TANGAZO


Friday, April 20, 2018

BALOZI SEIF IDDI AZINDUA KITUO CHA UTOTOAJI SAMAKI, AWATAKA WAFUGAJI SAMAKI NA MAZAO MENGINE YA BAHARINI KUBADILIKA NA KUACHANA NA TABIA YA KUFANYAKAZI KWA MAZOEA NA KUWATAKA KUZALISHA MAZAO HAYO KIBIASHARA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akifurahia Mradi wa Ufugaji wa Samaki pamoja na Rais wa Shirika la Kimataifa la Maendeleo la Korea {KOICA} Bibi Mikyung Lee mara baada ya kuzindua Kituo cha utotoaji wa Vifaranga vya Samaki Beit Ras.(Picha zote na Hassan Issa – OMPR – ZNZ)
Waziri wa Kilimo  Mh. Rashid Ali Juma wa Tatu kutoka Kushoto akitoa maelezo kwa Balozi Seif pamoja na wageni wengine ya vyakula vinavyotokana na mazao ya Baharini.  
Balozi Seif akichungulia  kibanda kilichojengwa kwa ajili ya uzalishaji wa majongooo kwenye Kituo cha utotoaji wa Vifaranga vya Samaki Beit Ras.Wataalamu wa Maabara ya Kituo cha utotoaji wa Vifaranga vya Samaki Beit Ras wakimpatia maelezo Balozi Seif na Rais wa KOICA Bibi Mikyung Lee namna ya utafiti na uendeshaji wa miradi ya Mituo hicho.  Mkurugenzi wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa {FAO} anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi na Sera za Kilimo Nchini Tanzania Bwana Emmanuel Barange akitoa salamu kwenye uzinduzi wa Kituo cha utotoaji wa Samaki Beit el Ras.Rais wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo ya Korea {KOICA} Bibi Mikyung Lee akielezea Mikakati ya Shirika lake katika kusaidia harakati za Maendeleo Zanzibar na Tanzania kwa jumla. 
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akizindua rasmi Kituo cha Utotoaji wa Vifaranga vya Samaki {Marine Hatchery} hapo Beit El Ras.

Na Othman Khamis Ame, Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/4/2018.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema wakati umefika kwa Wafugaji wa Samaki na Mazao mengine ya Baharini nchini kubadilika kufanya kazi kwa mazoea ya kupata kitoeo tu, bali wafuge Kibiashara kwa lengo la  kuongeza uzalishaji wa samaki ili kuinua Sekta ya Uvuvi kwa maslahi binafsi, Jamii na Taifa.
Alisema kwa vile Sekta ya Uvuvi Zanzibar hivi sasa huchangia chini ya asilimia 7.2% ya pato la Taifa, pamoja na kuongezeka kwa mahitaji ya mazao hayo kwenye harakati mbali mbali za chakula, ipo haja ya kuimarishwa zaidi Ufugaji wa mazao hayo ya Baharini.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati wa hafla ya ufunguzi wa Kituo cha Utotoaji wa Vifaranga vya Samaki {Marine Hatchery} kilichojengwa pembezoni mwa Kampasi ya SUZA iliyopo Beit - El Ras nje kidogo ya Kaskazini  ya Mji wa Zanzibar.
Alisema Mali asili za Baharini ni tegemeo kubwa kwa Maisha ya Jamii na Taifa kutokana na kugusa sehemu mbali mbali katika utekelezaji wake, akautolea mfano mradi wa ufugaji wa samaki unaoonyesha umuhimu wa pekee katika kusaidia ongezeko la ajira hasa kwa Vijana na Wanawake.
Balozi Seif  alifahamisha kwamba mradi wa kutotoa vifaranga vya samaki na mazo mengine ya Baharini umeanzishwa kwa lengo la kupanua wigo wa shughuli za ufugaji wa samaki ili Wananchi waweze kuwa na sehemu maalum ya kupata vifaranga vya kutosheleza na vyenye ubora unaohitajika.
“ Mataifa mbali mbali Duniani yanayozalisha vifaranga vya Samaki na mazao ya Baharini  kama Japan, mbali ya kuzalisha vifaranga kwa ajili ya kuwapatia wafugaji wao, pia husambaza vifaranga hivyo baharini ili kuongeza upatikanaji wa samaki ”. Alisema Balozi Seif.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliiagiza Wizara ya Kilimo, Mali asili, Mifugo na Uvuvi kuwaandalia mazingira bora Wananchi wa Unguja na Pemba yatakayowawezesha kupata vifaranga hivyo kwa urahisi.
Alisema Takwimu zinaonyesha kuwa Zanzibar hivi sasa ina zaidi ya Vikundi 144 viavyojishughulisha na harakati za ufugaji wa samaki ambapo vikundi vyote hivyo hutegemea vifaranga kutoka nje ya Zanzibar ambavyo havina uhakika wa ubora na upatikanaji wake.
Alieleza kuwa uzinduzi wa Kituo cha Kutotolea Vifaranga vya Samaki na Mazao ya Baharini  cha Beit – El Ras utakuwa ni ufumbuzi wa changamoto iliyopo kwa Wafugaji wa samaki Nchini hasa katika  upatikanaji wa vifaranga kwa uhakika ambapo kwa sasa wataweza kuzalisha samaki kwa wingi na kujiongezea kipato.
Balozi Seif alisisitiza umuhimu wa utunzwaji wa mazingira katika kuendeshwa kwa mradi huo mpya  unaopelekea kupunguza msongamano baina ya wavuvi na wakulima wa zao la Mwani katika maeneo wanaoshirikiana kwenye shughuli zao zinazokaribiana Kimazingira.
Alifahamisha kwamba zaidi ya asilimia 50% ya vyakula vyote vya Baharini {SEAFOOD} vinavyotumiwa Duniani hivi sasa vinatokana na ufugaji, hivyo maeneo ya hifadhi za Bahari ni vyanzo muhimu vya mazalia ya samaki yanayopaswa kupatiwa hifadhi ya msingi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwaomba Wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika uhifadhi wa mazingira ya Bahari kwa faida yao na vizazi vijavyo.
“ Waswahili wanasema kitunze kidumu. Tupige vita kwa nguvu zetu zote suala zima la uvuvi haramu. Uvuvi huo unaangamiza mazalio ya Samaki na unaharibu mazingira”. Alisema Balozi Seif.
Aliwapongeza Wafugaji wa Samaki na Wakulima wa Mwani kwa kuwa mstari wa mbele katika  kushirikiana na Serikali kwenye suala zima la kuendeleza Sekta ya Uvuvi na kusaidia upatikanaji wa virutubisho muhimu mwilini pamoja na kuyalinda mazingira.
Balozi Seif pia alilishukuru Shirika la Misaada ya Maendeleo la Korea {KOICA} pamoja na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa {FAO} kwa kuiunga Mkono Zanzibar katika kuanzisha na kutekeleza Mradi huo muhimu wa utotoaji wa Vifaranga vya Samaki Nchini.
Mapema akitoa Taarifa Katibu Mkuu  Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi Bibi Marya Abdulla Juma alisema Kituo hicho cha utotoaji wa Vifaranga vya Samakini chanza Barani Afrika na cha 10 Duniani.
 Alisema Mradi huu utatoa  fursa  ya ajira ya wafugaji samaki ipatayo 36,312, wachuuzi pamoja na wakulima wa mwani wapatao 2,1123,624 sambamba na Wizara kuendelea kuhamasisha Wananchi kujihusisha na sekta ya Uvuvi.
Bibi Maryam Abdulla Juma alifahamisha kwamba wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo kuwapatia mafunzo ya Ufugaji wa samaki wananchi 39 Nchini China tayari imeshajenga Mabwawa ya kufugia samaki ya utoaji mafunzo Matano unguja na Pemba na kutarajia kujenga mengine Manne.
Alisema Kituo cha utotoaji wa vifaranga vya samaki Beit el ras kinatarajiwa kuzalisha vifaranga 10,000 vya samaki, Kaa 75 pamoja na Majongoo 55 ili baadae kusambaza kwa wafugaji wa mazao hayo ya baharini.
Alisema wakati mazao ya Bahari yanatarajiwa kuongezeka kupitia mradi huo mkubwa Kituo kitakuwa na sehemu ya kukuza vifaranga vitakavyototolewa. Maabara, Chumba cha kuendesha Mafunzo, Ofisi na Bwawa la kuzalisha maji kabla ya kumwagwa.
Alieleza kwamba Ujenzi wa Kituo hicho ulioanza Mnamo Mwezi Julai Mwaka 2017 umefanywa na Kampuni ya Salem Construction LTD chini ya Mshauri Muelekezi Milennium Engineering zote za Zanzibar.
Akitoa salamu Rais wa Shirika la Kimataifa la Misaada ya Maendeleo ya Korea {KOICA} Bibi Mikyung Lee aliipongeza Zanzibar kwa kupunguza ukali wa maisha kutokana na kupiga hatua kubwa za Maendeleo ikiwemo Sekta ya Viwanda.
Bibi Lee alisema KOICA iliyoanza kufanya kazi Nchini Tanzania mnamo Mwaka 2002 imeshawishika na mazingira ya Tanzania na kuamua kuipa kipaumbele katika uendeshaji wa Miradi iliyomo ndani ya Sekta yya Uvuvi.
Alisema hatua hiyo iliyochukuliwa na KOICA imelenga kuimarisha Kilimo endelevukatika kuunga Mkono Azimio la Umoja wa Mataifa la kupambana na janga la njaa Ulimwenguni.
Naye kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kilimo na Chakula la Umoja wa Mataifa {FAO} anayeshughulikia Sekta ya Uvuvi na Sera za Kilimo Nchini Tanzania Bwana Emmanuel Barange alisema Shirika hilo limejipanga kuendelea kutoa mafunzo kwa Wafugaji na Wataalamu Wazalendo wa Zanzibar katika kuona Mradi huo muhimu unasimama na kuendelea kwa mafanikio.
Hata hivyo Bwana Emmanuel alisema Wataalamu wa fani hiyo waliomo vyuo Vikuu na wale waliomaliza mafunzo yao ni vyema wakafanya juhudi za makusudi katika kuupa nguvu mradi huo uliolenga kuwakomboa wananchi walio wengi Visiwani Zanzibar.
Bwana Emmanuel aliwakumbusha na kuwaomba Wananchi wote wa Zanzibar lazima wajivunie uwepo wa Mradi huo Zanzibar ambao ni wa kwanza Barani Afrika na wa Kumi Duniani.
Mradi huo wa Kituo Maalum cha Utotoaji Vifaranga vya Samaki Zanzibar uliogharamiwa na Shirika la Misaada ya Maendeleo la Korea {KOICA}kwa zaidi ya Dola za Kimarekani Milioni 3.2 unasimamiwa na kuendeshwa na Wataalamu wa Shirika la Kimataifa la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa {FAO}.

No comments:

Post a Comment