TANGAZO


Tuesday, March 6, 2018

MADIWANI WA MANISPAA YA TABORA WAPONGEZWA KWA UMOJA WAO

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Agrey Mwanri

Na Tiganya Vincent, RS TABORA
6 March 2018
BAADHI ya Vyama vya Siasa Mkoani Tabora vimelipongeza Baraza la Madiwani la Halmashauri ya Manispaa ya Tabora kwa kutokauwa na makundi na kuwa na mshikamano na umoja wakati wa uendeshaji vikao vyake.

Kauli hiyo imetolewa jana na viongozi mbalimbali wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF) walioalikwa kuhudhuria kikao maalumu cha Baraza hilo.

Katibu wa CHADEMA Wilaya ya Tabora Msabaha Kambambovu alisema uendeshaji wa kikao cha Baraza Madiwani wa Manispaa ya Tabora  na uchangiaji wa Madiwani umeonyesha kuwepo na umoja miongoni mwao licha ya viongozi hao kutoka Vyama tofauti vya kisiasa.

Alisema katika muda wote alipokuwa ndani ya ukumbi wa mikutano hakuona zomeazomea wala mjumbe kukatazwa kuchangia kwa sababu ya utofauti wake wa kisiasa.

Kambambovu alisema ni vema waendeleze mshikamano huo kwa ajili ya maslahi mapana ya kuwasaidia wakazi wa Manispaa ya Tabora.

Naye Mwenyekiti wa CUF Wilaya ya Tabora Mirambo Camil alisema kama ni mgeni wa Madiwani waliopo katika Baraza hilo unaweza kudhani wanatoka Chama kimoja kwa jinsi walivyokuwa wakishirikiana katika uchangiaji wa hoja mbalimbali.

Alisema umoja huo utasaidia kuijenga Tabora mpya ambayo itapeleka miradi ya maendeleo katika maeneo yote bila kujali nani Diwani wa Kata husika anatoka upinzani.

Naye Mtahiki Meya wa Manispaa ya Tabora Leopold Chundu aliwataka Madiwani wote kuendeleza Umoja na mshikamano ili waweze kusaidia katika kuwaletea maendeleo wakazi wa eneo hilo.

Alisema kuwa hata Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli anasema maendeleo hayana Chama kwa hiyo ni vema wakaendeleza umoja ili kuwaletea maendeleo wananchi.

Katika hatua nyingine Baraza la Madiwani la Manispaa ya Tabora  limepitisha mapendekezo ya marekebisho ya bajeti ya ruzuku ya miradi ya maendeleo ya miundombinu (LGCDG) ya bilioni 1.3 kwa ajili ya mwaka huu wa fedha (2017/18).

Mapendekezo ya marekebisho ya bajeti hiyo yaliwasilishwa jana Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri hiyo Bosco Ndunguru katika kikao cha dharura cha Baraza hilo.

Alisema wameamua kufanyika marekebisho hayo kufuatia agizo la Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa za kuzitaka Halmashauri zote nchini kufanyia uchambuzi upya bajeti za miradi ili kuwa na michache inayotekelezeka na kukamilika kwa wakati na kwa asilimia 100.

Mkurugenzi huyo Mtendaji alisema kuwa inalenga kuongeza wingi na ubora wa huduma za jamii na miundombinu pamoja na kuwezesha utawala bora.

Ndunguru alisema miradi itakayotekelezwa ni ile inahusu sekta ya afya na elimu ambayo ujenzi wake umefikia katika mtambaa panya na miradi hiyo inatakiwa kukamilika kabla ya mwaka huu wa fedha kumalizika.

Aliongeza miradi mingine itatekelezwa katika Bajeti ya mwaka ujao wa fedha kulingana na upatikanaji wa fedha

No comments:

Post a Comment