Kamishna wa Sensa ya
Watu na Makazi Bi. Hajjat Amina Mrisho Said (katikati) akiwa katika picha ya
pamoja na Wadadisi wa Utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi wa mwaka 2014
kwa Kanda ya kasikazini inayojumuisha mikoa ya Tanga, Arusha, Kilimanjaro na
Manyara. Mafunzo ya utafiti huo yanayotarajia kumalizika kesho jijini Tanga. (Picha
zote na Veronica Kazimoto - Tanga)
Na Veronica Kazimoto na
Aron Msigwa – Tanga.
OFISI ya Taifa ya Takwimu imewataka wadau mbalimbali wakiwemo
viongozi wa Serikali, siasa na waandishi wa habari kutumia takwimu sahihi
zinazotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu pindi wanapotekeleza majukumu yao.
Akizungumza na waaandishi wa habari pamoja na wadadisi wa Madodoso
ya utafiti wa Watu Wenye Uwezo wa Kufanya Kazi mwaka 2014 kutoka kanda ya kaskazini leo
jijini Tanga Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi kutoka Ofisi ya Taifa ya
Takwimu Bi. Hajjat Amina Mrisho Said amesema kuwa ni jukumu la kila
mtendaji katika eneo lake kuhakikisha kuwa anatumia takwimu sahihi
zinazotolewa na Ofisi hiyo.
Amesema Ofisi ya Taifa ya Takwimu ndiyo yenye mamlaka na
dhamana ya utoaji wa takwimu za masuala mbalimbali nchini na kuongeza kuwa
matumizi ya takwimu zisizo sahihi yana athari kwa jamii hasa wakati wa kupanga
mipango ya maendeleo kuanzia ngazi ya vijiji mpaka taifa.
Amesema kuwa takwimu sahihi huwezesha utekelezaji wa mipango ya
maendeleo na kuongeza kuwa zipo changamoto mbalimbali ambazo ufumbuzi
wake unaweza kupatikana kwa kufanya rejea ya takwimu sahihi kutoka Ofisi ya
Taifa ya Takwimu.
“Takwimu ni muhimu sana katika kupanga namna ya kukabiliana na
matatizo na majanga mbalimbali yanayotokea katika jamii kama mafuriko, njaa,
masuala ya ardhi na elimu ambayo kimsingi yanahitaji matumizi ya takwimu sahihi
ili kujua kiwango halisi cha ukubwa wa tatizo na namna ya kupata suluhisho
la kudumu kwa wananchi husika.
Amesema ni vema wadau wanaotumia takwimu kwenye majukwaa
mbalimbali na waandishi wa habari kujenga tabia ya kuwasiliana na Ofisi ya
Taifa ya Takwimu kabla ya kutoa takwimu walizonazo ili kupata ukweli wa hali
halisi.
“Natoa wito kwa wadau mbalimbali na waandishi wa habari
kuhakikisha kuwa mnapata takwimu sahihi hata kama mmezipata kutoka kwa viongozi,
tafadhali hakikisheni mnapitia mamlaka
husika kupata ukweli wa takwimu hizo ili kuepuka kutoa takwimu zisizo sahihi”, Amesisitiza
Kamishna wa Sensa.
Ametoa wito kwa wadau mbalimbali kutembelea tovuti ya Ofisi ya
Taifa ya Takwimu ikiwa ni moja ya chanzo sahihi cha habari katika masuala yote
yahusuyo takwimu na rejea sahihi na kuongeza kuwa takwimu zote zinazotumika
kutengeneza sera za taifa za mipango ya maendeleo zinatoka katika chanzo kimoja
tu ambacho ni Ofisi ya Taifa ya Takwimu.
Katika hatua nyingine Kamishna wa Sensa ya Watu na Makazi wa Ofisi
ya Taifa ya Takwimu Bi. Hajjat Amina Mrisho Said ametoa wito kwa Maofisa wa
Takwimu walio katika mikoa na wilaya mbalimbali nchini kutumia vikao mbalimbali
vinavyofanyika katika Halmashauri na mikoa kutoa elimu ya matumizi ya takwimu
zilizopo ili waweze kupanga mipango mbalimbali ya maendeleo na kutatua kero
mbalimbali za wananchi.
Amesema takwimu zilizopo lazima zitafsiriwe na jukumu hilo lazima
lifanywe na wawakilishi hao wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu walio katika mikoa
mbalimbali nchini na kuongeza kuwa wataalam hao kwa kushirikiana na viongozi
wengine wa halmashauri wana jukumu la kutoa elimu kwa makundi mbalimbali ya
jamii hasa vijana ili waweze kujiajiri na kutumia fursa zilizopo katika maeneo
yao ili kupunguza utegemezi.
“Naomba mtumie vikao hivyo vya hamashauri kutoa elimu kwa sababu
tayari ninyi mnazo takwimu, vikao vya halmashauri huwa vinahusisha viongozi
mbalimbali wa Serikali na jamii hivyo mnaweza kabisa kushauri na kushawishi kwa
viongozi hao kutumia takwimu sahihi ili kuondoa matatizo mbalimbali likiwemo
tatizo la ajira kwa vijana na kuondoa utegemezi kwa kuwajengengea uwezo vijana
wasio na ajira kujiajiri wenyewe”, amesema Kamishna.
Aidha ametoa wito kwa watafiti na wadadisi wa Madodoso ya Watu Wenye
Uwezo wa Kufanya Kazi 2014
watakaoendesha zoezi la utafiti wa idadi ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi
kutoa elimu kwa vijana ambao hawana kazi katika maeneo yote watakayopita ili
kuwajengea uwezo wa kufanya kazi pia kuwashauri kujiunga na vyuo vya ufundi
Stadi (VETA) vilivyopo katika maeneo mbalimbali nchini ili waweze kujiajiri na
kuondoa wimbi la utegemezi.
No comments:
Post a Comment