Wafuasi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Kata ya Nduli, Jimbo la Iringa mjini, wakiwa wamemnyanyua juu Diwani mteule wa kata hiyo, Bashir Mtove baada ya kutangazwa kuwa mshindi katika uchaguzi mdogo wa kata hiyo, dhidi ya mpinzani wake Ayub Mwenda wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), uliofanyika jana. (Picha na Francis Godwin Blog)
Na Francis Godwin, Iringa
KUFUATIA ushindi wa uchaguzi mdogo wa udiwani Kata zote tatu Mkoa wa Iringa ikiwemo kata ya Nduli jimbo la Iringa mjini, Chama Cha mapinduzi (CCM), Wilaya ya Iringa mjini kimetuma salam kwa Mbunge wa jimbo la Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) kuwa aanze safari ya kufungasha virago katika jimbo hilo, ili 2015 akabidhi jimbo CCM.
Kaimu Katibu wa CCM, Mkoa wa Iringa, Hassan Mtenga ambaye pia ni Kaimu Katibu wa CCM mkoa huo, akikaimu nafasi ya aliyekuwa katibu wa CCM mkoa marehemu Emmanuel Mteming'ombe alisema kuwa ameletwa mkoani Iringa kwa kazi moja pekee ya kuhakikisha mbunge wa jimbo hilo mchungaji Msigwa anaondoka madarakani kwa kukabidhi jimbo hilo kwa CCM mwaka 2015 kama alivyokabidhiwa mwaka 2010 .
Alisema kasoro zilizojitokeza mwaka 2010 kwa CCM asitegemee zitajirudia tena na kuwa wamejifunza vya kutosha na kuwa hata wana Iringa waliotegemea makubwa kutoka kwa mbunge Msigwa wameishia kushuhudia vurugu zisizo na mwisho za Chadema .
Mtenga alitoa kauli hiyo wakati akiwashukuru wana Nduli , Ibumi na Ukumbi kwa kukiwezesha chama cha CCM kuibuka na ushindi wa kishindo na kukionyesha Chadema kuwa mahitaji ya wana Iringa si Helkopta bali ni maendeleo na sera safi na si sera za vurugu na maandamano.
Huku mwenyekiti wa CCM mkoa wa Iringa Jesca Msambatavangu akisema kuwa mwendo huo ambao CCM imeanza nao katika chaguzi hizo ni mwendo ambao kitakwenda nacho hadi katika uchaguzi wa serikali za mitaa na uchaguzi mkuu 2015.
Msambatavangu alisema kuwa wananchi wa mkoa wa Iringa wamepata kukionyesha Chadema kuwa mahitaji yao si Helkopta wala vurugu ambazo Chadema wamekuwa wakizifanya hivyo kushindwa vibaya kwa Chadema ni fundisho kubwa na ushahidi wa kweli kuwa CCM bado itaendelea kubaki madarakani.
Alisema kuwa kitendo cha Chadema kutumia mamilioni ya shilingi kwa kukodisha Helkopta tatu na kupata kata tatu na kuambulia patupu mkoani Iringa ni aibu kubwa ni wazi hata mbunge wao Msigwa wananchi wa jimbo la Iringa mjini wameonyesha kumchoka.
Mkoa Iringa kata tatu ikiwemo ya Nduli, Mjini Iringa na Ukumbi na Ibumu wilayani Kilolo zilishiriki uchaguzi huo ikiwa ni matokeo ya waliokuwa madiwani wake, wote kupitia CCM kwa nyakati tofauti kufariki dunia.
Katika chaguzi hizo Chadema ilionekana kuwekeza nguvu iliyoshereheshwa na viongozi wake wa kitaifa kwa kupitia kampeni ya M4C Operasheni Pamoja Daima kufanya kampeni katika kata hizo.
Katibu Mkuu wa Chadema Dk Wilbroad Slaa na Mwenyekiti wake, Freeman Mbowe walifanya kampeni katika kata hizo kwa kutumia helkopta yao wakiwa na viongozi wengine wa kitaifa wa chama hicho huku wakiwa na matumaini makubwa ya kata hiyo ya Nduli ,Ibumu na Ukumbi kuchukuliwa na Chadema jambo ambalo limekuwa kinyume.
Pamoja na viongozi hao wabunge kupitia chama hicho, Mchungaji Peter Msigwa na yule wa Viti Maalumu Mkoa wa Iringa, Chiku Abwao waligawana majukumu katika kata hizo.
Wakati Mchungaji Msigwa akifanya kampeni katika kata ya Nduli na mara moja moja katika kata hizo zingine, Abwao kwa upande wake alikita zaidi katika kata ya Ibumu na Ukumbi.
Katika kampeni zake kata ya Nduli, Mchungaji Msigwa aliahidi kugawa mbolea kwa wananchi wa kituo cha kupigia kura ambacho Chadema ingeongoza kwa kura ahadi ambayo wananachi wa Nduli wanaisubiri hasa kituo Mitaba ambacho Chadema waliongoza.
Hata hivyo kati ya vituo tisa vya kata hiyo ya Nduli, Chadema ilifanikiwa kuongoza kwa kura katika kituo kimoja tu cha Mibata kwa mgombea wake kupata kura103.
Akitangaza matokeo katika kata ya Nduli, Msimamizi wa Uchaguzi, Simba Nyunza alisema kati ya kura zote zilizopigwa, Mgombea wa CCM, Bashir Mtove alipata kura 810 huku Ayubu Mwenda wa Chadema akiambulia kura 491.
Huko wilayani Kilolo matokeo yaliyothibitishwa na mawakala wa CCM yanaonesha chama hicho kimepata ushindi mkubwa.
Katika kata ya Ibumu, mgombea wa CCM Gift Msumule ameibuka kidedea baada ya kupata kura 1,400 huku mgombea wa Chadema, Juli Mpungula akiambulia kura zaidi ya 400.
Katika kata ya Ukumbi, mgombea wa CCM, Hemed Mbena ameshinda kwa kishindo baada ya kuzoa kura 1479 dhidi ya kura 829 alizopata mgombea wa Chadema, Oscar Ndale.
Huku mbunge Msigwa akikiri chama chake kushindwa katika uchaguzi huo kata ya Nduli kwa madai kuwa polisi imekisaidia chama tawala kushinda katika uchaguzi huo.
Mbunge Msigwa alitoa kauli hiyo katika taarifa yake aliyoitoa kwenye ukrasa wake wa fecabook juzi jioni baada ya matokeo kuonyesha chama chake kimeshindwa Nduli.
No comments:
Post a Comment