Waziri Ummy Mwalimu
1.0 UTANGULIZI
AWALIi ya yote namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia uzima na afya njema mpaka kufika na kuiona siku hii ya leo. Kipekee nawashukuru ninyi wanahabari kwa kuhudhuria mkutano huu ambao kupitia kwenu nitapata fursa ya kuongea na wananchi kuhusu Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani kwa mwaka 2018. Siku hii huadhimishwa tarehe 8 Machi ya kila mwaka ambapo Tanzania inaungana na nchi nyingine wanachama wa Umaja wa Mataifa kuadhimisha siku hii muhimu.
2.0 CHIMBUKO LA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Historia ya Siku ya Wanawake Duniani ni ndefu na inaanzia mwanzoni mwa mwaka 1900 nchini Marekani. Wakati huo wanawake waliokuwa wakifanya kazi viwandani waliandamana kupinga hali mbaya ya mazingira ya kazi ikiwemo ujira mdogo, kufanya kazi kwa masaa mengi, ukosefu wa huduma za kijamii na kuwepo kwa vitendo vya unyanyasaji. Serikali ya Marekani ya kipindi hicho ilisikia kilio cha wanawake hao na kukubali kuzingatia masuala yanayohusu hali na ustawi wa wanawake. Hivyo, kwa mara ya kwanza Siku ya Wanawake iliadhimishwa kwa mara ya kwanza mwaka 1911 nchini Marekani yaani miaka 107 iliyopita.
Aidha, mwaka 1945 Umoja wa Mataifa ulipoanzishwa tarehe 8 Machi ilitengwa kuwa siku ya kimataifa ya wanawake Duniani. Uamuzi huo wa Umoja wa Mataifa ulitokana na kukubali kwamba masuala ya haki, maendeleo na usawa wa wanawake yalihitaji msukumo maalumu na wa pekee. Tangu mwaka huo, Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani hufanyika tarehe 8 Machi kila mwaka duniani kote.
3.0 MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE HAPA NCHINI
Tanzania kama zilivyo nchi nyingine za Umoja wa Mataifa imekuwa ikiadhimisha Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi kila mwaka. Kwa mara ya kwanza maadhimisho haya yalifanyika mwaka 1997 na kuanzia mwaka huo hadi mwaka 2005 yalikuwa yakiadhimishwa Kitaifa kwa kila mwaka.
Mwaka 2005 Serikali ikapitisha uamuzi wa kufanya maadhimisho haya Kitaifa kila baada ya miaka mitano katika moja ya mikoa hapa nchini ili kutoa nafasi kwa Serikali, wadau, jamii, vyama vya siasa kupima mafanikio mbalimbali ya shughuli za maendeleo ya wanawake, kubaini changamoto pamoja na kuweka mikakati ya kukabiliana na changamoto hizo. Aidha, iliamuliwa kuwa katika miaka mingine Maadhimisho hayo yafanyike katika ngazi ya mkoa. Kwa mara ya mwisho Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani yalifanyika mwaka 2015 na hivyo Maadhimisho ya mwaka huu yatafanyika katika ngazi ya mkoa.
4.0 LENGO NA UMUHIMU WA MAADHIMISHO YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI
Lengo la kuadhimisha siku ya wanawake duniani ni kutathmini utekelezaji wa afua za kufikia usawa jinsia na uwezeshaji wanawake kiuchumi, kijamii, kisiasa katika kufikia maendeleo jumuishi. Maadhimisho haya pia yanatoa fursa ya kuelimisha jamii kuhusu jitihada mbalimbali zilizofanywa na jamii, Serikali, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi na wadau wa maendeleo katika kumwinua mwanamke wa kitanzania. Aidha, katika kuadhimisha Siku hii wadau wanapata fursa ya kutafakari na kubainisha upungufu uliojitokeza katika utekelezaji na kuzitafutia ufumbuzi changamoto zilizobainishwa.
Aidha, maadhimisho ya siku hii yanasaidia kuhamasisha jamii kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu maendeleo ya wanawake na usawa wa jinsia. Vilevile, katika kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani, wanawake wanapata fursa ya kujenga mshikamano miongoni mwao pamoja na jamii kwa ujumla.
5.0 KAULIMBIU YA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI 2018
Kaulimbiu ya Siku ya Wanawake Duniani ya Kimataifa huandaliwa na Umoja wa Mataifa kila mwaka. Kutokana na Kaulimbiu ya Siku ya Wanawake Duniani Kimataifa, kila nchi huitohoa Kaulimbiu yake kwa kuzingatia muktadha na mazingira ya nchi husika. Kwa mwaka 2018,
Kaulimbiu ya Kimataifa ya Siku ya Wanawake ni “Press for Progress for Gender Equality” ikimaanisha chochea maendeleo ya jinsia na Kaulimbiu ya kipaumbele ya Mkutano wa 62 wa Umoja wa Mataifa kuhusu Hali ya Wanawake Duniani ni “Challenges and opportunities for achieving gender equality and empowerment of rural women and girls” ikimaanisha changamoto na fursa za kufikia usawa wa jinsia na uwezeshaji wa wanawake na wasichana wanaoishi vijijini.
Katika muktadha wa Tanzania, Kaulimbiu ya mwaka 2018 ni “Kuelekea Uchumi wa Viwanda: Tuimarishe Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji Wanawake Vijijini.” Kaulimbiu hii inaendana na nia ya dhati ya Serikali ya Awamu ya Tano ya kujenga Tanzania ya Viwanda na uchumi jumuishi.
Aidha, inatoa msukumo wa kuhakikisha kuwa wanawake walioko vijijini hawaachwi nyuma katika kujenga na kunufaika na uchumi wa viwanda. Kaulimbiu pia inaweka msisitizo kwamba jukumu la kuwezesha kufikiwa kwa usawa wa jinsia ni letu sote yaani Serikali, Asasi za Kiraia, Sekta Binafsi, Wadau wa Maendeleo, jamii na mtu mmoja mmoja. Vilevile, kupitia Kaulimbiu hii, Maadhimisho ya mwaka huu yanahamasisha jamii kuongeza fursa za kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni kwa ajili ya wanawake wanaoishi vijijini ili washiriki na kunufaika na uchumi has katika kipindi hiki ambapo taifa letu linaelekea katika uchumi wa kati wa viwanda.
Kimsingi, kaulimbiu inatoa msisitizo kwa Serikali na Wadau wa ngazi zote kuendelea kuweka vipaumbele vya kuwainua wanawake wa vijijini ili waweze kuwa wajasiriamali wenye bidhaa bora, na kuwawezesha kupata masoko ya Kimataifa kwa lengo la kuitangaza nchi yetu pamoja na kuinua uchumi wa Taifa letu.
6.0 HALI YA WANAWAKE NA JITIHADA ZA KUFIKIA USAWA WA KIJINSIA NA UWEZESHAJI WANAWAKE VIJIJINI
kwa mujibu wa Taarifa ya Ofisi ya Takwimu hapa nchini inakadiriwa kuwa mwaka 2017 idadi ya wanawake ilikuwa ni 26, 425,396 sawa na asilimia 51.2 ikilinganishwa na wanaume 25, 101,967 sawa asilimia 48.8 ya Watanzania 51, 557,363. Aidha, Asilimia 70.3 ya watanzania wanaishi vijijini ikilinganishwa na asilimia 26.7 ya watanzania wanaoishi mijini. Kati ya Watanzania wanaoishi vijijini wanawake ni asilimia 51.1 ikilinganishwa na wanaume ambao ni asilimia 48.9.
Aidha, asilimia 53.3 ya nguvu kazi katika kilimo ni wanawake ambao kwa sehemu kubwa wanachangia kulisha taifa letu. Hivyo, kwa kuzingatia kaulimbiu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake mwaka huu pamoja na azma ya nchi yetu ya kujenga uchumi wa viwanda na maendeleo jumuishi, natumia fursa hii kuihamasisha na kuihimiza jamii ya Watanzania kokote walipo kutambua na kuthamini mchango wa wanawake wa vijijini pamoja na kuwawezesha kushiriki na kunufaika na uchumi wa viwanda.
Serikali kwa kutambua umuhimu wa masuala ya jinsia na uwezeshaji wanawake ikiwemo wanawake wa vijijini imeridhia na kutekeleza mikataba na Itifaki ya kimataifa na kikanda kuhusu usawa jinsia na uwezeshaji wanawake. Mikataba na Itifika hizo ni pamoja na: Mkataba wa Kimataifa wa Kuondoa Aina Zote za Ubaguzi Dhidi ya Wanawake wa mwaka 1979 ambao unaweka mkazo katika kutokomeza aina zote za ubaguzi dhidi ya wanawake na wasichana; na Itifaki ya Jinsia na Maendeleo ya Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika ya mwaka 1995, ambayo inaweka mkazo katika kufikia asilimia 50 ya uwakilishi wa wanawake katika nafasi za uongozi na maamuzi katika nyanja zote. Aidha, nyongeza ya Itifaki hiyo ya mwaka 1998 isisitiza katika kuzuia Ukatili wa Jinsia.
Tanzania pia inatekeleza Malengo ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (2030) ambapo lengo la 5 linasisitiza katika usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake. Katika utekelezaji wa malengo hayo tunasisitizwa kuhakikisha kuwa hakuna mtu anayeachwa nyuma ikiwemo wanawake wa vijijini. Pamoja na utekelezaji wa malengo hayo, vilevile nchi yetu inazingatia Agenda ya Maendeleo ya Afrika 2063 kuhusu Afrika Tuitakayo ambayo inazitaka nchi za Afrika kuzingatia usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake kwa maendeleo jumuishi.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Dkt John Pombe Magufuli imeendelea kuweka mazingira wezeshi kwa ajili ya kufikiwa kwa usawa jinsia, uwezeshaji wa wanawake ikiwemo kwa wanawake wa vijijini kwa ajili ya kuleta maendeleo jumuishi. Kutokana na jitihada hizo za Serikali na wadau wengine, Jukwaa la Uchumi Duniani katika Taarifa yake ya mwaka 2018 kuhusu viashiria vya maendeleo jumuishi limeiweka Tanzania katika nafasi ya kwanza Barani Afrika kwa kuwa na uchumi jumuishi. Taarifa hii kimsingi inaonesha namna ambavyo Tanzania inayapa kipaumbele na kuyashughulikia masuala ya usawa ikiwemo usawa wa jinsia.
Kufuatia Mkutano wa Nne wa Dunia kuhusu Wanawake uliofanyika Beijing China mwaka 1995, masuala ya jinsia na uwezeshaji wanawake yameendelea kupewa msukumo mkubwa zaidi. Katika kutekeleza Maazimio ya Ulingo wa Beijing, Tanzania imeyapa kipaumbele maeneo makuu manne ambayo ni: kuwawezesha wanawake kiuchumi na kuondoa umasikini; elimu, mafunzo na ajira kwa wanawake; ushiriki wa wanawake katika uongozi na ngazi za maamuzi; na kujenga uwezo wa wanawake katika masuala ya Sheria na haki za binadamu. Baadhi ya mafanikio yaliyopatika katika utekelezaji wa maeneo haya ni pamoja na:
Kuwezesha wanawake kiuchumi kupitia mikopo na mafunzo inayotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake, Benki ya Wanawake Tanzania na Mifuko mingine ya uwezeshaji wanawake kiuchumi.
Mfano, kuanzia mwaka 2015 wakati Serikali ya Awamu ya Tano ilipoingia madarakani hadi mwaka 2017 mikopo yenye thamani ya shs. 13,658,230,324.57 Erasto Ching'oroimetolewa kwa wanawake 772,075 waliojiunga katika vikundi vya kiuchumi wengi wao wakiwa wanawake wa vijijini.
Kwa upande wa elimu na mafunzo, Tanzania imefanikia kutoa elimu ya msingi na sekondari hadi kidato cha nne bila malipo na kuwezesha kufikiwa kwa uwino 1:1 kwa wanafunzi wasichana na wavulana katika shule za ngazi husika.
Tanzania imeridhia Itifaki ya Maendeleo na Jinsia ya Jumuia ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika inasisitiza ushiriki wa wanawake katika ngazi za Maamuzi kwa asilimia 50. Kutokana na utekelezaji wake Tanzania imefanikiwa kufikia asilimia 37 ya wanawake Bungeni, asilimia 41 wanawake majaji na asimia 30 wanawake madiwani. Aidha kutokana na jitihada hizi wanawake wanaendelea kuaminika na kuchukua nafasi za juu za uongozi na maamuzi ikiwemo nafasi ya Makamu wa Rais na Uspika.
Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki ya kisheria kwa wanawake ili kuwawezesha kupata haki zao za masingi ikiwemo kuzifanyia marekebisho sheria mbalimbali, kutunga sheria zinazowezesha upatikanaji wa haki kwa wanawake na kutoa mafunzo na msaada wa kisheria kwa wanawake.
8.0 HITIMISHO
Mwisho, nawaomba wanahabari wote nchini kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuimarisha usawa wa jinsia na uwezeshaji wanawake wa vijijini kwa kukuza uelewa wa jamii kuhusu umuhimu na mchango wa kundi la wanawake wa vijijini katika nyanja mbalimbali ikiwemo kijamii, kiuchumi, kisiasa na kiutamaduni. Aidha, kila mkoa utaadhimisha Siku ya Wanawake Duniani kwa kuzingatia mazingira yake.
Nawatakia maadhimisho mema ya Siku ya Wanawake Duniani Watanzania wote ambayo kilele chake kitakuwa siku ya tarehe 8 Machi, 2018 na Kaulimbiu inayoongoza maadhimisho haya ni ‘‘KUELEKEA UCHUMI WA VIWANDA: TUIMARISHE USAWA WA JINSIA NA UWEZESHAJI WA WANAWAKE VIJIJINI”.
AHSANTENI SANA KWA KUNISIKILIZA

No comments:
Post a Comment