Kauli hiyo imetolewa na washiriki wa mafunzo ya Elimu ya afya ya Uzazi na Elimu kwa mtoto wa kike yanayoendelea Micheweni, Kisiwani Pemba.
Wakichangia mada ya Afya ya Uzazi, iliyotolewa na Mkuu wa Elimu ya Afya Wilayani Micheweni, Sulemani Faki Haji, mshiriki kutoka Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali anayeratibu masuala ya Jinsia, Hidaya Khamisi amesema kwamba takwimu za udhalilishaji za hivi karibuni zinaonesha Kisiwa cha Pemba hususan Wilaya ya Wete inaongoza kwa asilimia 70 kwa vitendo vya ulawiti na ubakaji.
Kikundi kazi cha wanafunzi na akina mama kikifanya zoezi la kuwapima uelewa wao kuhusu somo walilopewa na malengo ya mafunzo hayo katika shule ya Sekondari ya Chwaka Tumbe, Micheweni, kisiwani Pemba.
Amesema vitendo hivyo vinasababisha fedheha katika jamii na kukatisha ndoto za mtoto kufikia malengo yake maishani.
Wakionyesha ukubwa wa tatizo washiriki wamesema kuwa kwa hivi sasa si shuleni, kwenye madrasa wala nyumbani ni mahali salama kwa watoto wa kiume na wa kike kwani kwa sababu si ajabu kumwona mtu anayeheshimika katika jamii hususan mzazi wa kiume akifanya mapenzi na watoto wake wa kuwazaa na kuwapa mimba huku walimu wa dini kuwadhalilisha watoto.
Hivi karibuni mkazi mmoja wa shehia ya Kiungoni Kimango, Hamad Omari Hamad mwenye miaka 56 alikamtwa na polisi kutokana na vitendo vya ubakaji alivyowafanyia watoto wake watatu akiwemo mtoto mdogo wa miaka minne na mmoja wao kupewa mimba na baba huyo. Kipindi cha mazoezi cha kuendesha mahojiano kwa ajili ya kupata habari kati ya Mtangazaji wa Redio Jamii Micheweni, Time Khamis na Mkuu wa Kitengo cha Elimu ya Afya ya Kujamiiana na Uzazi wa Mpango, Wilaya ya Micheweni, Pemba Dk. Suleiman Faki Haji. Mahojiano hayo ni miongoni mwa vielelezo katika mafunzo ya Elimu ya Kujamiiana na Uzazi iliyofanyika Micheweni, Pemba yenye lengo la kuwapa ujuzi stadi wanafunzi wa Shule nne za Sekondari na kikundi cha akina mama wilayani Micheweni, kutayarisha vipindi vya redio vinavyohusu masuala yao.
Kwa mujibu wa Mratibu wa Masuala ya Jinsia, Hidaya Khamisi, kuna mtandao ujulikanao kama cheni ridhia unaendelea katika baadhi ya shule Kisiwani Pemba wa watoto kwenda kufanya vitendo viovu iwe kupiga punyeto, kufanya ngono au kulawitiana.
Utafiti uliofanyika wilaya ya Wete mwaka 2016 kuhusiana na masuala ya unyanyasaji wa watoto iligundulika kwamba darasa zima lenye watoto 60, walisema kwamba wanataka wawekewe mazingira ili wasidhalilishwe kwa sababu watoto wote darasa hilo wamefanyiwa vitendo vya udhalilishaji hususan kulawitiwa.
Aidha ripoti nyingine kutoka shule moja wilayani Micheweni kwa mujibu wa Meneja wa Kituo cha Redio Jamii Micheweni, Ali Kombo imeonyesha kwamba kati ya wanafunzi 60 ni wanafunzi 10 tu ambao walikuwa bado hawajafanyiwa udhalilishaji wa kingono.
Mafunzo ya Elimu ya afya ya Uzazi na Elimu kwa mtoto wa kike yanayoendeshwa na UNESCO yana lengo la kuunda Vikundi vya Vijana Shuleni na Akina Mama Watayarishaji Vipindi vya redio kwa kushirikiana na Redio Jamii Micheweni, ambavyo vitasambaza Elimu rika kwa Vijana na Akina Mama.
No comments:
Post a Comment