliya Mapinduzi Zanzibar ni kufikia lengo la Melenium ambapo nchi zote zinatakiwa ifikapo mwaka 2015 pato la Wananchi wake liwe TSHS 884,000 sambamba na kuonekana fedha mifukoni na sio kwenye makaratasi.
Kuhusu matumizi ya fedha za Serikali, Maalim Seif alisema bado Serikali inakabiliana na changamoto kubwa juu ya matumizi ovyo ya fedha za Serikali.
Amesema Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya mwaka 2010/2011 imeonyesha bado wako baadhi ya Watendaji hujinufaisha kupitia fedha za Serikali jambo ambalo sio zuri na halikubaliki.
Amesema ,tatizo la matumizi yasiofuata taratibu linaendelea kujitokeza. Pia udhaifu wa kukosekana baadhi ya vielelezo muhimu katika ukusanyaji na matumizi ya Mapato limeonekana kujitokeza katika Taasisi mbali mbali za Serikali , kutokana na uchunguzi uliofanywa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.
Aidha Maalim Seif alisema kuwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amebaini kuwa kuna matatizo kwa baadhi ya Taasisi za Serikali kutokusanya mapato ipasavyo pamoja na kutumia fedha bila kufuata taratibu za Kisheria za fedha na malengo waliojipangia wenyewe Taasisi hizo.
Amesema kuwa ipo Miradi mingi imepewa fedha nyingi katika utekelezeaji wake lakini kazi iliotendeka hailingani na fedha zilizotolewa.
Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amesema kuwa, Serikali haitovumilia kuona baadhi ya Watendaji wanaendelea kukiuka sheria ziliopo za fedha na kuchukuwa fedha za Wananchi kujinufaisha binafsi.
No comments:
Post a Comment