Wananchi wa Senegal wanapiga kura katika uchaguzi wa rais huku viongozi wa kimataifa wamewaomba wawe watulivu.

Wafuasi wa Rais Abdoulaye Wade
 
Rais Abdoulaye Wade, mwenye umri wa miaka 85, anagombea muhula wa tatu ingawa katiba inaruhusu mihula miwili tu.
Uamuzi wake huo umezusha maandamano kwa majuma kadha.
Ili kuzimua hasira, mjumbe wa Umoja wa Afrika, rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, amependekeza kuwa, hata Bwana Wade akichaguliwa, basi ajiuzulu baada ya miaka miwili, badala ya kuongoza kwa muhula mzima wa miaka 7.
Bwana Obasanjo alisema, Bwana Wade ameshasema kwamba akichaguliwa, hatabaki madarakani kwa muhula mzima.
Bwana Obasanjo alisema, uhasama unahitaji kumalizwa haraka:
"Hisia za kutoaminiana kati ya upinzani na serikali haifai kubaki kwa muda mrefu"
"Yeyote yule atayeshinda uchaguzi, atahitaji kushinda na amani piya, na usalama, na kuileta nchi pamoja ili kupata maendeleo nchini humu"
Katika mkutano na waandishi wa habari, Bwana Obasanjo alipigiwa kilele na upinzani wakimwambia "usiichome nchi yetu kama
inavotokea nchini mwako".