TANGAZO


Saturday, October 20, 2012

Kiongozi wa UAMSHO Zanzibar Sheikh Farid Ahmed, arejea nyumbani kwake


Kiongozi wa kundi maarufu Visiwani Zanzibar la Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed.

ZANZIBAR, Tanzania

HATIMAYE Mwanaharakati na Kiongozi wa kundi maarufu Visiwani hapa la Uamsho, Sheikh Farid Hadi Ahmed, aliyedaiwa kutekwa siku tatu zilizopita na kusababisha vurugu kubwa kwa wafuasi wake ameonekana na sasa yupo nyumbani kwake.

Taarifa kutoka vyanzo vya kuaminika vinavyomzunguka Sheikh Farid vimedokeza kuwa, kiongozi huyo kipenzi cha Waislamu visiwani hapa amepatikana akiwa mzima, ingawa haijaelezwa alikuwa wapi na alifanywa nini akiwa huko mafichoni kwa siku tatu.

Habari zaidi zinadai kuwa, baada ya kuonekana aliporejea nyumbani usiku wa kuamkia leo, wafuasi wake waliendesha Dua Maalum ya kushukuru kupatikana kwake akiwa mzima, lakini pia kumuombea kheri kwa Mungu.

Kupotea kwa Sheikh Farid kumesababisha vurugu kubwa huko visiwani Zanzibar kutoka kwa wafuasi wa kundi la Uamsho kuchoma makanisa na Ofisi za Chama cha Mapinduzi ikiwa ni pamoja na kutishia kuwadhuru viongozi wa dini ya Kikristo.

Aidha, habari zisizoaminika zimedokeza kuwa, ni kweli Sheikh Farid alitekwa na watu wasiojulikana na kufichwa katika ‘mashimo maalum’ huku akipewa adhabu kadhaa huku akiulizwa maswali ya hapa na pale kuhusu harakati zake.

Hakuna taarifa rasmi kutoka kwake, wala kiongozi yeyote wa Uamsho ama wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, inayozungumzia kupatikana kwake, ingawa mitandao mbalimbali ya kijamii imeonesha picha zake akiwa nyumbani kwake na familia na waumini wengine waliomtembelea.

Wafuasi wa Sheikh Farid walikuwa wakiituhumu Serikali kumteka kiongozi wao, jambo ambalo serikali ililikana na kusema haitambui alipo Sheikh huyo na kwamba haihusiki na utekaji wake, tamko lililozua ghasia na kusababisha askari mmoja kucharangwa mapanga na kuuawa.

Tutaendelea kuwaletea taarifa zaidi kwa kadri tutakavyokuwa tunazipata kutoka kwa bvyanzo vyetu visiwani Zanzibar kuhuisiana na Sheikh Farid.

No comments:

Post a Comment