Bondia Karama Nyilawila, akiwa chini baada ya kupigwa kwa KO na Francis Cheka katika pambano la Ubingwa la WBO.
Mwamuzi wa pambano la Ubingwa wa WBO, Jerome Waruza kutoka Malawi, akimuhesabia bondia Karama Nyilawila baada ya kupigwa kwa KO katika raundi ya sita na Francis Cheka katika pambano lililofanyika kwenye Ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam, usiku wa kuamkia leo.
Mwamuzi wa pambano la Ubingwa wa WBO, Jerome Waruza kutoka Malawi akimuhesabia bondia Karama Nyilawila baada ya kupigwa kwa KO katika raundi ya sita na Francis Cheka katika pambano lililofanyika kwenye Ukumbi wa PTA, jijini Dar es Salaam
Bondia Karama Nyilawila akikwepa konde la bondia Francis Cheka
Mwamuzi Jerome Waruza (kulia) kutoka Malawi akimtangaza bondia Francis Cheka kuwa mshindi katika pambano hilo.
Bondia Karama Nyilawila (kushoto), akimtupia makonde Francis Cheka
Bondia Francis Cheka baada ya kutangazwa mshindi katika pambano hilo.
| Francis Cheka akitangazwa kuwa mshindi wa pambano hilo. |
Mdau wa michezo akimpongeza Francis Cheka. Kulia mlezi wa ngumi za kulipwa ambaye alikuwa mgeni rasmi katika pambano hilo, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova akivisha mkanda wa Ubingwa wa WBO, bondia Francis Cheka. Kushoto ni Rais wa PST, Emmanuel Mlundwa.
DAR ES SALAAM, Tanzania
Pambano hilo la uzani wa ‘Supermidle’ lililochezeshwa na mwamuzi Jerome Waruza wa Malawi kwenye Ukumbi wa PTA, wilayani Temeke, lilianza kwa Nyilawila kuonesha uhatari uliobashiriwa kumpa ushindi, huku akimlazimisha Cheka ‘SMG’ kulalia kamba ya ulingo mara kwa mra akikwepa makonde yake.
Kwa raundi nne za kwanza Nyilawila alikuwa moto na kutabiriwa angeweza kuhitimisha ubabe wa Cheka kwa mabondia wa Tanzania, kabla ya mambo kuja kubadilika katika raundi ya tano mwishoni na sita, ambazo Cheka alianza kubadili sura ya mchezo akishambulia mfululizo.
Katika raundi ya sita ya pambano hilo, lililokuwa na vipindi vifupi vya mabondia hao kushikana na kukumbatiana mchezoni, Cheka alimchapa Nyilawila kwa ngumi tatu nzito mfululizo na kumdondosha chini, ambapo mwamuzi Waruza alimhesabia na kukiri kushindwa kwake kuendelea na mpambano.
Mamia ya mashabiki waliofurika ukumbini hapo, walilipuka kwa shangwe baada ya mwamuzi kumaliza pambano hilo, huku Cheka mwenyewe akikimbia huku na kule ulingoni, kutambia ushindi huo, mbele ya aliyekuwa Mgeni Rasmi, Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Kova ambaye pia ni Mlezi wa Ngumi za Kulipwa nchini, alimvika Cheka mkanda wa ubingwa wa WBO, huku akisema anajivunia hatua aliyopiga kama mlezi ya kuutafutia mchezo wa ngumi wadhamini, ambapo alimtambulisha raia mmoja wa kigeni kuwa mmoja wa wadhamini hao.
Kabla ya Cheka na Nyilawila kupanda ulingoni, kulikuwa na mapambano kadhaa ya utangulizi, Said Mbelwa alimpiga kwa pointi Dickson Mwakipesile, Juma Kihiyo akipoteza pia kwa pointi dhidi ya Ibrahim Mahokola.
Mdogo wake Cheka, aitwaye Cosmas Cheka alifanikiwa kuibuka na ushindi wa pointi dhidi ya Fadhil Awadh, katika mfululizo huo wa mapambano ya utangulizi, huku Shaaban Kilumbelumbe akimpiga kwa pointi Anthony Mathias.
Katika mapambano hayo ya utangulizi, pambano pekee lililotoa mshindi kwa KO lilikuwa ni lile lililowakutanisha Safari Mbiyu, aliyemchakaza Khalfan Jumanne, katika raundi ya kwanza. Stan Kessy na Seba Temba, walitoka sare, huku Hassani Kidebe akichapwa na Deo Samwel kwa pointi.

No comments:
Post a Comment