TANGAZO


Tuesday, February 28, 2012

Fedha za Wahanga wa Mv Spice Islander kuanza kugawiwa


Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Zanzibar, Balozi Seif Ali Idd

Na Khadija Khamis/Maelezo Zanzibar   
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeamua kuanza kuchukua hatua ya kuzigawa fedha za maafa zilizokusanywa kupitia michango mbali mbali kutoka mashirika, makampuni na watu binafsi kwa ajili ya watu waliopatwa na ajali ya kuzama meli ya MV Spice Islander Septemba 10, mwaka jana.
 Fedha hizo zinatarajiwa kuanza kugawiwa mara tu baada ya kukamilika utaratibu wa uhakiki ili kujua wahusika halisi wanaopaswa kulipwa kutokana na ajali hiyo.
 Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya  Ocean View Kilimani, Makamu wa pili wa Rais Balozi Seif Ali Iddi alisema jumla ya shilingi bilioni moja, milioni miambili na thalathini laki mbili na elfu tatu mia nane na siti na moja zilikusanywa na kuhifadhiwa katika akaunti maalum ya Zanzibar Disaster Fund katika Benki ya watu wa Zanzibar na fedha zote ziko salama.
 Akizungumzia zao la karafuu, Balozi Seif alisema serikali itaendelea kuliimarisha zao hilo kwa vile ni zao pekee linalosafirishwa kwa wingi nchi za nje na kuwa bado linaendelea kuwa ni uti wa mgongo wa uchumi wa Zanzibar.
Amesema mavuno ya zao la karafuu msimu uliopita limevuka kiwango kilichokadiriwa cha tani elfu tatu na kufikia tani elfu nne mia saba ambapo kiasi cha tani alfu nne tayari zimeshauzwa na kuipatia serikali dola za kimarekani arubaini na tano milioni.
 Alisema serikali inaendelea na juhudi za kuendeleza kilimo chenye tija ili kuliwezesha taifa kuwa na uhakika wa upatikanaji wa chakula kwa kuwapatia wakulima miche, mbegu bora na dawa za kuulia wadudu waharibifu wa mimea.
 Amesema kiasi ya wakulima 296 wamepatiwa mafunzo ya mpunga wa umwagiliaji katika mabonde mbali mbali Unguja na Pemba na sasa wanauwezo wa kuzalisha mpunga kati ya tani nne hadi sita kwa hekta.
 Kuhusu mfumko wa bei kwa bidhaa mbali mbali, makamu wa pili wa Rais amesema tatizo hilo linasababishwa na uagiziaji mkubwa wa bidhaa za chakula hasa mchele, sukari na unga wa ngano ambapo bei zake zimekuwa zikipanda mara kwa mara katika soko la dunia, kuongezeka gharama za usafirishaji, kupanda kwa bei ya mafuta na kushuka thamani kwa sarafu ya Tanzania.
 Kuhusu mchakato wa katiba mpya ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, amewataka wananchi wa Zanzibar kujitokeza kwa wingi katika vikao vya kukusanya maoni ya wananchi ili kuhakikisha kuwa inapatikana katiba ambayo inazingatia maslahi ya wananchi wa visiwa hivyo.
                         

No comments:

Post a Comment