TANGAZO


Saturday, July 14, 2012

Yanga yakubali kipigo Kombe la Kagame

Kikosi cha Yanga kilichopambana na timu ya Atletico ya Burundi na kukubali kichapo cha mabao 2-0, Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam leo.


Na mwandishi wetu
MABINGWA watetezi wa michuano ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (Kombe la Kagame) Yanga imeanza vibaya harakati zake za kutetea ubingwa huo baada ya kukubali kipigo cha mabao 2-0 kutoka kwa Atletico ya Burundi katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja taifa Dar es Salaam leo jioni.
Atletico tangu kipindi cha kwanza walionekana wazi kutaka ushindi wa mapema baada ya washambuliaji wake kuonesha uchu wa kupachika mabao ya mapema japo mabeki wa Yanga walionekana kuwa imara katika kipindi hicho.
Wakati dakika za kipindi cha kwanza zikizidi kuyoyoma, Yanga ambao walijaza viungo wengi katikati wakiongozwa na Haruna Niyonzima, walicharuka na kuliandama lango la wapinzani lakini walinzi wa Atletico walikuwa makini kuondosha hatari zilizokuwa zikielekezwa.
Kutokana na kujitokeza kwa kosa kosa nyingi katika kipindi hicho ilifanya dakika 45 kumalizika huku timu zote zikienda mapumziko zikiwa hazifungana hali iliyofanya kipindi cha pili kila upande kufanya mabadiliko ambayo yalisaidia kubadilisha matokeo.
Baada ya mabadiliko ya wachezaji kufanyika katika kipindi cha pili, Atletico walianza kutandaza kandanda safi wakiongozwa na mshambuliaji wao wa kushoto Didie Kavumbagu ambaye alikuwa mwiba wakati wote wa mchezo.
Katika kudhihirisha kuwa wanahitaji kufanya vizuri katika mashindano huku wakishangiliwa na mashabiki wanaoaminika kuwa ni wa Simba, Atletico waliandika bao la kwanza dakika ya 81 likifungwa na Kavumbagu baada ya Christopher Ndashiaye kufanya kazi ya ziada na kupiga mgongeo uliomkuta mfungaji.
Baada ya bao hilo kuingia huku vijana wa Yanga wanaonolewa na Tom Saintfiet raia wa Ubelgiji walijaribu kupanga mashambulizi ili kurudisha bao hilo, lakini Kavambagu wa Atletico dakika ya 90 ya mchezo huo alizamisha jahazi la wapinzani wao alipopiga shuti la mbali lilimshinda mlinda mlango Yaw Berko na kutinga wavuni.
Mabao hayo mawili yalitosha kumaliza dakika 90 za mchezo huo kwa Atletico kuondoka na ushindi katika uwanja huo wa Taifa Dar es Salaam na kufanya kuwa mwanzo mbaya kwa kocha Tom Saintfiet, ambaye leo klabu yake inafanya uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizoachwa wazi na viongozi waliojiuzulu akiwemo aliyekuwa Mwenyekiti Lloyd Nchunga.
Mlinda mlango wa Yanga , Berko anastahili pongezi kubwa baada ya kupangua michomo mikali ya washambuliaji wa Atletico wakiongozwa na Hassani Dimana, Piere Kwizera, Henri Mbazumutima na beki wao wa kati anayepanda Francis Nongwe.
Pia Berko katika kipindi cha kwanza alionekana kuvaa jezi inayotumiwa na timu ya taifa yake ya Ghana iliyokuwa na nembo ya Puma lakini kipindi cha pili alibadilisha na kuvaa jezi inayotumiwa kwenye mashindano hayo.
Katika mchezo wa kwanza wa kundi C, uliopigwa kwenye uwanja huo APR ya Rwanda iliiadhibu El Salaam ya Sudani kwa mabao 7-0.
Leo kutakuwa na michezo mitatu, kundi B timu ya Azam itashuka dimbani kumenyana na Mafunzo ya Zanzibar kwenye Uwanja wa Chamazi, Dar es Salaam.
Katika kundi A, Simba itavaana na URA kuanzia saa 10:00 jioni, huku Vital Club ataanza dimbani saa 8:00 mchana kumenyana na Sports kwenye Uwanja wa taifa Dar es Salaam.


  

No comments:

Post a Comment