Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri
Na Tiganya Vincent
RS-Tabora
22 Januari 2018
KANISA la Tanzania Assemblies of God (TAG) mkoani Tabora limeanza kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kupanda miti mbalimbali ikiwemo mikorosho ikiwa ni sehemu ya kutunza na kuhifadhi mazingira.
Kauli hiyo ilitolewa jana wilayani Uyui na Mkurugenzi wa Taifa wa Idara ya Elimu wa Kanisa la TAG Jonas Mkoba wakati wa zoezi la upandaji miti ikiwemo mikorosho liliongozwa na Askofu Mkuu wa TAG Askofu Dkt Barnabas Mtokambali na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri.
Alisema kuwa wameshanunua kilo 10 za mbegu ya mikorosho ambapo wanatarajia kuiotesha kwa ajili ya kupanda ekari 30 katika eneo hilo kama sehemu ya kuitikia agizo la viongozi wa Serikali la kuwataka kulima katika Mkoa wa Tabora zao la korosho kama zao la biashara.
Askofu Mkuu wa TAG Dkt Barnabas Mtokambali alisema kuwa Kanisa linaunga juhudi zote za Serikali za uhifadhi wa mazingira kwani maagizo ya Mwenyezi Mungu la kuwataka wanadamu walime na kuitunza nchi kwa kutunza mazingira.
Alisema kuwa upandaji wa miche ya mikorosho utawawezesha kupata zao la biashara na kupata miti inayohifadhi mazingira.
Kwa upande wa Mkuu wa Mkoa Mwanri alilipongeza Kanisa la TAG kwa hatua zake za kuanga mkono kampeni za Serikali za kuanza kupanda miti mbalimbali ikiwemo mikorosho.
Alisema kuwa hatua hiyo sio tu inasaidia katika utunzaji na uhifadhi wa mazingira pia inatekeleza agizo la Waziri Mkuu lakuwataka wakazi wa Mkoa wa Tabora kuanza kupanda mikorosho katika eneo yao ikiwa ni sehemu ya kujipatia kipato chao na Serikali kupata kodi.
No comments:
Post a Comment