Macky Sall na Rais Wade kwenda kwa duru ya pili ya uchaguzi

Tume ya uchaguzi nchini Senegal imesema kuwa kutakuwepo na duru ya pili ya uchaguzi wa urais baada ya rais wa sasa Abdoulaye Wade, kushindwa kuzoa kura za kutosha kutangazwa mshindi wa moja kwa moja katika duru ya kwanza.
Bwana Wade alipata asilimia thelathini na tano ya kura zote zilizopigwa katika uchaguzi wa urais uliofanyika siku ya Jumapili. Rais huyo sasa atachuana na aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo wakati wa utawala wake Macky Sall ambaye alipata asilimia ishirini na sita ya kura zote zilizopigwa.
Hata hivyo ameelezea matumaini ya kunyakua tena uongozi wa nchi.
Awali rais Wade alibashiri kupata ushindi mkubwa katika duru ya kwanza ya uchaguzi.
Wadadisi wamesema rais Wade atakuwa na kibarua kigumu katika duru ya pili ikiwa upinzani utaungana dhidi yake.
Mpinzani wake, Macky Sall amesema yuko tayari kukabiliana na rais Wade na kuongeza kuwa upinzani umeshinda viti vingi zaidi vya ubunge.