TANGAZO


Monday, August 13, 2012

Rais Shein aagana na Balozi wa Korea, akutana na wa Denmark nchini,

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Kim Young  Hoon, alipofika kumuaga Rais, katika ukumbi wa Ikulu mjini Zanzibar leo. (Picha zote na Ramadhan Othman, Ikulu)


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Kim Young Hoon, alipofika kumuaga Rais, katika ukumbi wa  Ikulu mjini Zanzibar leo.



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akiagana na Balozi wa Korea nchini Tanzania, Kim Young Hoon, alipofika kumuaga Rais,  Ikulu mjini Zanzibar leo.



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akisalimiana na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Johnny Flento, alipofika  Ikulu mjini Zanzibar leo, kwa mazungumzo na Rais.




Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza na Balozi wa Denmark  nchini Tanzania, Johnny Flento, alipofika  Ikulu mjini Zanzibar leo, kwa mazungumzo na Rais.



Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, akifuatana na Balozi wa Denmark nchini Tanzania, Johnny Flento, alipofika Ikulu mjini Zanzibar leo, baada ya mazungumzo yao.


Rais Shein azungumza na Balozi wa Korea, Denmark nchini, mjini Zanzibar leo

Na Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
13.8.2012                                                                                           

JAMHURI ya Korea imeahidi kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta za maendeleo ikiwemo kilimo cha umwagiliaji maji.
Balozi wa Korea  nchini Tanzania, Mhe. Kim Young  Hoon, aliyasema hayo leo, wakati alipofika Ikulu mjini Zanzibar kwa ajili ya kuaga baada ya kumaliza muda wake wa kazi hapa nchini.
Katika mazungumzo yake, Balozi Hoon alimueleza Dk. Shein kuwa Korea tayari imeshaweka mikakati maalum katika kuongeza juhudi zake kwenye sekta ya kilimo hasa kilimo cha mpunga wa kumwagilia maji hapa Zanzibar.
Balozi Hoon alisema kuwa uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu uliopo kati ya Zanzibar na Korea hasa katika kuimarisha miradi ya maendeleo umesaidia katika kufikia hatua kubwa za kimaendeleo hapa nchini ambapo aliahidi kuendelezwa na nchi yake.
Alisema kuwa ana matumaini makubwa kuwa kilimo cha umwagiliaji maji kinaweza kusaidia kwa kiasi kikubwa katika maendeleo ya kilimo hapa Zanzibar.
Aidha, Balozi huyo alimueleza Dk. Shein kuwa mbali ya juhudi za makusudi zinazochukuliwa na Korea katika sekta ya kilimo hasa cha umwagiliaji maji pia, hatua maalum zimeshaanza kuchukuliwa katika mradi mkubwa wa kilimo hicho utakaoanza hapo mwakani.
Balozi Hoon pia, alieleza kuwa mbali ya mashirikiano yaliopo katika sekta ya kilimo ambapo nchi hiyo imekuwa ikiiunga mkono Zanzibar kwa kiasi kikubwa pia, Korea imeweza kuiunga mkono Zanzibar katika sekta ya elimu.
Balozi huyo alieleza kuwa Korea imekuwa na mashirikiano mazuri na Zanzibar katika kuimarisha Taasisi zisizokuwa za Kiserikali(NGOs) ambapo baadhi yake zimekuwa zikipata misaada kadhaa kutoka nchini hiyo kwa ajili ya kuendeleza maendeleo ya wananchi wa Zanzibar.
Pamoja na hayo, Balozi huyo aliupongeza uongozi wa Dk. Shein sanjari na juhudi anazozichukua katika uongozi wake huku akiahidi kuendelea kuwa balozi wa kuitangaza Zanzibar kiutalii kutokana na vivutio vyake kadhaa viliopo.
Balozi huyo pia, alimueleza Dk. Shein kuwa mbali ya mashirikiano katika sekta hizo pia, kumekuwa na mshirikaino mazuri kati ya Kotea na Tanzania ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa kampuni za nchi hiyo ambazo zinafanyakazi hapa Tanzania.
Katika mazungumzo hayo pia, Balozi huyo ametoa mkono wa pole kwa Rais wa Zanzibar pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kufuatia ajali ya kuzama kwa meli ya MV Skagit hivi karibuni.
Naye Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Kohamed Shein, alimueleza Balozi huyo kuwa Zanzibar inathamini uhusiano na ushirikiano mwema kati yake na nchi hiyo ikiwa ni pamoja na mashirikiano mazuri juu ya sekta za maedeleo ikiwemo kilimo.
Dk. Shein alieleza kuwa kutokana na Korea kupata mafanikio makubwa katika kuimarisha sekta ya kilimo cha umwagiliaji maji hatua ya kuiunga mkono Zanzibar kwenda kwenye kilimo hicho itasaidia.
Katika mazungumzo hayo, Dk. Shein alitoa pongezi kwa Balozi huyo kwa kuwahamasisha watalii pamoja na Kampuni kadhaa kutoka nchini kwake na kuja Tanzania wakiwemo watalii ambao huja kutembelea Zanzibar.
Kutokana na mashirikiano pamoja na uhusiano mzuri uliopo kati ya Korea na Zanzibar, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa ipo haja ya kuimarisha zaidi hatua hizo hasa katika kuimarisha sekta ya kilimo, kikiwemo cha umwagiliaji maji, elimu hasa katika sekta hiyo na nyenginezo, utafiti na sekta nyenginezo.
Akieleza miongoni mwa hatua zinazoendelea kuchukuliwa na Serikali ya Mapindyuzi Zanzibar katika kuhakikisha suala la usafiri wa baharini linapatiwa ufumbuzi, Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Serikali imeamua kwa makusudi kununua meli kwa ajili ya kuwasaidia wananchi katika sekta hiyo ya usafiri.
Wakati huo huo, Dk. Shein alifanya mazungumzo na Balozi wa  Denmark nchini Tanzania Mhe. Johnny Flento ambapo katika mazungumzo yao viongozi hao walieleza umuhimu wa  kuendeleza uhusiano na ushirikiano katika kuimarisha sekta za maendeleo hapa Zanzibar.
Dk. Shein alimueleza Balozi huyo kuwa Denmark imekuwa na mashirikiano na Zanzibar kwa muda mrefu na kuweza kuiunga mkono katika kuimaarisha sekta mbali mbali zikiwemo afya, elimu na nyenginezo.
Viongozi hao pia, walizungumza juu ya ajali ya kuzama kwa meli ya MV Skagit ambapo Balozi Flento alitoa mkono wa pole kwa Rais pamoja na wananchi wa Zanzibar huku akieleza kuwa ataendelea kuwashajiisha wananchi wa nchi yake kuendelea kuja kuitembelea Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo Dk. Shein pia, alimuhakikishia Balozi huyo kuwa Zanzibar ni salama hatua ambayo inatokana na juhudi za kuimarisha amani na utulivu hali ambayo imeipa sifa na mafanikio makubwa Zanzibar ndani na nje ya nchi.
Pamoja na hayo, Dk. Shein alimpongeza Balozi huyo kwa juhudi zake za makusudi za kuja Zanzibar hapo kabla kwa ajili ya kujifunza lugha ya kiswahili hatua ambayo itasaidia kwa kiasi kikubwa katika kazi zake sanjari na mawasiliano kwa ujumla wakati akiwepo hapa nchini.



No comments:

Post a Comment