Rais wa Sudan Hassan Omar el Bashir anatarajiwa kuzindua mamlaka mpya leo Jumatano, itakayosimamia utekelezwaji wa mapendekezo yanayolenga kuleta amani ya kudumu katika jimbo la Darfur linalokabiliwa na mzozo magharibi mwa taifa hilo.
Mamlaka hiyo inatarajiwa kutekeleza makubaliano ya amani ambayo yatatoa mamlaka pamoja na ugavi wa rasilmali. Pia itatarajiwa kuwarejesha nyumbani watu waliokimbia ghasia pamoja na kuwafidia waathirika.
Jukumu jingine la taasisi hiyo ni kuhakikisha haki na usalama wa raia wa Darfur.
Hata hivyo makubaliano hayo ya Doha yalitiwa saini na kundi moja lijulikanalo kama Liberty and Justice Movement -huku makundi mengine matatu yenye ushawishi yakikataa kutia saini.
Wakosoaji wanaamini kuwa makubaliano hayo yana dosari nyingi ambayo yalishuhudiwa pia kwenye makubaliano mengine ya amani yaliotiwa saini mwaka wa 2006 mjini Abuja.
Minni Minnawi ambaye aliongoza kundi la waasi na kutia saini makubaliano ya Abuja alirejea tena uasi. Mapigano yamepunguka sana tangu mwaka wa 2006 lakini bado hali ya usalama ni mbaya.
Kundi lenye ushawishi mkubwa la Justice and Equality Movement tayari limegawanyika tangu kiongozi wake Khalil Ibrahim kuuawa mwezi wa Disemba.
Umoja wa Mataifa unakadiria kuwa zaidi ya watu 300,000 wamekufa katika kipindi cha karibu miaka kumi wakati machafuko kwenye eneo la Darfur yalianza ingawaje serikali inasema ni watu elfu kumi pekee wamefariki.